Tanzania bila dampo la bidhaa feki inawezekana!

27Feb 2016
Abdul Mitumba
Nipashe
Tanzania bila dampo la bidhaa feki inawezekana!

WIMBI la uingizaji wa bidhaa 'feki' hapa nchini limezidi kushika kasi, na waingizaji na inavyoonekana mahali pa kwenda kuzitupa bidhaa zao ni Tanzania.

Bidhaa feki zikiaribiwa na kalandinga.

Uthibitisho wa hayo ni kiwanda cha kuzalisha chumvi cha Sea Salt Company limited, kilichopo eneo la Saadan, mkoa wa Pwani, kufungwa baada ya kubainika bidhaa inayoingiza haifai kwa matumizi ya binadamu.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Shirika la Viwango nchini (TBS), kukagua bidhaa hiyo na kugundua kutokuwa na viwango.
Afisa Mdhibiti Ubora wa TBS, Deusdedith Paschal, alithibitisha bidhaa hiyo kuwa na upungufu mkubwa wa madini joto.

Chumvi inatakiwa kuwa na kiwango cha madini joto miligramu 30-60, lakini chumvi ya kiwanda hicho ilikuwa na madini joto ya miligramu 14.9, jambo ambalo ni hatari kwa afya za watumiaji.

“Tumezuia kutolewa mifuko 276 ya chumvi iliyozalishwa ambayo ilikuwa tayari kwenda sokoni,” alinukuliwa Paschal na kuongeza kuwa, kiwanda hicho kiliomba kupatiwa leseni ya ubora TBS na baada ya shirika kufanya uchunguzi wa sampuri ya chumvi hiyo katika maabara zake ikabaini ina upungufu wa madini joto.

Chumvi hiyo pia imegundulika kuwa na vitu ambavyo haviwezi kuyeyuka kirahisi kwenye mwili wa binadamu.

Wakati Shirika hilo likiwataka wazalishaji kutengeneza bidhaa zao katika viwango vya ubora na kufuata utaratibu, baadhi ya viwanda vinaonekana kupuuza agizo hilo na kuyaweka maisha ya wananchi katika hatari kiafya
Wakati hatua hizo zikichukuliwa, tayari chumvi hiyo ilikuwa ikitumiwa na walaji kwa muda mrefu na haijulikani ni madhara gani yaliyopatikana baada ya walaji kuitumia kwa muda wote huo.

Mbali na chumvi, kuna mayai yaliyowahi kuingizwa kwa njia za panya. Mayai yaliyosadikiwa kutokea nchi za Uganda na Kenya, ambayo wafanyabiashara huyaingiza na kuyauza kwa bei ya chini.

Mayai hayo kimsingi yalikuwa yatotolewe, lakini kutokana na kuwa chini ya ubora suala la utotoleshaji kwa muda unaotakiwa,wafanyabiashara waliona njia pekee ni kuyatupa kwa njia ya kuwauzia binadamu wenzao.

Waliyaingiza kwenye mzunguko na kuyauza, na kuyafanya mayai yaliyopo nchini kukosa soko na hivyo kulazimika kushuka bei yake.

Aliyekuwa Naibu wa Wizara ya Mifugo, Mathayo David, alishawahi kupelekewa taarifa na kesi ya namna ya kuingizwa kwa mayai kutoka nchini Malawi na Zambia kinyemela.

Yalikamatwa Kibaha mkoa wa Pwani yakiwa tayari yameshaingia kwenye mzunguko.
Kumbukumbu zinaonesha kuwa waziri Mathayo alilivalia njuga tatizo hilo, ingawaje haifahamiki jitihada zile ziliishia wapi.

Licha ya kuwapo kwa taarifa za wataalamu wa afya wakitoa athari zinazoweza kutokea kwa walaji, hasa kwa wanaume kukosa nguvu za kiume, lakini pia ikiwemo baadhi yao kuwa na matiti makubwa mithili ya wanawake. Na kwa wanawake inasadikiwa kuwa hupata homoni nyingi za kiume, ikiwamo kuwa na ndevu na sauti nzito.

Ni mara ngapi tunasikia kuna maziwa ya unga feki, vipodozi feki, dawa feki mchele na vyakula vingine mbalimbali vikiripotiwa kuwa havina ubora kwa mlaji. Wakati huo vinapokamatwa au kuhisiwa, tayari vinakuwa vimetumika, hata kinachokamatwa ni kidogo kuliko kilichotumika.

Sakata la kuwapo kwa sukari inayopitishwa kwa njia za panya kutoka nje ya nchi isiyo na ubora pia, ni miongoni mwa taarifa mbaya.

Katika dampo la Kinyamwezi lililopo Ruvu nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na mahali pengine nchini, mara nyingi bidhaa feki zilizo chini ya viwango zimekuwa zikichomwa moto na kuteketezwa chini ya ulinzi mkali na usimamizi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Nchini (TFDA).

Taarifa za mara kwa mara za kupatikana kwa bidhaa hizo na tahadhari kwa watumiaji, zimekuwa zikitolewa na mamlaka hiyo kupitia vyombo vya habari.

Ingawaje hakuna aliye na uhakika kama elimu na tahadhari hiyo inayotolewa na mamlaka hiyo kwenye radio au luninga na kwa muda mchache, inawafikia wangapi na kwa muda upi? Maana kwa utafiti ulivyo ni asilimia chache sana ya Watanzania wanaozingatia taarifa za kupitia vyombo vya habari.

Hapa ni wazi sheria za udhibiti na uhakiki wa bidhaa zimelegea au kusinzia usingizi wa pono. Kwani hazizingatiwi ipasavyo, na pengine kuna shida kwa upande wa watendaji au hawana utaalamu wa kutosha.

Kimsingi, ni vigumu kabisa bidhaa kuhisiwa au kukamatwa baada ya kuingia kwenye mzunguko kwa miezi kadhaa. Moja kwa moja huo ni uzembe!

Ikiwa jibu ndilo hilo. Na zoezi la ukaguzi wa mara kwa mara kwenye maduka husika, linatakiwa lifanywe kwa muda gani kabla ya ukaguzi ule wa kwanza?

Kama ukaguzi haufanyiki tena ule wa mara kwa mara, si jukumu letu kuwakumbusha wenye mamlaka hizo nini cha kufanya. Isipokuwa wenye ufahamu watajua kuwa huenda ndiyo kikomo cha ufikiri wao, na hawana njia nyingine mbadala ya kujaribu kupunguza kasi hii ya uingizaji bidhaa feki; kama si ukomeshaji kabisa.

Tutegemee kuwaona Watanzania wa leo baada ya miaka mitano na kuendelea wakiwa kwenye mabadiliko makubwa ya maumbile na mwonekano. Hakutakuwa na haja ya kumtafuta mchawi, kwa kuwa tayari tutakuwa tunamfahamu kwa vile tunavyoishi naye na kuamka naye.

Mungu Iponye Tanzania!
0713/0765 937 378.
[email protected]

Habari Kubwa