Sita wanaotajwa kumrithi Emery

02Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Sita wanaotajwa kumrithi Emery

MIEZI 18 baada ya kumtea Unai Emery kuwa kocha wake, klabu ya Arsenal imeamua kuachana na mwalimu huyo, baada ya kupata matokeo mabaya dimbani.

Unai Emery

Kibarua cha Emery kilifikia tamati Ijumaa baada ya Washika Bunduki hao kucheza mechi nyingi zaidi bila ushindi tangu mwaka 1992, huku kichapo kutoka kwa Eintracht Frankfurt cha 2-1 katika mchezo wa Ligi ya Europa kikifikisha mechi saba bila ushindi katika mashindano yote.

Baada ya kutimuliwa, nafasi yake amepewa mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, Freddie Ljungberg ambaye atakuwa kocha wa muda.

Makala hii inakuchambulia makocha sita wanaopewa nafasi ya kuchukua mikoba ya Unai pale kwenye dimba la Emirates.

Carlo Ancelotti​

Kwa sasa Arsenal hawataweza tena kufanya haraka katika kutafuta kocha wa kikosi hicho, ili aweze kurudisha makali yao kwenye Ligi Kuu England.

Katika umri wake wa miaka 60, Ancelotti anaonekana kuwa kwenye nafasi nzuri ya kupewa mikoba hiyo hasa kutokana na ukweli kwamba, nyuma yake ana mafanikio makubwa.

Aliweka historia pale Chelsea huku sasa akiiongoza vizuri zaidi Napoli, ana nafasi kubwa ya kuchukua jukumu hilo.

Mauricio Pochettino

Licha ya kuwa na mafanikio makubwa pale Tottenham, Pochettino alitimuliwa baada ya timu hiyo kuwa na mwanzo mbaya zaidi wa Ligi Kuu.

Aliifanya Tottenham kuwa moja ya timu iliyoleta ushindani mkubwa zaidi kwenye Ligi Kuu England na pia kuifikisha fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita.

Kwa sasa Pochettino ni mmoja wa makocha bora zaidi Ulaya na kuna uwezekano mkubwa Arsenal wakaamua kutupa ndoano yao kumchukua. Lakini kushinda kwake kuipa taji lolote Spurs kwa kipindi cha miaka mitano aliyokaa pale, kunaweza kuwa changamoto kubwa kwake.

Freddie Ljungberg

Raia huyu wa Sweden amepewa nafasi ya kuwa kocha wa muda, lakini kama atakuwa na matokeo mazuri kwenye mechi zinazokuja, anaweza kupewa mkataba wa kuinoa timu hiyo angalau hadi mwishoni mwa msimu huu.

Licha ya kwamba hana uzoefu wa kutosha, akitoka kuifundisha timu ya Arsenal chini ya umri wa miaka 23, na baadaye kupandishwa kwenye timu ya wakubwa kumsaidia Emery, anaweza kuliongoza jahazi hilo vizuri.

Kama ataweza kuiweka kwenye nafasi nzuri katika kipindi chake hiki cha muda, Ljungberg anaweza kupewa mkataba wa kudumu wa kuinoa timu hiyo.

Nuno Espirito Santo

Kocha huyo wa Wolves, Santo amekuwa akihusishwa kwa muda mrefu na kupewa nafasi ya kuinoa Arsenal hata kabla Emery hajatimuliwa.

Ni rahisi kujua kwanini. Kuitoa Wolves toka daraja la chini na baadaye kusumbua kwenye Ligi Kuu na kufuzu Ligi ya Europa kwenye msimu wake wa kwanza, ni mafanikio makubwa kwake.

Katika umri wake wa miaka 45 anaweza kuwa chaguo sahihi kwa Arsenal katika harakati zake za kutaka kurudisha ubora wao.

Massimiliano Allegri

Huyu ni kocha wa daraja la juu kabisa duniani. Rekodi ya kushinda mataji mengi pale Juventus ni moja ya sifa kubwa aliyonayo kocha huyu, huku akipendelea zaidi timu yake kuwa na safu imara ya ulinzi.

Alifanya kazi nzuri akiwa AC Milan na baadaye Juventus, hivyo jina lake linapewa nafasi kubwa zaidi ya kuchukua mikoba ya kuwanoa The Gunners hao.

Mikel Arteta

Huyu ni kocha msaidizi wa Manchester City na amekuwa nahodha wa Arsenal wakati akicheza pale. Kabla ya Emery kuteuliwa kuwa kocha, Arteta ndiye alikuwa akipewa nafasi kubwa zaidi ya kuchukua mkoba ya kuinoa Arsenal.

Akiwa ametumia miaka mitatu akifanya kazi chini ya Pep Guardiola, hali hiyo inamfanya Arteta kuwa na uzoefu wa kutosha.

Pamoja na wasifu wake Arteta ndiye anayetajwa zaidi kupewa nafasi ya kuwa kocha wa Arsenal ili kuchukua mikoba ya Mhispania mwenzake, Emery.

Habari Kubwa