Tafakari ya mvutano unaoendelea bungeni

22Jun 2016
Bangila Balinsi
Dar es Salaam
Nipashe
Tafakari ya mvutano unaoendelea bungeni

MAMBO yanavyoendelea katika vikao vya Bunge la bajeti ya serikali ya mwaka 2016/17 yanasikitisha. Kwa sababu inashangagaza kuona kwamba serikali iliyopo madarakani inaona ni sawa tu mambo kuwa kama yalivyo bila kuchukua hatua ya kurekebisha hali iliyopo.

Kitendo cha wabunge wa upinzani kususia vikao vya Bunge kwa sababu ya kutokuwa na imani na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, huku bunge likiendelea na mijadala ya bajeti likiwa na wabunge wa upande mmoja wa chama kinachounda serikali, kinatia shaka kama kweli matakwa ya utawala bora katika demokrasia ya vyama vingi yanazingatiwa.

Ili kuelewa kwamba hapa kuna tatizo kubwa la kiutawala yatubidi tutafakari tena mambo mawili muhimu katika utawala wa kidemokrasia: Je, Bunge lipo kwa maslahi ya nani?; na jambo la pili ni matakwa na mipaka ya demokrasia.

Tukiyatafakari mambo haya vizuri labda tutaona umuhimu wa kurekebisha mambo yanavyoenda.

Ili kujua bunge lipo kwa maslahi ya nani ni vyema tukajiuliza kwa nini kuna mabunge. Katika utawala wa kidemokrasia bunge lipo ili kurahisisha demokrasia iweze kutekelezeka katika jumuiya zenye watu wengi.

Kwa kuwa demokrasia ni utawala wa watu kwa ajili ya watu ingebidi kila kitakachofanyika watu wote wawe wamehusishwa. Huu ndiyo utawala wa demokrasia wa moja kwa moja.

Katika jumuiya yenye watu wachache au kikundi kidogo hilo la kupata maoni na maamuzi ya kila mmoja linawazekana, lakini kwenye watu wengi kama nchi hilo haliwezekani.

Sasa ili kuwezesha demokrasia itekelezeke kwenye jumuiya kubwa ya watu ndiyo demokrasia ya moja kwa moja ilitafutiwa mbadala wa demorasia wakilishi.

Katika mtindo huu watu wanajiunga katika makundi ambayo kwa hapa kwetu huitwa majimbo. Ni katika maana hii tunaona kwamba wawakilishi wanachaguliwa katika majimbo na aliyechaguliwa hujulikana kama mbunge, na jumuiko la wawakilishi wote hawa ndiyo huunda Bunge.

Kwa hiyo sasa ni rahisi kujibu swali letu kwamba bunge lipo kwa ajili ya wawakilishi wa wananchi na kazi ya wawakilishi hao ni kuwakilisha, kuangalia na kusimamia maslahi ya wananchi.

Watawala wanapata madaraka ya kuendesha nchi kwa niaba ya wananchi baada ya kutangaza sera zao juu wanayotaka kuyafanya kwa ajili ya wananchi. Kwa hiyo lazima kuwapo na chombo cha kuona kwamba watawala wanawajibika na wanatenda kadri walivyo ahidi.

Watawala ndiyo serikali na chombo cha kusimamia maslahi ya wananchi ni bunge.

Sasa katika muktadha huu ni jambo la ajabu kuona kwamba serikali inaleta mapendekezo muhimu ya inachotaka kufanya kwa mwaka kupitia bajeti huku ikianisha njia itakazozitumia kupata fedha za kufanyia kazi ili kufanikisha mipango yake halafu eti mwakilishi na msimamizi wa maslahi ya waliomtuma kutoka jimboni hayupo.

Ni jambo la kusikitisha kweli sana kwa sababu hata mwakilishai mmoja asipokuwapo ni vibaya kwa kuwa kuna watu hawakutendewa haki kwa kutokuwakilishwa. Kama hivyo ndivyo je, ni vibaya kiasi gani watu wa majimbo mia moja na ushehe kukosa wawakilishi katika mjadala unaogusa maisha yao moja kwa moja?

Ni jambo la kushanganza kuona kwamba kama wawakilishi hawa wamekosea na hawakutimiza wajibu wao kwa wananchi basi angalau serikali inayojua kwamba kuna watu waliyoiingiza madarakani kupitia kura ya urais, hawajawakilishwa, ingechukua hatua.

Kwa sababu kama serikali ingekuwa inajali utawala wa kidemokrasia na hasa demokrasia ya vyama vingi ingesitisha shughuli ili kutoa nafasi kwa pande mbili zinazopigana bugeni kuweka mambo sawa.

Lakini inaonekana serikali ya sasa haoni umuhimu hata ya wapinzani kuwepo na kuna mambo imekuwa ikiyafanya ili kuwadhibiti wasifanye chochote na hivyo kutoa picha kwamba inaminya demokrasia.

Kwa kutofanya juhudi zozote ili wawakilishi wa upande wa pili wa mawazo mbadala warudi bungeni ni dhahili utawala wa kidemokrasia umefifishwa.

Lakini kwa upande mwingine serikali inastahili kubebeshwa lawama kwa sababu mhusika mkuu wa mgogoro huu ni Naibu Spika ambaye aliipata nafasi hii kwa kilicholalamikiwa kuwa ni shinikizo kutoka serikalini. Malalamiko haya yanaweza kukubalika kwa sababu kuu mbili.

Sababu ya kwanza ni ukweli kwamba jimbo la Naibu spika wa sasa ni ikulu; jambo la pili linalotazamwa ni kwamba Naibu Spika hakuwa na uzoefu wa aina yoyote katika uendeshaji wa Bunge wakati wa kuchaguliwa kwake.

Katika hali ya kawaida hilo lilipaswa liwe gumu kama hakuna shinikizo la aina moja au nyingine kwa sababu waliokuwa wameomba nafasi hiyo kutoka hata katika chama chake wengine walikuwa na uzoefu wa kuendesha bunge kama wenyeviti wa bunge.

Sasa kunapotokea matatizo yanayoonekana kwamba wale wasiokuwa upande wa serikali wanakandamizwa na mlalamikiwa, mtu anaweza kupata sababu ya kuwasikiliza kama siyo kuwaamini kabisa.

Lakini hapa haina maana kwamba upande wa wawakilishi kufanya majukumu yao wako sahihi. Ukweli ni kwamba na wao wanastahili lawama kwa kutofikiria njia mbadala ya kuendelea na jukumu lao la uwakilishi huku wakitafuta ufumbuzi wa kutosikilizwa na Naibu Spika.

Kamati ya uongozi ya Bunge nayo haikwepi lawama katika sakata hili, wao waliangalia upande mmoja na wakashauri kitu kinachoonekana kama kukomoa pale waliporuhusu Bunge liendeshwe na Naibu Spika bila kupishana na wenyeviti wengine wa bunge kama ambavyo tumezoea ili ‘kuwakomesha’ wapinzani kwa sababu ni jambo ambalo lingewalazimisha kutoka nje kila siku.

Ufumbuzi wa mgogoro huu unaweza kupatika katika tafakari ya pili ambayo ni juu ya matakwa na mipaka ya demokrasia.

Ili demokrasia ifanye kazi katika jumuiya ya watu kuna mambo yanayotakiwa kujengeka kama utamaduni wa kidemokrasia. Jambo mojawapo na muhimu sana ni kwamba kila raia anatakiwa kuheshimu haki za wengine na kuheshimu utu wa kila mtu.

Jambo lingine muhimu katika utamaduni wa demokrasia ni lazima kila mtu atambue kwamba mpinzani wake kisiasa si mtu mwovu na asiyestahili kuwepo kwa sababu tu ana mawazo tofauti. Hapa jambo la kufanya ni kuyachukulia mawazo tofauti kama changamoto.

Haitakiwi kushikilia msimamo wako tu bila kuona upande wa wenzako. Lazima katika kujenga demokrasia tujue kuna upande mwingine wenye msimamo tofauti. Kwa hiyo bora kujipa nafasi kuona wema uliondani ya upande mwingine.

Jambo jingine muhimu sana ili demokrasia ifanyekazi, mtu anapotaka kitu chake na kuweka madai yake akumbuke kwamba katika demokrasia ni vigumu kila mtu kupata anachokitaka.

Demokkrasia inahitaji sadaka kwa hiyo mtu awe tayari kuachia baadhi ya anavyovitaka na kupata baadhi ili mradi kila mtu apate kitu kuliko kujaribu kila mtu kupata kila kitu anachotaka. Hapo hapatakuwa na muafaka.

Yapo mambo mengi ya namna hii yanayopaswa kujengeka kama utamaduni wetu wa demokrasia, lakini la mwisho na muhimu pia ni kwamba demokrasia si ya walio wengi tu. Lazima hata makundi ya wachache yasikiliwe.

Kuacha kusikiliza hoja za watu kwa sababu ni wachache hata kama hoja zao ni za msingi lazima kutaleteleza hao wasiosikilizwa kutafuta njia nyingine za kuwafanya wengi wakawasikilize na daima njia hizi ni za kuleta maafa.

Kutokana na tafakari hizi ni dhahiri kuwa mgogoro uliondani ya bunge unastahili kutafutiwa majibu haraka ili wananchi watendewe haki ya kuwakilishwa. Aidha, ni wazi pia kwamba ufumbuziwa mgogoro huu ni kwa pande zilizotofautiana kukaa mezani na kuzungumza kwa sababu hiyo ndiyo njia sahihi ya kidemokrasia ya kumaliza migogoro.

Jambo la kuzingatiwa na pande zote ni kwamba demokrasia haiwezi kukamilika bila kuwepo na utamaduni wa kuheshimiana, kusikilizana, kuvumiliana (kumbukeni ushauri wa spika aliyepita Mama Anna Makinda) na kuzunguza.

Pande zote zinapaswa kujua kwamba demokrasia inafanya kazi tu haya yakizingatiwa, ikiwa ni pamoja na watu kuheshimu tofauti baina yao na hivyo kuwa tayari kuzijadili na pengine kugawana madaraka.

Habari Kubwa