Takwimu Azam vs Yanga mashindano yote

09Jan 2017
Sanula Athanas
Dar es Salaam
Nipashe
Takwimu Azam vs Yanga mashindano yote

JUMAPILI Januari 7, 2017 ni siku nyingine mbaya kwa mashabiki wa klabu ya Yanga kutokana na timu yao kufungwa mabao 4-0 dhidi ya Azam FC, kipigo kikubwa zaidi kwao tangu Mei 6, 2012 walipolala 5-0 dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo ya juzi iliyokuwa ya mwisho kwenye Kundi B la michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar, Yanga ililala kwa idadi hiyo kubwa ya mabao yaliyopachikwa nyavuni na Nahodha John Bocco 'Adebayor', Mohamed Yahaya, Joseph Mahundi na mtokea benchini Enock Agyei.

Ushindi huo mnono uliipa Azam FC uongozi wa Kundi B ikifikisha pointi saba, moja mbele ya Wanajangwani walioshinda 6-0 dhidi ya Jamhuri na 2-0 dhidi ya Zimamoto katika mechi mbili za awali kabla ya kukumbana na kipigo hicho cha juzi.

Takwimu za Spotika zinaonyesha kuwa, bao la dakika 85 lililowekwa kambani na Mghana Ageyi ni la 63 kufungwa katika mechi 28 za michuano yote kati ya Azam FC na Yanga tangu zilipoanza kukutana kwa mara ya kwanza Oktoba 15, 2008.

Bao hilo ambalo Ageyi alilifunga kwa shuti la mguu wa kulia ndani ya boksi, pia ni la 28 kwa Azam kuifunga Yanga, saba nyuma ya mabao ya Wanajangwani dhidi ya timu hiyo ya Chamazi.

Takwimu za Spotika pia zinaonyesha kwamba, ushindi wa juzi ni wa 10 kwa Azam FC dhidi ya Yanga ambao pia wameifunga timu hiyo ya Wanalambalamba mara 10 na kutoka sare mara nane.

Kabla ya mechi ya juzi, ambayo ilikuwa ya tatu kwa timu hizo mbili kukutana katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, Yanga walikuwa wameizidi Azam FC kwa ushindi wa mechi moja na mabao 11 kwenye mashindano yote.

YANGA VS AZAM MASHINDANO YOTE
P W D L GF GA GD Pts
Yanga 28 10 8 10 35 28 7 38
Azam 28 10 8 10 28 35 -7 38
CHANZO: Maktaba ya Nipashe

Timu hizo zimekutana mara 17 katika Ligi Kuu Tanzania Bara, kila moja ikishinda mara tano na kutoka sare mara saba.
Katika mechi hizo 17, Yanga wamefunga mabao 23, huku wakifungwa mara 22 na Azam FC.

Hata hivyo, ni Azam iliyofanya vizuri zaidi katika miaka ya karibuni kwani mara ya mwisho kufungwa na Yanga Ligi Kuu ilikuwa Februari 23, 2013 ilipolala 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa.

YANGA VS AZAM FC LIGI KUU
P W D L GF GA GD Pts
Yanga 17 5 7 5 23 22 1 22
Azam 17 5 7 5 22 23 -1 22
CHANZO: Maktaba ya Nipashe

AZAM VS YANGA LIGI KUU

2008/09
1. Azam 1-3 Yanga (Oktoba 15, 2008)
2. Yanga 2-3 Azam (Aprili 8, 2009)

2009/10
3. Azam 1-1 Yanga (Oktoba 17, 2009)
4. Yanga 2-1 Azam (Machi 7,2010)

2010/11
5. Azam 0-0 (Okt 24, 2010)
6. Yanga 2-1 Azam (Machi 30, 2011)

2011/12
7. Azam 1-0 Yanga (Sept 18, 2011)
8. Yanga 1-3 Azam (Machi 10, 2012)

2012/13
9. Azam 0-2 Yanga (Nov 4, 2012)
10. Yanga 1-0 Azam (Feb 23, 2013)

2013/14
11. Azam 3-2 Yanga (Sept 22, 2013)
12. Yanga 1-1 Azam (Machi 19, 2014)

2014/15
13. Yanga 2-2 Azam (Des 28, 2014)
14. Azam 2-1 Yanga (Mei 5, 2015)

2015/16
15. Yanga 1-1 Azam (Okt 17,2015)
16. Azam 2-2 Yanga (Machi 5, 2016)
17. Azam 0-0 Yanga

CHANZO: Maktaba ya Nipashe

KOMBE LA KAGAME

Timu hizo pia zimewahi kumenyana mara mbili katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Yanga ikishinda 2-0 fainali ya 2012 kwenye Uwanja wa Taifa.

Azam walilipa kisasi mwaka juzi kwa kuishindilia Yanga mikwaju 5-3 ya penalti baada ya kutoka suluhu katika dakika zote 90 za mechi ya robo fainali ya Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa Taifa.

NGAO YA JAMII
Timu hizo zimekutana mara nne katika mechi za Ngao ya Jamii kuashiria uzinduzi wa msimu mpya, Yanga ikitoka na ngao mara tatu ikifunga mabao sita dhidi ya mawili ya wapinzani wao hao.

AZAM VS YANGA - NGAO YA JAMII
2013: Yanga 1-0 Azam
2014: Yanga 3-0 Azam
2015: Yanga 0-0 Azam (pen. 8-7)
2016: Yanga 2-2 Azam (pen. 1-3)

KOMBE LA MAPINDUZI
Katika Kombe la Mapinduzi, timu hizo zimewahi kukutana mara tatu; fainali ya mwaka 2012 ambayo Azam FC walishinda 3-0, hatua ya makundi mwaka jana zilitoka sare ya 1-1 na juzi kwenye Kundi B Yanga ikikubali kipigo hicho kikubwa zaidi kufungwa na Azam (4-0).

Takwimu hizo zinamaanisha Azam imeibamiza Yanga jumla ya mabao 8-1 kwenye mashindano hayo ambayo mwaka huu yanafanyika kwa mara 12 tangu yaanzishwe mwaka 2004 (hayakufanyika 2006 na 2009).

KOMBE LA FA
Azam na Yanga zilikutana pia katika fainali ya michuano ya Kombe la FA ambayo ilifufuliwa tena na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mwaka jana, Wanalambalamba 'wakafa' 3-1.

MECHI YA HISANI
Mwaka 2011, timu hizo ambazo mechi zake zimekuwa na upinzani mkali katika miaka ya karibuni kutokana na kuimarika kwa kikosi cha Azam, zilikipiga pia katika mechi ya hisani kuchangia walemavu, Azam ikashinda 2-0.

Mbali na kukumbushia kipigo cha fedheha cha mabao 5-0 Mei 6, 2012 kisicho midomoni mwa mashabiki wa Simba, ushindi wa juzi wa Azam ulikumbushia kipigo kingine kibaya zaidi cha mabao 6-0 ambacho Yanga ilikipata kutoka kwa wapinzani wake wa jadi, Simba mwaka 1977.

Habari Kubwa