TALGWU: Rais Samia amefuta machozi ya miaka sita

14May 2022
Mary Geofrey
Nipashe
TALGWU: Rais Samia amefuta machozi ya miaka sita

BAADA ya serikali kutangaza nia ya kuongeza mishahara kwa wafanyakazi, Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU), kimeeleza furaha yake na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwakumbuka baada ya miaka kadhaa kupita.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU), Rashid Mtima, akiongea na waandishi wa habari hawapo pichani.

Katibu Mkuu wa TALGWU, Rashid Mtima, anasema chama hicho kinaungana na wafanyakazi wa kada mbalimbali kuonyesha shukrani zao kwa rais kutangaza neema mwaka ambao chama hicho ndicho kimeratibu sherehe hizo.

Anasema Rais Samia, amejenga ari ya kufanya kazi na kuleta matumaini mapya kwa wafanyakazi ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakisahaulika.

 “TALGWU tuna furaha kuandaa sherehe za Mei Mosi kitaifa na Rais ambaye alikuwa mgeni rasmi kutoa ahadi ambayo wengi tulipenda kusikia,” anasema Mtima.

Anasema furaha kubwa kwa wafanyakazi ni kuona mkuu wa nchi anatambua na kuthamini kazi kubwa wanayofanya wafanyakazi katika sekta mbalimbali kuleta maendeleo katika Taifa.

“Mtima natoa shukrani kwa niaba ya watumishi wote nchini kwa kuwahakikishia nyongeza ya mishahara. Ni muda mrefu sasa watumishi wa umma hawajapandishiwa mishahara kwani kilio hiki kilikuwa cha muda mrefu na sasa jambo hili linaenda kutekelezwa kama alivyosema Rais Samia,"anaongeza kusema.

TALGWU inaunganisha wafanyakazi wote waliopo chini ya Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi nyingine nchini.

Chama hicho ni miongoni mwa vyama vya wafanyakazi nchini ambacho jukumu lake kuu ni kujenga nguvu ya pamoja ya kutetea haki na maslahi ya wafanyakazi waliopo chini ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Katika muungano wake ni moja ya vyama vinavyounda Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi vinavyotoa Huduma kwa Umma duniani (PSI) na Mtandao wa Vyama vya Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Afrika (AMALGUN).

Katika utendaji wake wa kazi, TALGWU ina jukumu la kuelimisha, kunatetea, na kulinda ajira na ujira wa wanachama wake kwa kuzingatia sheria, taratibu, kanuni, miongozo na nyaraka mbalimbali za kazi.

Katika kuadhimisha sherehe ya Mei Mosi mwaka huu, yenye kauli mbiu isemayo, ‘Mishahara na Maslahi Bora kwa Wafanyakazi ndio kilio chetu Kazi Iendelee’, inajivunia kwa kuwa na matokeo chanya baada ya miaka sita bila matokeo ya nyongeza za mishahara.

Hali mbaya kwa wafanyakazi inatokana na kukaa miaka mingi bila kuongezwa mshahara, sekta binafsi inafikia miaka tisa.

Katibu huyo anasema wafanyakazi ni injini ya maendeleo katika taifa lolote duniani, hivyo ni vema mchango wao unapaswa utambulike na kuthaminiwa ili kuhakikisha wanaongeza ukuaji wa  uchumi wa nchi.

Pia anamshukuru Rais Samia kwa kusikiliza kilio chao kuhusu maslahi ya watumishi walioondolewa kazini kwa vyeti vya kughushi.

“Kama chama kupitia TUCTA kwa muda mrefu tulikuwa tukiiomba serikali kuliangalia kundi hili la Watanzania ambao walitumikia kwa uadilifu nchi yetu,"anasema Mtima.

Anasema Rais Samia ameonyesha upendo mkubwa kwa Watanzania ambao waliitumikia nchi kwa nguvu zao zote hatimaye ameagiza Wizara ya Fedha na mipango kushughulikia na kuwalipa stahiki zao zinazotokana na makato ya mishahara yao.

Mtima anasema agizo kwa mifuko ya hifadhi ya jamii na maofisa utumishi kuhakikisha wanashughulikia haki na stahiki za watumishi wanaotarajiwa kustaafu linazidi kuwapa faraja zaidi.

Anasema kuundwa kwa bodi ya kima cha chini cha mishahara kwa sekta ya umma ambayo imeshaanza kufanya kuthmini ya mishahara ni jambo kubwa na la kuigwa na viongozi wengine.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa TUCTA, Cornel Magembe, anasema kwa ahadi ya Rais Samia ni wazi kuwa amekubali kuongeza mishahara na anaimani kuwa mwaka wa fedha wa Serikali utakapoanza kutakuwapo na mabadiliko.

Anawaomba wafanyakazi kuwa na subira katika kipindi hiki kwa sababu kiongozi huyo wa nchi hajawahi kusema na kutotekeleza,

"Rais ni kiongozi mkubwa hawezi kwenda kinyume hivyo niwaombe wafanyakazi wavute subira kwani mwaka wa fedha wa serikali unaanza mwezi wa saba na ninaimani kipo kitu kitaongezeka," anasisitiza.

Habari Kubwa