Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu kupaisha wanafunzi

09Aug 2016
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu kupaisha wanafunzi

ELIMU ina mchango mkubwa katika kumuwezesha mtu kupata mafanikio ya uhakika katika dunia ya leo. Elimu inayomwezesha mtu kujitambua, kuyatambua mazingira,kukabili changamoto na kujimiliki mwenyewe.

waziri wa elimu, profesa joyce ndalichako.

Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda, Februari 7, 2014, alizindua mpango wa Serikali wa kukuza Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu ujulikanao kama KKK akiwa katika Chuo Kikuu cha Dodoma-UDOM.

Akizindua mpango huo wa KKK wa miaka mitatu alisema kuwa utawasaidia wanafunzi wa kati ya miaka mitano -13 unalenga kuwafikia watoto walio katika mfumo rasmi na wale walio katika vituo vya elimu nje ya mfumo huo.
Matokeo makuu yanayotarajiwa katika mpango huu ni Kukua kwa Stadi KKK kwa watoto walengwa.

Mpango wa KKK unafadhiliwa na Ushirika wa Kimataifa wa Elimu-GPE, Shirika la Maendeleo la Uingereza-DFID kupitia mradi wa EQUIP-T, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mtoto-UNICEF pamoja na Shirika la Maendeleo la Marekani-USAID

Pinda alieleza kwamba ili utekelezaji wa Mpango huo uweze kufanikiwa ushirikiano wa wadau mbalimbali unahitajika.

Kama hiyo haitoshi, mpango huo uhusishe watu wote kuanzia Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Mashirika ya Kiserikali, Mashirika yasiyo ya Kiserikali na Wakereketwa wote wa elimu.

Aliyewahi kuwa Rais wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela, aliwahi kusisitiza umuhimu wa elimu kwa maendeleo ya jamii,

“...Elimu ni injini kubwa ya maendeleo ya mtu. Ni kupitia elimu ndipo binti wa mkulima mdogo anaweza kuwa daktari bingwa, kwamba mtoto wa kibarua wa mgodini anakuwa Mkuu wa Mgodi, na mtoto wa kibarua wa mashambani anakuwa Rais wa taifa kubwa”.(Mandela, 1991).

MIKAKATI YA SERIKALI

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako wakati akifungua warsha la uzinduzi wa taarifa ya hali ya KKK kwa wanafunzi wa darasa la kwanza na pili kwa mwaka 2016, alisema kuwa, serikali inatarajia kupokea msaada ya dola za Marekani milioni 35 ( Tsh. bilioni 75.34 ) kutoka kwa wahisani wa kimataifa lengo ni kusaidia mpango wa KKK kwa shule za msingi.

Prof. Ndalichako alisema hali ya KKK kwa wanafunzi wa shule za msingi kwa mwaka huu umeimarika ikilinganishwa na mwaka 2013 wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) hali ilikuwa mbaya.

Utafiti walioufanya kwa shule za msingi 650, alisema kuwa wanafunzi zaidi ya 7,000 walifanyiwa majaribio ya KKK na kubainika kuwa uwezo umeongezeka.

Jitihada za serikali za kuinua kiwango cha KKK kwa wanafunzi,alisema kuwa kinaungwa mkono na wahisani wa elimu wa kimataifa kutoka nchi za Sweden, Marekani, na Uingereza.

"Wahisani kutoka Sweden wametuahidi kutupatia dola za Marekani milioni saba (Sh. bilioni 15.068) na Shirika la DFID la Marekani watatoa dola za Marekani milioni 20 (Sh.bilioni 43.05), Benki Kuu ya Dunia (WB) watatoa Dola za Marekani milioni nane (Sh. bilioni 17.22).

Kwa mujibu wa Waziri, katika utafiti huo walikuwa wanawapa mtihani wa kusoma wanafunzi lengo halikuwa kuwapima wanafunzi uwezo wa kusoma tu pia kusoma kwa haraka.

Tanzania imepata mafanikio ya KKK, lakini mafanikio hayo hayatoshi kwa kuwa nchi bado inahitaji mafanikio mengi zaidi, alisema katika utafiti huo uwezo wa Kusoma kwa wanafunzi umeongezeka kulinganisha na uwezo wa Kuhesabu

Alisema mikakati ya serikali ni kuinua ubora wa elimu kwa kuimarisha KKK, kujenga misingi mizuri ya ufundishaji kwa kuchapisha vitabu na kuvisambaza nchi nzima, kutoa mafunzo kwa waalimu wanaofundisha KKK.

Prof. Ndalichako anasema pia kutoa mafunzo kwa waratibu wa elimu wa kata, wakuu wa shule lengo ni kuimarisha KKK, pia kuwashirikisha jamii kwa kuwapa elimu.

KATIBU MKUU ELIMU

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Leonard Akwilapo anasema serikali ilianza mikakati ya kuboresha KKK kwa kubadilisha mitaala ya ufundishaji wa wanafunzi wa shule za msingi kwa kuwapunguzia wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili idadi ya masomo anayosoma na kubakiza masomo ya KKK.

Ili elimu iweze kuleta mabadiliko ya kweli kimaendeleo ni lazima iwe elimu bora- inayolenga kumbadilisha mtu na kumwezesha kufikiri, kubuni, kujitambua, kuhoji, kudadisi, kupenda kazi, kuwa na mwenendo mwema na kuboresha afya, maisha yake binafsi na ya jamii.

Alisema elimu ni ukombozi iwapo italenga kumpatia mtu uwezo wa kupambana na changamato zinazoikabili jamii na taifa kwa ujumla.

"Elimu inamjenga mtu kuwa raia makini na mzalishaji ndani ya nchi yake," alisema Dk Akwilapo

Alisema Mpango wa Serikali wa KKK unalenga kuboresha elimu katika madarasa ya chini hivyo ni rahisi kuleta matokeo mazuri kwa sababu watoto watajifunza wangali wadogo.

“Kuna msemo usemao Mtoto mkunje angali mbichi, hivyo kwa kutekeleza KKK katika madarasa ya chini ni sawa na kumkunja mtoto angali bichi,” .

Kimsingi huu ni wakati mzuri wa kumkunja mtoto angali mbichi kwa kuwa Mpango huu utaweka msingi wa watoto wakiwa katika madarasa ya chini.