Tambua faida ya kila bidhaa unayouza.

23Sep 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Tambua faida ya kila bidhaa unayouza.

Unafahamu faida unayopata kwa kila bidhaa unayouza? Wafanyabiashara wengi hususani wanaouza bidhaa zaidi ya moja katika biashara zao, huwa hawajua faida inayopatikana kwa bidhaa mojamoja. Wengi hujua faida ya jumla kwa maana mzigo walioagiza ukiisha basi wanajua wamepata faida kiasi gani.

Moja ya vigezo ambavyo hutumiwa na mfanyabiashara akitaka kuleta bidhaa ni kuangalia inayouzika zaidi, maana yake bidhaa inayopendwa na wateja atakuwa na uhakika wa kuuza.

Pia kuna sababu nyingine ambayo inaweza kukushawishi ni faida utakayopata katika bidhaa hiyo. Faida kubwa itakuwa miongoni mwa bidhaa hizo ambazo yakupasa kuleta hususani kama soko lake ni zuri.

Ukijua faida ya kila bidhaa, itakuwezesha kutoa kipaumbele kwa bidhaa zinazokupa faida kubwa. Kwenye timu ya mpira wa miguu, kila mchezaji ana thamani yake kutokana na mchango wake katika timu na viwango vya mishahara yao hailingani.

Hivyo ndivyo ilivyo kwenye biashara. Bidhaa moja haiwezi kuwa na mchango sawa na nyingine. Kwa hiyo kuna umuhimu wa kufahamu mchango wa kila bidhaa kwenye maendeleo yako.

Nini kifanyike? Cha msingi ni kutunza kumbukumbu sahihi ya bei ya kununua, kuuza, idadi ya bidhaa zilizouzwa na tarehe ya kununua na kuuza. Najua kwa kiasi kikubwa wafanyabiashara hutunza kumbukumbu hizi, lakini wanapokokotoa faida ya bidhaa mojamoja ndiyo huwa tatizo.

Kwa kawaida, faida inapatikana kwa kuchukua bei ya kuuzia toa bei ya kununua, japo faida hii haionyeshi ongezeko la asilimia (percentage change) ambayo inaonyesha mchango wa bidhaa katika biashara. Ili kujua umepata faida asilimia ngapi (percentage profit) ni faida uliyoipata zidisha kwa 100 gawanya kwa bei uliyonunulia . Mfano, Radio umenunua (N) sh. 140,000 ukaiuza (U) sh. 170,000
Faida ni U - N, 170,000 - 140,000 = 30,000.Kujua umepata faida asilimia ngapi, chukua faida zidisha kwa mia moja gawanya kwa bei ya kununulia yaani 30,000*100/140,000 = 21.4 (%. ) Kwa mfanyabiashara mathalani wa nguo, itamsaidia je hii kanuni?

Mfano sketi imenunuliwa sh 8,000 na kuuzwa sh. 15000 faida ni sh. 7,000 sawa na asilimia 87.5. Na suti imenunuliwa kwa sh. 22000 na kuuzwa sh. 30,000 ambayo faida ni sh. 8,000 sawa na asilimia 36.36

Ukiangalia mfano huu suti inakupa faida ya sh. 8,000 lakini ukiangalia asilimia ni 36.36.Pia ukiangalia nguo aina ya sketi inakupa faida sh. 7,000, lakini asilimia ya faida (percentage profit) ni 87.5

Kwa haraka haraka, unaweza kushawishika kuuza suti zaidi kwa sababu unapata faida kubwa ambayo ni 8,000 lakini kwa uhalisia na kama mtaji wako ni mdogo bora ukajikita zaidi kwenye uuzaji wa sketi na kama soko la bidhaa hizi linalingana kwa maana wateja wake.

Maana ukiwa na mtaji wa sh 88,000, una uwezo wa kununua suti nne, na baada ya kuuza utapata faida ya sh 32,000 (8000*4 = 32,000). Lakini ukichukua mtaji huohuo wa sh 88,000 na kununua sketi, utaweza kununua sketi 11 na baada ya kuziuza utapata faida ya sh (7000*11 = 77,000)77,000/=, ambayo ni zaidi ya mara mbili kwa faida iliyopatikana baada ya kuuza suti.

Kumbe mfanyabiashara anatakiwa kuipa kipaumbele bidhaa ya sketi kwa faida kubwa, hususani kama mtaji wake siyo mkubwa. Asante sana tukutane muda mwingine