Taasisi yawafungulia milango Watanzania  kusoma ng’ambo

20Jul 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Taasisi yawafungulia milango Watanzania  kusoma ng’ambo

KATIKA jitihada za kunyanyua elimu nchini kumekuwa na mbinu mbalimbali ambazo zinatumiwa na taasisi za serikali na zisizo za umma kuboresha ili kufikia azma hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Global Education Link (GEL), Abdulmalik Mollel.

Zote zikiwa na lengo la kuhakikisha elimu inakuwa imara, bora na endelevu.

Pamoja na jitihada hizo za serikali na taasisi nyingine  kuboresha elimu nchini, inaonekana wazi kuwa wazazi wengi wanapenda kuwapeleka watoto wao nje ya nchi kusoma wakiamini kuwa huko kuna mazingira mazuri na elimu bora zaidi.

Hakuna asiyefahamu kwamba kuwapo na elimu  na mazingira bora ya kumvutia mwanafunzi kusoma ndipo kutamfanya aweze kufaulu vyema masomo yake na kuipenda shule.

Katika kuliona hilo, Kampuni ya Global Education Link inayofanya kazi ya kuwatafutia wahitimu nafasi za kwenda kusoma katika vyuo vya nje ya nchi, inaeleza kuwa itaendelea kuifanya kazi hiyo kwa weledi.

Regina Lema ni Meneja wa Tawi la kampuni hiyo mkoa wa Dar es Salaam, anasema tangu kampuni hiyo ilipoanzishwa mwaka 2016 mpaka sasa imefanikiwa kuwapeleka wanafunzi zaidi ya 5000 nje ya nchi kwenda kusoma.

 

Lema anasema mwitikio wa wanafunzi kwenda kusoma nje ya nchi umekuwa mkubwa jambo ambalo limesaidia kuongezeka kwa wataalam wengi nchini.

Anasema mwitiko huo pia unatokana na ufaulu mzuri wa wanafunzi hao waliopata nafasi ya kusoma nje ya nchi.

Lema anasema kampuni yao imekuwa kiwafuatilia wanafunzi hao wanaokwenda kusoma nje kuanzia hatua ya ushauri, pamoja na kupita mashuleni kutoa elimu juu ya kozi gani wanaweza kusoma chuo kikuu.

“Sisi tumekuwa tukiwafuatilia wanafunzi wetu huku nje ya nchi wanapokwenda kusoma lakini pia wanapohitimu masomo tunaendelea kuwashauri pia,” anasema.

Anaeleza kuwa kila mwanafunzi anayechagua chuo cha kusoma nje ya nchi kupitia kampuni yao humfanyia mchakato wa udahili, utafutaji wa visa, hati ya kusafiria pamoja taaratibu nzima ya vibali vya serikali.

“Baada ya hapo sisi pia tunafanya mchakato wa kumtafutia tiketi na mara nyingi wanafunzi wetu hutumia ndege moja kusafiri unakuta wanafunzi 50 wanasafiri kwa pamoja wakiwa na wafanyakazi wetu wanne,” anasema.

Anaeleza kuwa wanafunzi hao baada ya kufika huko  huwapeleka hadi chuoni na wakishaanza masomo ndipo wafanyakazi hao wanarejea nchini kwa ajili ya shughuli zingine.

Lema anasema ili kujua anachokifanya mwanafunzi akiwa masomoni, wanamfumo maalum ambao humfatilia  kwa kuangalia matokeo yake ya mtihani, majaribio pamoja na mwenendo mzima wa maisha yake.

“Kipo pia kitengo kingine ambacho kazi yake ni kuhakikisha wanafatilia maendeleo ya siku kwa siku ya wale wanafunzi yaani namna wanavyofanya kazi zake darasani, kuchukua matokeo na kuwapatia wazazi na masuala mbalimbali ya kijamii wanayoyafanya huko,” anasema.

Kadhalika, pia wanao umoja wa wazazi wa wanafunzi wanaosoma nje ya nchi ambao umekuwa ukituma mwakilishi kuzunguka nchi mbalimbali ambazo wanafunzi hao wanasoma kwa lengo la kuangalia mienendo ya watoto wao.

KUHUSU MAHAFALI

Akizungumzia mahafali, Lema anasema mwaka huu kampuni hiyo kwa mara ya kwanza itafanya mahafali ya kwanza ya wanafunzi  waliosoma nje ya nchi kwa lengo la kuwahamasisha wanaoendelea kusoma kwa bidii na hao waliomaliza huwaunganisha na fursa za ajira.

“Wanafunzi hawa wameshamaliza kusoma huko nje na kufanya vizuri sasa wanarudi nyumbani wanafanyiwa mahafali mengine, hii tunaimani itawasaidia waliopo masomoni kujitahidi kusoma kwa bidii ili waje kuwasaidia wazazi,” anasema Lema.

Mahafali hayo ambayo yanatarajia kufanyika Agosti 11 mwaka huu yatawakutanisha wahitimu hao na waajiri ambao wanaamini watapata fursa ya kuwaona vijana hao namna walivyokuwa bora kisha kupendezewa kuwaajiri.

“Waajiri watakuwepo hivyo itakuwa ni rahisi kwao kuwapata watu wa taaluma mbalimbali waliosoma nje ya nchi, lakini pia wanafunzi hawa wataandika na kuandaa project zao ambazo zitawasaidia na wao pia kama wakipata watu wa kufanya nao kazi,” anasema.

Anasema kwa sasa kampuni hiyo imetanuka kutoka kuwapo katika mkoa mmoja hadi  kwenye mikoa mingine mitano ambayo ni Mwanza, Arusha, Dodoma, Mbeya na Zanzibar.

 

CHANGAMOTO

Meneja wa Tawi la Dar es Salaam, anasema moja ya changamoto wanayokumbana nayo ni uelewa mdogo wa wanafunzi kuhusu kozi anayotaka  kwenda kusoma jambo linalochukua muda mrefu kumuelewesha.

“Hii ni changamoto ambayo tunakumbana nayo, unakuta mtu anapomaliza kidato cha sita ndipo anaanza kufikiria cha kusoma jambo ambalo halitakiwi, “ anasema Lema.

Na ili kukomesha jambo hili tumekuwa tukizunguka mashuleni kutoa ushauri kwa wanafunzi na kuwaeleza ni kozi gani anaweza kusoma pindi anapomaliza elimu yake ya Sekondari” anasema Meneja Lema.

Anaeleza kuwa kwa miaka ya nyuma pia walikuwa wakikumbana na changamoto ya wazazi na wanafunzi kufikiri kuwa kwenda kusoma nje ya nchi ni gharama kubwa.

“Miaka ya nyuma changamoto hii ilikuwa kubwa sana ila sasa hivi tunashukuru inapungua kwani tunawaelewesha watu kuwa upo mkopo usiokuwa na riba ambao mzazi anaweza kukopa na kwenda kumsomesha mtoto wake nje ya nchi,” anasema.

 

Lema anasema changamoto nyingine ni kuchelewa kutoka kwa matokeo ya kidato cha sita hapa nchini hali inayochangia shughuli za kumfanya mtoto kwenda kusoma nje ya nchi kufannyika kwa muda mfupi.

“Matokeo yanachelewa sana kutoka hivyo inamlazimu mtoto kutumia muda mfupi kufanya udahili wa kusoma nje ya nchi na hii inakuwa mzigo hata  kwa mzazi kwakuwa wanakuwa hawajajiandaa,” anasema.

MALENGO YAO

Lema anabainisha malengo yao ni kuwa moja ya mawakala wakubwa duniani wanaowatafutia wanafunzi vyuo vikuu nje ya nchi vyenye ubora wa hali ya juu.

“Pia lengo letu si tu kuwapeleka watu kwenda kusoma nje ya nchi tunategemea na wenzetu huko waje hapa nchini ili na  wao waweze kusoma na kwa kulitekeleza hilo tayari tumeshafungua ofisi zetu China, Zambia na tunawakala Kenya,” anasema Lema.

Aidha, lengo lao jingine ni kuhakikisha jamii inaelimika hivyo watajitahidi kwa hali na mali wanafunzi wapate elimu bora.

WITO

Meneja Lema anatoa wito kwa wahitimu wote wa elimu ya sekondari kutembelea kampuni hiyo kwa lengo la kupata ushauri kuhusiana na chuo gani anaweza kusoma nje ya nchi.

“Tunafanya kazi na vyuo zaidi ya 500 nje ya nchi hivyo wanafunzi wasisite  kututembelea ili kupata ushauri au maelekezo.” Anasema Lema.