Tangu 1964 SMZ haijawahi kuangusha wakulima karafuu

12Jan 2019
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Tangu 1964 SMZ haijawahi kuangusha wakulima karafuu

CHEI CHEI Watanzania leo taifa linasherehekea miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yaliyoung’oa usulutani na kuwapa Wazanzibari heshima ya uhuru iliyokatilia mbali mapingu ya ukoloni wa kiarabu.

Kama kawaida uhuru ni kazi na kilimo ndiyo msingi wa maendeleo, ndiyo maana hata baada ya miongo mitano ya uhuru Zanzibar, ulioletwa na mapinduzi, taifa limeendelea kushuhudia manufaa mengi na faida za kilimo cha karafuu.

Uchumi wa visiwa hivi unategemea zaidi sekta ya kilimo hasa kwa mazao ya viungo, karafuu ikiongoza.

Kwa miaka yote hiyo huwezi kuliondoa zao hili kwenye ramani wala ardhi ya visiwani kwani karafuu imekuwa ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya fedha za kigeni ikifuatiwa na sekta ya utalii ambayo imekuwa na tija kubwa kwa wakazi wa Unguja na Pemba.

Kwa mujibu wa taarifa na takwimu za Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi zao hili huingiza kiwango kikubwa cha fedha za kigeni na ndilo pia linalotoa ajira kwa wananchi na vijana wengi ambao ni wakulima na wafanyakazi viwandani, hivyo kuneemesha hali zao kiuchumi.

MAGEUZI YA KARAFUU

Zanzibar hivi sasa kimaendeleo ni tofauti na ile ya miaka 60 wakati mapinduzi yalipofanyika.Kimaendeleo imeimarika katika kila sekta ikiwamo ya biashara ya zao la karafuu,ambayo husimamiwa na Shirika la Biashara la Zanzibar.

Taarifa za Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi zinabainisha kuwa serikali ya awamu ya saba chini ya uongozi wa Dk. Ali Muhamed Shein, imetoa kipaumbele kuimarisha maslahi ya wakulima katika kufikia mageuzi ya sekta hiyo.

BEI INAYOVUTIA

Serikali imekuwa bega kwa bega na wakulima kwanza kubadilisha sera ya malipo kwa wakulima kwa lengo la kuwanufaisha zaidi na kupunguza malalamiko.Serikali ilitangaza bei ya kununulia karafuu kutoka kwa mkulima kuwa asilimia 80 ya bei ya kuuza karafuu ng’ambo.

Bei hiyo iliwatia ari na moyo wakulima kukiimarisha zaidi kilimo cha zao hilo kwa kupanda mikarafuu mingi zaidi, kuhudumia mashamba na kuuza karafuu zao serikalini.

Katika miaka mitano ya uongozi wa Dk Shein alifanya utekelezaji wa mageuzi, wakulima waliuza karafuu zao kwa Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC) kwa wastani wa bei ya Shilingi 14, 000 kwa kilo badala ya Shilingi 5, 000.

Wizara inasema bei hiyo ilikuwepo tangu mwaka 2010 na kwamba ongezeko hili ni sawa na asilimia 180 na kwamba kilimo cha karufuu hususan kisiwani Pemba kimebadilisha maisha ya wananchi na hivi sasa wengi wameondokana kuishi katika nyumba za udongo na kuezekwa kwa makuti hivyo kujinafasi katika nyumba za kisasa.

Wizara ya Kilimo inasisitiza kuwa kutokana na umuhimu wa zao hilo,Serikali ya Zanzibar, haina mpango wowote wa kubinafsisha biashara na kilimo cha zao la karafuu na inaendelea kuinunua karafuu kutoka kwa wakulima ili kumwezesha mkulima kuendelea kujenga imani na kuithamini karafuu.

SAUTI YA MKULIMA

Ali Hamadi, mkazi wa Ulenge kisiwani Pemba ni miongoni mwa vijana waliojiimarisha kutokana na kilimo cha karafuu na hivi sasa anamiliki duka la vifaa vya ujenzi, ambalo ni matokeo ya kilimo.

Anaieleza Nipashe kuwa mafanikio aliyonayo yameanza mwaka 2015, baada ya kukodi mashamba mawili ya mikarafuu katika kijiji cha Mjimbini.

Anasema baada ya kuuza alitengeneza faida na kuongeza kipato.Alikodi mashamba ya mikarafuu kwa shilingi 3,000,000 baada ya kutoa gharama, alipata faida ya shilingi 2,000,000.

Anasema katika faida hiyo aliyoipata alitumia shilingi milioni kununua ng’ombe, ambao wanasafirisha mizigo kutoka eneo moja kwenda jingine.

Anasema katika msimu wa karafuu wa mwaka 2016, alikodi mashamba mengine mawili katika msitu wa Mbiji mkoani Pemba kwa shilingi milioni 4.2.

“Baada ya mavuno nilipata faida ya shilingi milioni 3.1, ambazo niliamua kuziwekeza kwenye duka la vifaa vya ujenzi liliopo kijiji cha Stahabu.” Anasema Hamad.

Hamad anaeleza kuwa amejifunza utamaduni wa kukodi mikarafuu kila msimu na sasa ana mtaji unaokaribia Shilingi milioni 11.

“Mbali ya kumiliki duka, pia nina nyumba ya vyumba vinne tena ni ya kisasa ambayo ndiko ninakoishi pamoja na familia yangu,”anasema Hamad.

Katika kipindi cha miaka saba tangu aingie madarakani, Dk. Shein, amefanya mageuzi makubwa katika sekta ya karafuu hali iliyorejesha ari ya wananchi ya kukiendeleza kilimo cha zao hilo.

Mageuzi hayo ya miaka 10 yanaanzia 2011 hadi 2021 yanalenga kurudisha hadhi na thamani ya karafuu kwa maendeleo ya Zanzibar.Katika mageuzi hayo, Dk. Shein anaangalia zaidi mabadiliko ya kimaisha na mtazamo wenye kuleta tija na maendeleo ya nchi kwa kuipa hadhi na msukumo wa kipekee sekta ya karafuu.

Mipango hiyo inakwenda sambamba na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (Mkuza II1) na malengo endelevu ya dunia, kwa vile kuimarika kwa sekta ya karafuu ni kuimarika kwa uchumi wa nchi, kuongezeka ajira, kuimarika kipato cha wakulima na wananchi wanaotegemea zao hilo na kupunguza umasikini.

Katika miaka mitano ya kwanza (2011 -2016), hatua maalum zimechukuliwa na serikali katika kuongeza uzalishaji, usafirishaji, ubora na tija, kwa wakulima na serikali kwa ujumla.

Serikali imefanya mageuzi makubwa katika sekta nzima ya karafuu ikiwa ni pamoja na kutunga sheria, sera na miongozo mbalimbali ya kusimamia sekta hiyo ambapo faida, tija na ustawi wa maisha ya wanaotegemea kupata kipato kutoka katika zao hilo.

KUONGEZA UZALISHAJI

Utekelezaji wa mkakati huo umeleta mafanikio kwa sekta ya karafuu kwani kwa kipindi cha miaka saba kuanzia 2012 hadi 2018 tani 31,085.60 za karafuu zenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 437.195 zimeuzwa sehemu mbalimbali.

Hali hiyo inadhihirisha kwamba katika kipindi cha miaka saba ya uongozi wa Dk. Shein, wakulima wa karafuu wamejipatia Shilingi bilioni 437.195 kutoka bilioni 42.6 miaka mitano kabla ya utekelezaji wa mkakati huo.

Ongezeko hilo la fedha zilizoingia mifukoni mwa wakulima ni asilimia 80. Aidha, katika kipindi hicho, tani 5,271.5 za makonyo ya karafuu zenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 4.071 zimenunuliwa kutoka kwa wakulima.

Licha ya elimu inayotolewa kwa wakulima juu ya namna ya kulinda ubora wa zao la karafuu, ZSTC inafanyakazi ya ziada, imelazimika kununua mashine maalum za kusafisha karafuu kabla ya kusafirishwa nje kwa lengo la kuhakikisha kuwa karafuu zinakuwa safi.

KUFIDIAWAKULIMA

Shirika pia limerudisha mpango wa kutoa fidia kwa wakulima wanaopata ajali wakati wa uchumaji ili kujenga ari na moyo kwa wananchi kushirika katika kazi za uchumaji karafuu.

Shirika la Biashara la Zanzibar kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu limetoa fidia ya Shilingi milioni 186.56 kwa wakulima Unguja na Pemba katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji.

CHANGAMOTO

Pamoja na mafanikio, kuna baadhi ya changamoto zinazolikumba shirika ikiwa ni pamoja na baadhi ya wakulima kuchafua karafuu kwa makusudi kwa kuchanganya na makonyo na vitu vingine ili kuongeza uzito.

Pia, baadhi ya wakulima wanaanika karafuu bila ya kuzingatia maelekezo ya kulinda ubora wengine huzianika karafuu barabarani, juu ya mabati na sakafuni, jambo ambalo ni hatari kwani zinaweza kupoteza ubora.

Aidha, kuna baadhi ya wakulima huchelewa na hata kutorudisha fedha za mikopo ya uchumaji wa karafuu.

Habari Kubwa