TAFIRI yafungulia Mwanza njia kupitia vizimba samaki Viktoria

26Nov 2021
Neema Emmanuel
Mwanza
Nipashe
TAFIRI yafungulia Mwanza njia kupitia vizimba samaki Viktoria
  • RC mstaafu, aliyepo waonyesha pa kutokea

HIVI karibuni serikali ilizindua Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano kuanzia 2021/22 hadi 2025/26, ukiwa na dhima ya kujenga Uchumi Imara Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.

Mtafiti Mwandamizi kutoka TAFIRI Mwanza. Hillary Mrosso, akieleza namna maabara ya kutengeneza chakula cha samaki inavyofanya kazi. PICHA: NEEMA EMANUEL.

Ni hatua yenye dhima ya kuchochea uchumi shindani, shirikishi na kuimarisha uzalishaji wa ndani na utoaji huduma, kukuza uwekezaji na biashara, kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu.

Katika Mpango huo utakaogharimu Sh. trilioni 114.8, serikali itachangia Sh. trilioni 74.2, huku sekta binafsi ikichangia Sh. trilioni 40.6.

Ni mpango unaozingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025, sera na mikakati kisekta na tafiti zilizofanyika nchini, pamoja na Dira ya Afrika Mashariki ya 2050.

KUTOKA MWANZA

Katika kuitikia jitihada hizo za kupambana na umasikini na ukosefu wa ajira, serikali mkoani Mwanza imejipanga kuwezesha miradi ya ufugaji samaki kwa vizimba ndani ya Ziwa Victoria, ili kuwawezesha wananchi kunufaika na ‘uchumi wa bluu.’

Ni mradi unaolenga kutumia fursa zilizopo kwenye ‘uchumi wa bluu’ utakaogharimu Sh. bilioni 1.9 ili kuwasaidia vijana na kada nyinginezo kujiajiri na kunufaika kiuchumi, pamoja na kuboresha maisha ya jamii.

Takwimu zinaonyesha, tangu mwaka 2016 jumla ya vizimba 109 vya ufugaji samaki vilijengwa ziwani Victoria na kwa sasa vimefikia vizimba 431 vinavyomilikiwa na wafugaji 28.

Hillary Mrosso, mtafiti mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Samaki Tanzania (TAFIRI), akiwasilisha taarifa yake kwenye mafunzo ya namna ya kuandaa na kuwasilisha taarifa za sayansi, teknolojia na ubunifu kwa watafiti na waandishi wa habari, anaeleza njia zilizochukuliwa.

Katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), anasema duniani kote ufugaji samaki ndio njia mbadala wa kuzalisha samaki, ili kuziba pengo litokanalo na kupungua samaki wa asili.

Mrosso anafafanua, mseto wa ufugaji samaki na kilimo ni eneo lenye fursa ya kukuza ‘uchumi wa bluu’ ambako uzalishaji vyanzo mbadala vya protini ya kulishia samaki, unahitaji kufanyiwa tafiti.

Anatoa takwimu, vifaranga waliozalishwa wako 313,215 wenye bei ya wastani na kuna wafugaji 119 wamenufaika na mbegu bora ya samaki, pia wamepata mafunzo na ushauri nasaha kuhusu ufugaji bora wa samaki.

Matokeo yake ni kuongezeka uzalishaji samaki kupitia ufugaji utakaoziba pengo la upungufu wa samaki wanaovuliwa katika maji ya asili na kukua uwezo wa taasisi katika uzalishaji mbegu na vyakula bora vya samaki kwa ajili ya wafugaji.

Anasema, TAFIRI inalenga kushirikiana na wadau wa ukuzaji viumbe maji katika utekelezaji miradi katika Kanda ya Ziwa, ili kuhakikisha gharama za mradi zinachangiwa kupitia mauzo ya mbegu na vyakula vya samaki vinavyozalishwa.

SHIDA KATIKA MABWAWA

Anazungumzia shida zinazowakabili ni kukosekana uzio katika eneo la mabwawa, kwani wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la wezi wanaovamia maeneo hayo na kuiba samaki.

Pia, anataja miundombinu chakavu, upungufu katika maabara ya ubora wa maji na viumbe wala samaki kuvamia mabwawa watakofugia.

"Tumeomba ufadhili COSTECH wa kulikarabati jengo la utafiti wa mbegu kwa sababu nilazamani pamoja na kuboreshewa mfumo wa tanki la kusukuma maji, kwa sababu maji yanaposhuka hayaingii kwenye tanki la chini kwa asilimia 100, "anaeleza 

HATUA ZINAZOCHUKULIWA

Mrosso anataja kuanzishwa vikundi vya ufugaji samaki aina ya sato wa jinsia moja kwenye vizimba, utapunguza changamoto ya ajira kwa vijana, kuwanufaisha kiuchumi na kimazingira.

Anasema sekta ya uvuvi, ufugaji wa samaki unahitaji kutumia teknolojia ya kisasa ya vizimba ambavyo vifaranga vya samaki vinawekwa ndani ya kizimba kilichotengenezwa madhubuti kwa ama chuma au plastiki, baada ya kutumbukizwa majini.

Mtafiti huyo anaeleza vifaa hivyo vinapaswa kuwa vyepesi, visivyopata kutu, visivyo na sumu na vinastahimili mabadiliko hali ya hewa.

Vilevile anafafanua, vifaa vinavyotumika kutengeneza vizimba hivyo vya maumbile tofauti ni pamoja na nyavu, mabomba, mbao, maboya, kamba na nanga.

RC MSTAAFU ACHANGIA

Mkuu wa Mkoa wa zamani wa Dar es Salaam na Kilimanjaro, Mecky Sadiki, anatoa uzoefu wake kwenye uwekezaji wa ufugaji samaki kwa vizimba, kwamba licha ya Tanzania kumiliki asilimia 53 ya Ziwa Victoria, bado haijanufaika nao kutokana na migongano ya sheria akilinganisha na nchi jirani.

Anasema ufugaji samaki vizimbani ‘unalipa’ na anawashauri watu wasiogope au kukatishwa tamaa na gharama za uwekezaji, kwani kuna soko la uhakika, ikiwamo malighafi ya kutengeneza chakula cha samaki.

“Kwa kutumia teknolojia hii, wavuvi haramu wataondoka wenyewe na huo ndio mbadala wa kumaliza uvuvi haramu. Tatizo hapa ni tozo kubwa, mfano Ukerewe kilo moja ya samaki inatozwa ushuru wa Sh.300,”anasema Sadiki.

Anafafanua utumiaji vizimba samaki ni bora na wa kisasa, kwa sababu eneo dogo linazalisha samaki wengi na suala la gharama mwanzo wa mradi hazikwepeki.

Sadiki anachanganua mtaji ulivyo, kwamba kizimba kinagharimu Sh. milioni 20, inayohusisha vifaranga 10,000, gharama za ujenzi na vibali vyote.

Anawashauri wanaotaka kufuga samaki kwa njia hiyo, waungane kwenye vikundi na kupata nguvu ya kuanzisha kizimba kimoja kisha wataendelea kuongeza vingine kadiri watakavyokua kibiashara na kusisitiza ufugaji huo unalipa, wasiogope gharama.

RC MWANZA

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, anasema mkoa huo kwenye ‘uchumi wa bluu’ bado haujafanyiwa kazi ya kina, ilhali malighafi na ziwa, nguvu kazi ipo ikiwamo ya wasomi.

Anasema lengo la mpango huo wa Maendeleo wa Miaka Mitano kipindi cha kwanza, ni kutumia vizuri rasilimali za nchi, kuondokana na umasikini na tayari mpango umeshabeba dhana ya kuangalia fursa za ukuaji wa uchumi.

Pia, anashangaa chakula cha samaki kuagizwa kutoka nje ya nchi, akihoji nchi ilikokwama na anashauri wasomi waliopo waangalie mazingira ya kukuza uchumi wa Mwanza, lengo ni kunufaika na rasilimali zake, zilete mapinduzi ya kiuchumi.

Anasema, ili kwenda sambamba na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, watalaamu wa ndani watumike kuzalisha, akionya wasitumike madalali.

Mkuu wa mkoa anasisitiza anachokitaja ‘biashara ni uchumi na nguvu ya nchi’, hivyo shida zinazoibuliwa za ucheleweshaji kutoa nyaraka, nishati ya umeme na nyingine, zitafutiwe ufumbuzi ili kuweka mazingira bora uwekezaji.

Pia, anataja kubuniwe mikakati ya kuwezesha viwanda vilivyopo kuwa shindani na kuhamasisha mashirika ya umma na sekta binafsi kuwekeza katika uanzishaji wa viwanda saba vipya vya kusindika na kuongeza thamani ya mazao ya samaki.

Habari Kubwa