Sudan yavuna ilichopanda Janjaweed wakitwaa hatamu Baraza la Kijeshi

12Jun 2019
Ani Jozen
DAR
Nipashe
Sudan yavuna ilichopanda Janjaweed wakitwaa hatamu Baraza la Kijeshi

UMMA wa Sudan umeanza kujitafakari nini hasa kinatokea nchini humo baada ya kukwama kwa juhudi za kuunda serikali ya mpito inayoongozwa na raia, licha ya kuwa na wajumbe wengi wa Baraza la Kijeshi linalosema ni la mpito hadi ufanyike uchaguzi mkuu.

Jenerali Mohamed Hamdan “Hemeti” Dagalo, Naibu Mkuu wa Baraza la Kijeshi linaloongoza Sudan kwa hivi sasa.PICHA: MTANDAO

Baada ya pande hizo mbili kukwama katika kuamua nani ataongoza chombo maalum cha utawala (hasa ni baraza mchanganyiko), inaelekea kuwa watendaji katika Baraza la Kijeshi wamefikia uamuzi kuwa kutumia nguvu ndiyo njia ya kumaliza mvutano huo.

Viongozi wa maandamano walisakwa na zaidi ya waandamanaji 100 kuuawa, huku ikijitokeza kuwa kundi la Janjaweed linatenda hayo.

Kundi hilo linajulikana nchini humo kwa jina la kijeshi (kitaaluma) la Rapid Support Forces, yaani vikosi vyenye uwezo wa kuwekwa katika medani ya vita kwa haraka, na wachambuzi wa habari wanasema ni kundi lile lile lililosikika dunia nzima kwa jina la Janjaweed.

Lilishutumiwa miaka zaidi ya 10 iliyopita kwa kuzingira makazi na kunyang‘anya mali, kuua watu wengi katika eneo la Darfur, wakilizingira kwa kutumia askari wanaopanda farasi na kusomba watu bila kufuata utaratibu wowote wa kisheria.

Mkuu wa kundi hilo sasa ndiye naibu mwenyekiti wa Baraza la Kijeshi linalotawala sasa, na amekuwa msemaji wake, kuainisha umuhimu wa vikosi vyake katika mazingira ya Sudan hivi sasa, ambako sehemu ya jeshi la kawaida inawajali watu.

Mashambulio yaliyofanywa na vikosi vya jeshi na vikosi maalum vya medani ya vita (nusu mgambo na kwa upande fulani kuna makomandoo miongoni mwao) ilishtua dunia wakati ilipoonekana kuwa wako waliouawa kwa risasi wakati wa maandamano, na wengine kuonekana tu wakielea katika mto wa Nile.

Ni watu waliotafutwa maeneo tofauti, hata majumbani kwao wakati wa usiku, wakateswa kwa muda kupata habari za usimamizi wa maandamano, wakapigwa risasi na kutupwa katika mto, hali iliyoishtua dunia kuwa jeshi la Sudan linaandaa umwagaji damu wa kina ili maandamano yaishe. Bado mwanya haujaonekana katika hali hiyo.

Dhamira ya utawala wa kijeshi kufuata mwelekeo wake huo ilidhihirika bila kificho wakati watawala walipomruhusu Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia kufika nchini humo kujaribu kupata usuluhishi akaongea na viongozi wa upinzani, halafu wajumbe wa Baraza la Kijeshi.

Punde, viongozi wa waandamanaji walioshiriki walikamatwa, angalau baadhi yao, ingawa haikutajwa kama kuna aliyeuawa hadi sasa, baada ya kushiriki majadiliano hayo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje alisema labda juhudi za kutafuta muafaka zitafanikiwa; labda, labda.

Miili iliyoopolewa kutoka Mto Nile ilifikia 40 kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Madaktari wa Sudan (moja ya asasi muhimu za kuratibu maandamano hayo), ambako taarifa zilisema kuwa baadhi ya walioopolewa walikuwa wamejeruhiwa, wakatupwa mtoni na kufa.

Kuna hofu kuwa idadi ya waliouawa na hata kutupwa mtoni inaweza kuongezeka siku zinavyopita, kwani kuna mkanganyiko mkubwa kuhusu watu kadhaa waliopo, na si rahisi kuthibitisha kila taarifa kuhusu mtu kuwa salama au kuuawa, kama mwili haujapatikana.

Lawama zote zinaelekezwa kwa kundi hilo la Janjaweed, linalofahamika kwa utamaduni wake wa ukatili na kutojali haki za binadamu katika kuendeleza malengo ya utawala wa kijeshi dhidi ya makundi yenye mwelekeo tofauti.

Pamoja na kuwa sehemu kubwa ya viongozi wa maandamano na sehemu kubwa zaidi ya waandamanaji wenyewe ambao wengi zaidi ni vijana, bado kuna tatizo la kitaasisi na kitamaduni kwani upande wa Kaskazini wa iliyokuwa Sudan kubwa ilikuwa upande wa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Jenerali Omar al-Bashir.

Ni kama vile wananchi wa rika la kati na vijana wanavuna walichopanda wazazi wao, kwa kujitofautisha na wakazi wa Kusini ya nchi, hasa kwa kuutukuza ‘Uarabu’ na kuubeza Uafrika, wakati lugha yenyewe ya Kiarabu imegawanyika vipande vipande, na si rahisi kusema kuwa kule Misri au Jordan wanawatambua kina Al Bashir kama ni Waarabu.

Viongozi wa waandamanaji wamebakiwa na silaha moja tu, yaani kuendelea na maandamano, kufunga barabara za jiji la Khartoum (na labda kwingineko nchini) na kutazamia kuwa nchi za nje zitaongeza msukumo kwa utawala wa kijeshi kuonyesha nia dhahiri ya kutoa madaraka kwa raia, ili kipindi cha mpito kisiwe cha kuimarisha udikteta.

Hasa ni kufufua ngome za u-Bashir na kusheheni Janjaweed katika ngazi tofauti za utawala nchini humo.

Hata hivyo si rahisi kuona kinachoweza kutokea kwani nchi za nje zimegawanyika, kwa mfano jirani Eritrea ni mtetezi wa mstari wa mbele wa Baraza la Kijeshi na kutoangalia vitendo vyake, ila kutoingiliwa kutoka nje.

Mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ulifanyika New York baada ya kuona hatua za kwanza za mazungumzo zinakwama, na kabla ya kupigwa risasi kwa waandamanaji na miili kuopolewa katika mto wa Nile.

Hapakuwa na muafaka wowote na hata taarifa ya kina ya mjadala haikutolewa, hali inayoashiria kuwa hapakuwa na pendekezo lolote lililoungwa mkono na wajumbe wengi, hata kama baadhi ya wanachama hasa wa kudumu wenye ‘kura ya turufu’ wasingekubaliana.

Ina maana juhudi za kuuingiza Umoja wa Mataifa zinaelekea kukwama bado.

Yako maeneo mengine ambako juhudi tofauti za kimataifa zinawezekana, tena si kwa diplomasia ila kwa mashtaka ya jinai, kwani baadhi ya watendaji na hasa msemaji wa Baraza la Kijeshi ni mmoja wa vinara wa kuendeleza vitendo vya kukiuka haki za binadamu hasa jimbo la Darfur wakati uliopita.

Ikiwa naibu mwenyekiti wa Baraza la Kijeshi ataendeleza mbinu za kuua wale wanaoandamana na kutupa mtoni baadhi kuwa funzo kuwa utawala wa kijeshi uko ‘ngangari kinoma,’ si vigumu kuona Mahakama ya Jinai ya Kimataifa (ICC) huko The Hague ikitaka afikishwe huko, pamoja na baadhi ya watu wake wa karibu.

Si ajabu vilevile vikwazo vya kina vikawekwa pamoja na kuwa yapo mataifa makubwa yasiyoweza kuafikiana kuchukua hatua hizo, zichelewe.

Kina cha umahiri na nafasi ya Janjaweed katika Baraza la Kijeshi la mpito inaonekana wazi katika itifaki ya kutoa matangazo ambako naibu mwenyekiti kimsingi ndiye msemaji, na pia rejea zote kuhusu baraza hilo linaainishwa kuwa mwenyekiti wake ni Jenerali Abdel-Fattah al-Bourhani na naibu mwenyekiti ni Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, wanayemwita ‘Hemeti’ ambaye pia ni kamanda wa RSF, vikosi maalum vya kupeleka mstari wa mbele.

Mstari huo wa mbele wa vita nchini humo sasa ni kupambana na waandamanaji, na hawatokani na wale ambao Janjaweed ilikuwa inawasaka maeneo ya Kusini hasa Darfur, ila wale ambao - katika kizazi kilichopita – walisimama pembeni wakiwasikiliza wapambe wa Rais Al Bashir wakijitetea.

Jambo la msingi katika msuguano huo ni kuwa Sudan tangu mwaka 1989 imeongozwa na utawala wa kijeshi ambao ndani yake wakuu wa makabila na koo nchini humo wanafanya maamuzi kuhusu bajeti na usimamizi wa sheria kwa jumla.

Ni baada ya kuanguka kwa utawala wa kijamaa wa Jenerali Jafaar el Nimeiri na kuingia kwa uzalendo wa siasa kali, kusafisha makundi yasiyotaka utawala huo. Sasa wazawa wenyewe wa Kaskazini wanataka demokrasia.

 

Habari Kubwa