Siri ya Barclays kujiengua Afrika, ila inabaki Tanzania

04Mar 2016
Na Waandishi Wetu
Dar
Nipashe
Siri ya Barclays kujiengua Afrika, ila inabaki Tanzania

WIKI hii imekuwa na taarifa nzito zinazogusa uchumi wa Bara Afrika, kwa benki maarufu duniani kuondoa miradi iliyo nayo katika nchi 12.

Ni uamuzi ambao kwa namna moja au nyingine, jamii na uchumi kwa jumla ina maana kubwa katika maisha ya. Benki ya Barclays imekuwa barani humo kwa karne moja sasa.

Mchambuzi wa uchumi na raia wa Kenya, Philip Mwema akihojiwa juzi na televisheni ya BBC, anasema wateja waliozoea benki hiyo kwa miaka mingi, inakuwa vigumu kwao kujenga mazoea katika benki mpya katika kuwekeza fedha zao na huduma nyingine za kibenki.

Kwa Watanzania kuna mtazamo tofauti kidogo, kuhusu benki hiyo kujiondoa barani Afrika
Mkurugenzi Mtendaji wa Barcalys Tanzania, Kihara Maina, anakiri kuwapo taarifa za benki hiyo kusisitisha huduma zake, lakini anasema kuna mabadiliko ya msimamo, baada ya kutoka kwa taarifa ya mwaka wa fedha za tawi la Tanzania, kwamba Barclays itaendelea kufanya kazi kama kawaida.

Anasema benki hiyo imekuwa kimapato kwa asilimia 10 katika soko la Hisa la Afrika Kusini walikowekeza, sababu inayowafanya waendelee kutoa huduma zake.

“Napenda kuwaambia Watanzania kuwa tutaendelea kutoa huduma zetu kama kawaida, tena mara mbili ya hapo awali. Wale wote walioweka fedha zao Barclays waondoe hofu, ziko salama na wafahamu kuwa hatutafunga benki hii,” anasema.

Maina anasema wafanyakazi 500 wa benki hiyo nchini wataendelea na kazi kama kawaida na wapo katika mpango wa kuwashawishi kuendelea kubaki, baada ya taarifa hiyo kutoka.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Barclays Afrika, Maria Ramos, anaitetea benki yake kuwa bado ipo imara na itaendelea kutoa huduma zake katika sehemu nyingi barani.

Barclays ina historia kubnwa nchini Tanzania, kwani mwaka 1967 kutokana na Azimio la Arusha, ni miongoni mwa benki binfasi ziliizotaifishwa na kuunda mali zake zikaunda Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), iliyodumu hadi mwaka 1997.

Ni mabadiliko yaliyowezesha kuanzishwa benki nyingi nchini kama vile Benki ya Nyumba Tanzania (THB), Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), Benki ya Ushirika na Maendeleo Vijijini (CRDB) na kadhalika.

Baada ya mabadiliko ya kisera nchini mwaka 1985 na taifa kurudia sera huria, mwaka 1992 yalifanyika mabadilko ya kisheria kwa kuanzishwa Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha, ambayo imeshafanyiwa mapitio mapya mwaka 2006.

Ni sheria iliyofungua milango ya kuanzishwa benki binafsi na taasisi za fedha nchini na miaka kadhaa baadaye serikali ilibinafsisha benki zake, isipokuwa TIB.

NBC ilivunjwa na mageuzi hayo yaliyoendana na ubinafsishaji huo ndio uliozaa NBC 1997, ambayo mmiliki wake mpya mkuu ni kampuni ya ABSA ya Afrika Kusini, ambayo ni sehemu ya Barclays.

Wakati Barclays inatangaza kujiondoa, watendaji wake wakuu katika vipindi tofauti,
walikuwa wanaieleza Afrika kama soko lao kubwa linaloajiri ya watu 45,000 na kuna wateja milioni 12.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Barclays inaondoa asilimia 62.3 ya hisa zake barani Afrika, huku ikiacha kitendawili ni namna gani inaoanishwa na taarifa za kitaalam kwamba bara hilo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa.

Barclays iliingia barani Afrika mwaka 1925 na katika hisa zake za barani Afrika inamiliki asilimia 62.3 ya hisa zake zote, huku katika Afrika Mashariki ina hisa kubwa katika mataifa ya Kenya, Tanzania na Uganda.

Awali kabla ya uamuzi uliotangazwa na makao makuu ya kampuni hiyo nchini Uingereza, Barclays Afrika ilitangaza kupunguza hisa zake barani Afrika.

Nchi zingine zilizotangazwa kuuzwa mapema ni hisa katika benki zake za nchini Misri na Zimbabwe, ambako kunaelezwa uchumi wake si imara na inafanya kazi kwa hasara.

Miongoni mwa mambo ambayo benki hiyo imekuwa ikilalamikia ni kuanguka kwa masoko ya bidhaa mbalimbali barani Afrika mwaka jana na athari za kusuasua uchumi wa China, nchi ambayo inahusiana na uchumi wa Afrika kwa karibu.

Pia imeguswa na tatizo la fedha za nchi hizo zinashuka thamani kwa kasi, jambo linalodaiwa kuitia hofu Barclays katika biashara yake barani Afrika na hakuna ishara nzuri ya kuamka kibiashara.

Jingine lililoguswa ni takwimu za ukosefu wa ajira, ambayo imo katika orodha ya mambo yaliyoifanya Barclays ihofu, kwa maana ya kupungua idadi ya watu watakaoweka akiba benki.

Mbali na hoja hiyo inayojengwa, bado kuna nchi kama Nigeria, ni kinara wa uchumi Afrika,kutokana na kushamiri biashara ya mafuta yanayochimbwa nchini humo.

HOJA ZA BOSI MPYA

Muda mfupi baada ya kufanyika mabadauiliko kwa Barclays duniani kupata bosi mpya, Jes Stanley, ndani ya miezi sita ya uongozi wake kasi ya mabadiliko hayo ikashuhudiwa.

Katika falsafa yake ya kuleta mabadiliko makubwa ndani ya benki katika kipindi kifupi, anasma hivi sasa uchumi ulioko si imara katika baadhi ya sehemu barani Asia na Afrika, ambako rungu lake limeshatua rasmi wiki hii.

Hata hivyo inaelezwa kuwa
bado imeshindwa kuhimili ushindani wa benki zingine za kimataifa barani Afrika kwa kutumia vyema fursa za kukua uchumi wa nchi mbalimbali,

Miongoni mwa benki zinazotajwa kuishinda Barclays ni Standard na Ecobank ambazo zote zina matawi nchini Tanzania.

Kinachofanyika hivi sasa ni kwamba, mali zote za Barclays ziko katika mchakato unaendelea kuunganishwa katika hisa za kampuni kubwa ya benki barani Afrika, ABSA ambayo kwa sasa ndiyo mmiliki mkuu wa NBC (1997) ya nchini.

Mtendaji Mkuu Stanley anasema licha ya kampuni yake kumiliki zaidi ya asilimia 62 barani Afrika na huku mzigo wa madeni makubwa.

Anasema hivi sasa haja ya kuelekeza macho katika uwekezaji wea kuhamishia ni katika masoko ya nchi kama Russia na razil.

Jingine analosema mtendaji huyo mkuu ni kwamba, hisa zote za kampuni Barani Afrika zimewekezwa katika Soko la Hisa la Johannesburg, Afrika Kusini.

Anafafanua kuwa, thamani ya fedha za nchi hiyo - Rand imeanguka kwa wastani wa asilimia 40 tangu mwaka jana na haoni dalili ya uchumi wa nchi hiyo kutengemaa.

Inaelezwa kuwa, hisa za Barclays zilizoondolewa katika uwekezaji Afrika, zitapoingizwa sokoni kutahitajika mnunuzi wa kiasi cha Pauni za Uingereza Bilioni nne.

Kuna taarifa zisizo rasmi kwamba katika mchakato wa kuuza hisa za Barclays, taasisi ya rasilimali ya Afrika Kusini iitwayo, Public Investment Corporation inawania kuzinunua.

Wakati wenye hisa wengi katika matawi ya benki ya Barclays zilizosajiliwa katika nchi mbalimbali Afrika wakiwa na shaka kubwa juu ya usalama wa mitaji yao, makao makuu ya benki kwa kushirikina na mdau wake mkuu ABSA, wamewahakikishia wasiwe na shaka.

Nchini Tanzania Barclays ina jumla ya matawi 18, Mgawanyo wake ni Jijini Dar es Salaam kuna matawi 10; Arusha ina matawi mawili; na tawi moja katika kila miji ya Morogoro, Mbeya, Moshi, Dodoma, Iringa, Mwanza, Tanga na Zanzibar.

Imeandikwa na Peter Orwa na Mary Geofrey

Habari Kubwa