Tabora kuwa jangwa, chanzo kukata miombo

13Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
TABORA
Nipashe
Tabora kuwa jangwa, chanzo kukata miombo
  • Uharibifu watishia kukausha Ziwa Tanganyika

ONGEZEKO la ukataji miti, kilimo, kuchoma mkaa na ufugaji mkoani Tabora hususani Urambo na Kaliua, limechangia kutoweka misitu ya miombo yenye ‘lindimaji,’ na kuwa chanzo cha kushuka mno kiwango cha mvua hadi kuwa chini ya wastani uliokuwapo miongo kadhaa iliyopita.

Baadhi ya wakazi wa Urambo wakiangalia mti unaoteketea kwa moto kwenye Hifadhi ya Msitu wa Ulyankhulu mkoani Tabora, hivi karibuni. PICHA ZOTE: VERONICA MAPUNDA

Makala hii inayoandikwa kwa msaada wa Rainforest Journalism Fund na Pulitzer Center, inaeleza zaidi.

 

Kutokana na ukame kuna hatari wilaya za Urambo na Kaliua kuwa jangwa, licha ya jitihada kadhaa zinazofanywa na wadau kuidhibiti hali hiyo.

Shughuli za kukata miti ili kuandaa mashamba na kukausha tumbaku, kuchakata mbao, kuchoma mkaa ambao ni nishati mbadala wa umeme na gesi zinachangia kutoweka miti miombo.

 

Ofisa Misitu wa Wilaya ya Urambo, Jacob Mbeshi, anasema miti yenye ukubwa wa mita nane za ujazo inatumika kukaushia tumbaku iliyovunwa eneo la ekari moja inayokaushwa kwenye matanuru ya kisasa, wakati teknolojia ya kale inatumia miti zaidi.

Mkuu wa Idara ya Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Shadrack Yomba, anasema kabla ya mwaka 1990 maeneo mengi Tabora kama Urambo na Kaliua yalipata mvua kwa wastani usiopungua milimita 1,000, ikiwa ni matokeo ya kuwapo misitu mingi.

Anataja ongezeko la wahamiaji kwenye misitu ya wilaya hizo wakitokea Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Geita na Kigoma, kuanzia mwanzoni mwa 1990, kiasi hicho cha mvua kimepungua kufikia chini ya wastani wa milimita 870 kwa mwaka.

Anasema hatua hiyo imesababisha kuwapo joto kuliko unyevunyevu kama ilivyokuwa kabla ya mwaka 1990.

 

Pia, mtaalamu huyo wa masuala ya mazingira anasema kumekuwapo upotevu wa mimea ya asili hasa isiyostahimili ukame kwenye maeneo hayo.

 

KUHIFADHI MAZINGIRA

“Kuna jitihada kadhaa za uhifadhi zinazofanywa na serikali kama kuhamasisha wakulima kupanda miti, lakini zinaathiriwa na kipindi kirefu cha jua kali kinachosababishwa na kutoweka kwa misitu,” anasema Yomba.

Takribani asilimia 20 ya miti inayopandwa mashambani hukabiliana na ukame kwenye maeneo hayo ndiyo inayostawi na mengine hukauka anasema na kuongeza kuwa ukanda wa miombo unahusisha misitu iliyopo wilaya za Uvinza na Kibondo mkoani Kigoma, Mlele Katavi na mikoa ya Morogoro, Iringa, Lindi na Mtwara.

Mjumbe wa serikali ya Kijiji cha Igunguli wilayani Urambo, Eliud Luago, anasema miaka ya 1990, eneo hilo lilikuwa na mvua nyingi zilizochangiwa na kuwapo misitu ya miombo, lakini sasa ni kukame.

Aidha, anasema ardhi inapungua rutuba kutokana na kilimo cha tumbaku kinachohusisha ukataji miti kwa wingi na kwamba

kuna dalili za mabadiliko ya tabianchi kwenye maeneo yao, kama ilivyotokea msimu wa kilimo wa mwaka huu ambao kiwango cha mvua kilikuwa kikubwa na kuharibu mazao.

 

MSITU UNATOWEKA

Eneo linalotajwa kuathirika zaidi kwa ukataji ovyo wa miti ya miombo ni msitu wa Ulyankhulu uliopo wilayani Urambo, msitu huo wenye ukubwa wa hekta 229,600 ni miongoni mwa hifadhi za misitu ya wilayani humo inayojumuisha pia msitu wa Gereza la Kilimo Nsenda (hekta 2,380) na ile ya vijiji vya Kangeme, Itebulanda na Utenge -KIU ambacho ni kifupi cha majina ya vijiji hivyo, wenye hekta 846.5.

Awali, Halmashauri ya Urambo ilimiliki pia Hifadhi ya Msitu wa Ugala Kaskazini wenye ukubwa wa hekta 163,482.39 ambao umemilikishwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Ofisa Misitu Mbeshi anasema ingawa umilikishwaji huo umechangia kupunguza mapato kwa Halmashauri ya Urambo na kuondoa fursa za uvunaji mazao ya misitu kama asali, lakini utachangia jitihada za uhifadhi wenye tija kutokana na TANAPA kuwa na weledi wa usimamizi na uhifadhi wa maliasili ikiwamo misitu.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Urambo (wakati taarifa za makala haya zikikusanywa),  Sadoki Magesa, anasema asili ya msitu wa Ulyankhulu kuvamiwa na kugeuzwa makazi ya kudumu, kulitokana na kuingia kwa wahamiaji wakitafuta ardhi yenye rutuba na mvua za kutosha kwa ajili ya kilimo na ufugaji.

Anasema waliongezeka huku wageni wengine walioingia wakijitwalia maeneo na kupanua shughuli za kilimo hasa cha tumbaku, mazao ya chakula na ufugaji.

Magesa anasema umuhimu wa msitu wa Ulyankhulu upo kwenye lindimaji ambalo hukusanya maji yanayoingia mito Ugalla, Igombe na Malagarasi, maziwa Nyamagono na Sagala hadi Ziwa Tanganyika.

Jarida la Umoja wa Mataifa, ukurasa wa mtandaoni wa …stories.undp.org/lake-tanganyika-what-the-future-holds, ziwa Tanganyika ni miongoni mwa maziwa ya maajabu duniani, ni kongwe, lina kina kirefu barani Afrika, likitenganisha Burundi, Congo na Tanzania likinufaisha kiuchumi watu zaidi ya milioni 10.

Hifadhi ya msitu wa Mto Igombe uliopo wilayani Kaliua ni miongoni mwa maeneo yanayohitaji zaidi uoto wa miombo kutokana na kutegemea maji yanayotokea Ulyankhulu.

Hivyo, hatua ya wahamiaji kuingia na kuweka makazi kwenye hifadhi ya Ulyankhulu, inatarajiwa kuathiri pia upatikanaji mvua utakaochochea kukauka kwa vyanzo vya maji na kupotea kwa ekolojia ya eneo hilo.

Mratibu wa Wakala wa Huduma ya Misitu (TFS) wilayani Kaliua, Jackson Temu, anasema, Hifadhi ya Msitu wa Mto Igombe ilitokana na tangazo la serikali namba 32 la mwaka 1958, una ukubwa wa hektari 244,480 na ndicho chanzo kikuu cha maji ya bwawa la Igombe linalotumiwa na wakazi wa Manispaa ya Tabora na vijiji jirani.

Vilevile, anasema msitu huo una ardhi oevu ya Malagarasi inayohudumiwa na kusimamiwa na TFS katika wilaya za Kaliua, Uyui na Nzega mkoani Tabora.

Ofisa Miti wa Wilaya ya Kaliua, Bucheye Wambura, anasema, karibu kila eneo limechukuliwa na wahamiaji waovuna miti na rasilimali nyingine wanavyotaka na kusabibisha ugumu wa usimamizi.

 

ATHARI KIIKOLOJIA

 

Ofisa Misitu wa Wilaya ya Urambo, Jacob Mbeshi, anasema athari nyingine za kuharibu mazingira ni kupotea miti muhimu kama mninga ambayo kamati ya wilaya ya uvunaji iliweka zuio la kuivuna. Aidha, mti wa mkurungu ni miongoni mwa inayovunwa ovyo na kuharibu uoto wa asili wa miombo.  

 

WANYAMAPORI

Kwa upande mwingine, uharibifu wa misitu hiyo unatajwa kuwa chanzo cha kutoweka kwa wanyamapori ambao awali, walipatikana kwenye maeneo kadhaa.Wanyama hao ni tandala, kongoni, palahala, tohe, simba na twiga.

 

Wenyeji wa maeneo ya karibu na msitu wa Ulyankhulu wanasema, wanyama hao walihamia msitu uliopo Igombe na kuelekea Hifadhi ya Kigosi.

 

Shuhuda nyingine za wenyeji zinaeleza kwamba kuna nyakati simba wamekuwa wakitokea Kigosi walipotorokea, na kurejea Ulyankhulu kupitia eneo wazi linalosababishwa na kukata miti hadi Ugala, hatua inayoelezwa kuwa kuna hatari ya watu na mifugo kushambuliwa na wanyama hao.

 

MIFUGO NA UKAME

 Kishike Darushi, mfugaji aliyekuwa akilisha mifugo kwenye Hifadhi ya Msitu wa Ulyankhulu, anasema kuna ukame unaosababisha watembee umbali kusaka maji na malisho, aidha hakuna kivuli kutokana na kukata miti ovyo na wafugaji huchomwa na jua muda wote.

 

WAVAMIZI KUSAJILIWA

Licha ya kudaiwa kuvamia na kuweka makazi, wahamiaji hao walifanikiwa kusajili makazi yao na kupata hadhi ya vijiji rasmi, wakifikishiwa huduma za kijamii kama shule, zahanati na umeme, ingawa baadaye, vyeti vya usajili vilirejeshwa kwenye halmashauri husika ili kufanyiwa uhakiki.

 

Vijijini vilivyopo Ulyankhulu na kata zake kwenye mabano ni pamoja na Ukwanga na Mlangale (Songambele), Unzali, Uyogo, Igunguli, Milambo, Igembensabho na Kasela (Uyogo).

 

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Magesa aliliambia Nipashe hivi karibuni kuwa Ulyankhulu ni miongoni mwa misitu iliyotangazwa hivi karibuni na serikali, kutumika kwa makazi na shughuli za kibinadamu.

 

“Tumepata taarifa ya serikali kuruhusu vijiji hivyo kuendelea kuwapo, lakini bado hatujapewa barua rasmi ya kiofisi,” Magesa anasema.

 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Igunguli ambacho ni miongoni mwa vilivyomo kwenye hifadhi hiyo, Lucas Lala, anasema kaya zenye takribani watu 6,545 kijijini humo wanatambua kuwa eneo hilo ni halali kwa makazi na shughuli za binadamu.

 

URASIMISHAJI MISITU

Kwa mujibu wa Ofisa Misitu wa Wilaya ya Urambo, Jacob Mbeshi, urasimishaji misitu ni  utekelezaji wa mradi wa miombo, uliofanyika kwa msaada wa  Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Global Environment Facility (GEF).

Habari Kubwa