Taka barabarani, ajali zisizoisha ‘zinavyoimaliza’ Hifadhi Mikumi

17Jan 2019
Ashton Balaigwa
Mikumi
Nipashe
Taka barabarani, ajali zisizoisha ‘zinavyoimaliza’ Hifadhi Mikumi
  • Nyani wahama, kila siku anakufa mnyama
  • Tani moja ya uchafu kila kunavyokuchwa
  • Operesheni ‘kamata wakaidi’ yaanza rasmi

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), kupitia mradi wake wa Protect, unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID), uliamua kuzuru katika Hifadhi za Taifa Mikumi, mkoani Morogoro, kutathmini jitihada inazofanywa kukuza na kuhifadhi utalii katika hifadhi hiyo.

Hifadhi ya Mikumi ipo umbali wa kilomita 283. Magharibi mwa jiji la Dar es Salaam wilayani Kilosa, mkoa Morogoro na Kaskazini mwa Mbuga ya Selous, ambayo ni kubwa kuliko zote nchini.

Ni kitega uchumi kilichoanzishwa mwaka 1964 kwa Tangazo la Serikali Namba 465, ikiwa na ukubwa kilomita za mraba 1,070.

Miaka tisa baadaye, mwaka 1975, serikali iliona umuhimu wa kuongeza eneo lake upande wa Kusini na Kaskazini kufikia ukubwa wa kilometa za mraba 3,230 kwaTangazo la Serikali Namba 121.

Mahali ilipo ni katika barabara kuu inayounganisha Dar es Salaam na nchini Zambia. Ni njia inayotumiwa na abiria na magari ya mizigo.

Kwa mkoa Morogoro, barabara hiyo imepita katika baadhi wilaya za Mvomero na Kilosa, kilomita 50 zinapita ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

Ni mazingira yanayoleta changamoto na athari mbalimbali kwa wanyamapori wanaohifadhiwa hifadhini, ikisababisha baadhi yao kupoteza asili na wengine kufa.

Uchafuzi huo unamaanisha taka zinazotupwa na wapitaji, zikiwemo vyakula na matokeo yake kuathiri tabia za asili za wanyama hao, huku wengine kufa.

MHIFADHI MKUU

Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo ya Mikumi, Godwell Ole Meing’taki, anasema uchafu unatokana na mabaki ya vyakula mbalimbali vinavyotupwa na abiria wanaotumia barabara hiyo vimekuwa tishio kwa wanyama na kuharibu ikolojia zao na kwamba wameamua kuanzisha mkakati maalumu wa udhibiti.

Ole Meing’taki, anasema athari hizo za kutupwa mabaki ya vyakula zimesababisha baadhi ya wanyama hao hasa jamii ya nyani kuishi sasa kwa kutegemea mabaki hayo, wakisubiri pembezoni mwa barabara kuu inayopita katikati ya hifadhi, zikitupwa na abiria.

Mhifadhi huyo anasema wastani wa tani moja ya uchafu mbalimbali hutupwa kila siku na abiria wanaosafiri katika barabara kuu, kipande hicho cha kilomita 50. Wataalamu wanalalamika athari ya wazi iko katika ikolojia za wanyama jamii ya nyani.

“Hawa wanyama siku za nyuma kwa tabia zao za asili wamekuwa wakijitafutia vyakula wenyewe kama matunda na vingine, lakini siku za karibuni kutokana na abiria wanaopita katika barabara iliyopo ndani ya hifadhi hii kuwatupia mabaki ya vyakula.

“Hivi sasa wameanza kubadili ikolojia zao, kwa kutegemea kutupiwa vyakula hivyo ili waishi na ndio maana muda mwingi unawakuta wapo barabarani” anasema mhifadhi huyo.

KAMPENI YAANZISHWA

Ole Meing’taki anasema, sasa wameanzisha kampeni maalumu, kwa kushirikiana na Polisi Kikosi chake cha Usalama Barabarani, wilaya za Mvomero na Kilosa, wakiwataka madereva na abiria wanaopita katika barabara hiyo, wazingatie sheria za hifadhi.

Anasema, kampeni hizo zimelenga ufuatiliaji sheria za hifadhi, ikiwemo kutoa elimu kwa abiria na madereva kuacha kutupa taka ovyo, hifadhini ili kusaidia kunusuru uhai wa wanyama.

Takwimu zinaonyesha kila saa 24, kuna zaidi ya magari kati ya 2,000 na 2,500 yanapita katika Hifadhi ya Taifa Mikumi, ambalo watumiaji vyombo hivyo wanatupa mabaki ya vyakula na taka, zikiwemo biskuti na matunda yanayowaathiri sana wanyama.

Mhifadhi huyo anasema, kampeni hizo zinazoenda sambamba na kuzuia ajali ndani ya hifadhi zinazochangia wanyama kugongwa, baadhi yao wanakufa, ikiishia katika tafsiri kubwa ya hasara ya umma na serikali yao, katika eneo ambalo watalii wa ndani na kimataifa wanafika kuangalia wanyama.

“Wakati mwingine hawa abiria wanaona kama wanafanya hisani kwa kuwatupia wanyama kama jamii ya tumbiri, vyakula ili waweze kula,” anasema Ole Meing’taki na kuongeza:

“Lakini, wanafanya makosa makubwa kwakuwa kila mnyama ana asili ya vyakula vyake hivyo ukimtupia chakula kingine unaathiri asilia yake, pia tunachafua mazingira.”

Kuhusu kampeni ya kuzuia vifo vya wanyama wanaogongwa na magari, mhifadhi huyo anasema licha ya kuwekwa kwa vibao na alama za kuonyesha tahadhari za wanyama wanaovuka katika barabara hiyo na sheria za adhabu, lakini bado kuna madereva wanaokaidi kwa kuwagonga wanyama.

Ni hali ambayo mhifadhi huyo anaieleza, inajenga hofu, ya kupungua baadhi ya wanyamapori, ikizingatiwa takwimu zinaonyesha wastani wa mnyama mmoja anagongwa kila siku.

Hivi sasa katika kampeni ya kuokoa wanyama wanaogongwa, mhifadhi huyo anasema wanakusudia kufunga kamera maalum za CCTV barabarani, itakayoonyesha kila mpitaji barabarani na kasi yake, ndani ya eneo la hifadhi.

POLISI TRAFIKI

Mkuu wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mikumi, Sunday Ibrahimu, anasema wameanza kufanya ukaguzi wa kila mara kukagua utii wa agizo hilo.

Anaeleza kwamba hilo litatekelezwa kwa kuangalia mengi, ikiwemo elimu na utii wa kanuni na sheria za barabara, pamoja na maelekezo mengine ya usalama na utunzaji mazingira.

Ibrahimu anasema, katika mkakati huo hivi sasa wanashirikiana na wenzao Polisi wa Usalama Barabarani Mvomero, wanawadhibiti madereva wanaotembea kwa mwendokasi pindi wawapo hifadhini, ili kuokoa wanyama wanaoweza kugongwa.

“Tumeweka vituo maalumu vya ukaguzi ndani ya hifadhi inapopita barabara ndani ya kilomita 50, ili tuweze kuwabaini madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani na zile za hifadhi na tukiwabaini tunawafikisha mahakamani, ili wachukuliwe hatua kali “anasema Ibrahim.

MADEREVA

Dereva wa mabasi anayefanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Tunduma, Mohamed Hussein, anapongeza kuanzishwa kampeni hiyo ya elimu kwao na abiria, akisema suala la uchafu ni kero kubwa kwao, kwani licha ya kuwekwa vifaa vya kuhifadhi taka ndani ya mabasi, bado kuna abiria waliokosa utaarabu kutupa taka nje.

“Wapo abiria wananunua ndizi makusudi maeneo ya stendi kuu ya Morogoro, ili wakifika katika hifadhi hiyo waitupe kuona wanyama wanavyokula,” analalamika Hussein.

“Tunajitahidi kutoa elimu kwao na kuweka vifaa vya kuhifadhia taka, lakini wapi hawaelewi, hivyo elimu hiyo inayotolewa katika mabasi juu ya uhifadhi, ni muhimu sana na itasaidia kuokoa maisha ya wanyama,” anafafanua.

Dereva mwingine, Abbas Shaibu, anayeendesha basi kati ya Dar es Salaam na Ifakara, anaunga mkono hoja hiyo akisema kampeni ya kuzuia ajali za wanyama, imekuja katika wakati sahihi.

Anawanyooshea vidole baadhi ya wezake wanaoendesha kwa spidi kali, tofauti na iliyowekwa hifadhini na kuchangia ajali za wanyama, akiamini hatua sasa italeta mabadiliko ya sheria kufuatwa.

Rai yake ni kwamba, zitungwe sheria ndani ya hifadhi ili ziwadhibiti madereva wakorufi, hali itakayodhibiti vitendo hivyo na wakati huo huo, ikitanua elimu ya madereva kuhusiana na manufaa na ulinzi wa hifadhi nchini.

WAOKOTA TAKA

Katibu wa Kikundi cha Uzoaji Taka ndani ya Hifadhi ya Mikumi(Mecode), Chrisandus Mdoe, anasema wameingia katika mkataba wa kuzoa taka na Hifadhi ya Taifa Mikumi.

Anasema, kila wiki kuna wastani wa tani moja ya taka hizo za mabaki ya vyakula,vyuma chakavu na chupa za maji wanazookota barabarani.

Mdoe anafafanua kwamba, katika kila wiki wamekuwa wakinufaika kwa kuuza baadhi ya vitu wanavyookota kama vile chupa za plastiki. Anafafanua: “Pale hifadhini tunapoingia kufanya usafi, tunanufaika na vitu vingi sana. Yapo magari yanayotupa vyuma chakavu, matairi na hata bidhaa nyingine.

“Basi, sisi tunaokota kama uchafu na kuleta hapa ofisini kwetu na kuanza kuchambua, kisha zile za plastiki tunapeleka sehemu wanazotaka na kuwauzia wao, wanayeyusha na kutengeneza mifuko au chupa nyingine. Kwa hiyo, tunajipatia mapato ya kutosha.”

RC MORO

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Stephen Kebwe, anasema mkakati wa mkoa ni kwamba umejipanga kuhakikisha unatangaza vivutio vyote vya utalii ndani ya mkoa, ili kuongeza mapato yake na hasa fedha za kigeni.

Anasema, kwa kuanzia vivutio vyote vya utalii vitawekewa mazingira mazuri, ikiwemo kudhibiti ajali za wanyama na vikwazo vinavyochangia utalii kukwama, ikiwemo kudhibiti ujangili na uhalifu vinakomeshwa.

“ Kwa kuanzia ili kuhamasisha utalii wa ndani na nje, sisi kama mkoa tumejipanga watumishi wote wa serikali na familia zetu, tunaenda kutembelea hifadhi zetu zote zilizopo mkoani Morogoro, ili kuhamasisha utalii nchini” anasema Dk, Kebwe.

WAZIRI MALIASILI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla, alipotembelea Hifadhi ya Mikumi, anasema serikali inatafakari kubadilisha mwelekeo wa kilomita 50 za barabara zinazopita ndani ya Hifadhi ya Taifa Mikumi au kutoza kodi ya utalii kwa wanaotumia barabara hiyo, kukabiliana na changamoto zilizopo.

Dk.Kigwangalla anasema, baada ya uongozi wa hifadhi kuiomba serikali kuchepusha barabara hiyo kutokana na athari tajwa za uwepo wake ndani ya hifadhi, hususan vifo vya wanyamapori,ujangili na serikali kukoseshwa mapato.

Waziri anasema, barabara ya lami inayokatiza hifadhini, haiko katika mazingira rafiki. Anafanua: “Kuna hiyo barabara ambayo inaleta watalii hapa. Ni barabara ambayo iko ‘bize’ sana, ni barabara ya kitaifa na kwa vyovyote vile, hii sio barabara mahsusi kwa ajili ya shughuli za utalii.

“Sisi (serikali) tunatafakari namna ya aidha kuiondoa hiyo barabara au namna ya kuwachaji watu wanaokatiza hizi kilometa 50 ambazo zipo ndani ya hifadhi ya Mikumi.”

Anasema, takwimu zinaonyesha kwamba kati ya mwaka 2014 wanyamapori waliogongwa walikuwa 351; mwaka 2015 (361) na mwaka 2016 walikuwa 218.

Anataja changamoto nyingine, ni uchafuzi wa mazingira ambayo wastani wa taka ngumu zisizopungua kilo 138.3, huzalishwa kila siku na watumiaji barabara.

Dk. Kigwangalla anataja mengine, ni ukosefu wa mapato ya serikali, kwani hakuna geti za kulipia tozo za utalii kwa watumiaji barabara hiyo wanaofaidi utalii huo bure.

Pia, anataja ujangili ambao ni hasi kwa Hifadhi ya Mikumi, akisema majangili wanaingia hifadhini kirahisi kwa njia mbalimbali, zikiwemo magari na pikipiki.

Habari Kubwa