TARI Ilonga kumaliza shida ya mafuta nchini

19Jul 2019
Ashton Balaigwa
MOROGORO
Nipashe
TARI Ilonga kumaliza shida ya mafuta nchini
  • *Yalenga  kuzalisha tani 500,000 za ufuta kuondoa tatizo

TANZANIA imekuwa ikiagiza wastani wa tani 400,000, za mafuta ya kula kila mwaka kutoka nje ya nchi . Hali hiyo ni kutokana na kuwepo kwa uzalishaji mdogo wa mbegu za mafuta unaotokana na sababu mbalimbali zikiwamo mazao yanayokamuliwa mafuta kutolimwa kwa wingi.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa kilimo Tanzania(TARI), Dk Geofrey Mkamilo, kushoto (anayenyoosha mikono), akizungumza kuhusu pilipili hoho kwa Naibu
Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba, mbele (wa kwanza kulia), wakati alipotembelea
vipando vya mazao vilivyopo katika kituo cha TARI Ilonga.

Kwa mujibu wa takwimu ya Wizara ya Viwanda na Biashara, inakadiriwa kuwa  mahitaji ya mafuta kitaifa  ni tani 500,000, huku uzalishaji pia ukikadiriwa kuwa tani 180,000 .

Kiwango hicho cha mafuta kinatokana na zao la alizeti, michikichi, ufuta na mazao mengine ya mbegu yanayozalishwa nchini.

Kati ya tani hizo zinazozalishwa hapa nchini asilimia 50 husindikwa katika viwanda vikubwa  vilivyopo Mwanza, Dar es Salaam na Singida wakati asilimia 50 nyingine husindikwa katika viwanda vidogo vidogo vilivyopo katika mikoa inayozalisha mazao hayo.Kutokana na uzalishaji mdogo wa mafuta hapa nchini Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania(TARI) Ilonga, iliyopo wilayani Kilosa mkoa  wa Morogoro ,imeamua kuvaa njuga kwa kuhakikisha inaisaidia kupunguza uagizaji wa mafuta kutoka nje na badala yake kuongeza kasi ya uzalishaji wa ndani.Mtafiti wa Ilonga akizungumzia mkakati  wa uzalishaji wa zao la alizeti, ili  kupunguza uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi, mtalaamu  Frank Reuben, anasema wameanza kuongeza uzalishaji wa mbegu  za alizeti zilizothibitishwa ubora ili wakulima nchini waweze kuzalisha kwa kiwango kikubwa cha  mafuta ya kula .Anasema kuwa kupitia mkakati huo watafiti wa TARI Ilonga, wamepewa jukumu la kuzalisha mbegu hizo za alizeti ikiwemo ya sasa ya rekodi iliyoboreshwa na kutumiwa na wakulima kuzalisha mafuta na kuongeza uzalishaji huku wakiendelea kufanya utafiti wa mbegu nyingine ili kuweza kuingizwa sokoni .Mtafiti huyo wa alizeti nchini anasema kuwa tayari katika kipindi cha mwaka 2019 wameshazalisha mbegu mama ya alizeti aina hiyo ya rekodi tani 37.8 ambazo zimeanza kusambazwa kwa wakulima katika mikoa inayolima zao la alizeti .Anasema kupitia uzalishaji wa mbegu hizo  jumla ya hekari 18,500,zitapandwa zao hilo la alizeti katika mikoa mbalimbali ambayo kwa sasa imekuwa ikizalisha zao hilo ili kuweza kuchangia kuongezeka kwa uzalishaji kiwango cha  mafuta  nchini katika mikoa iliyokewa mkakati huo ikiwemo Singida,Dodoma na Morogoro.

Reuben anasema kuwa mbegu hiyo ya rekodi ambayo imesafishwa na kuboreshwa kutokailiyokuwa mbegu ya zamani  imesambazwa kwa wakulima na uzalishaji wake umeonyesha mafanikio makubwa ambapo hekari moja inatoa kilo zisizopungua kati ya 600 mpaka 800.Mtafiti huyo wa alizeti anasema kuwa kwa sasa mbegu ya alizeti ya rekodi ndiyo inachukuaasilimia 85 katika soko na ndiyo inayochangia asilimia 90 ya uzalishaji wa alizeti nchini na kuchangia  asilimia 70 ya mafuta yanayozalishwa hapa nchini.Akizungumzia kuhusu takwimu za uzalishaji wa zao la alizeti nchini anasema kuwa umekuwa ukiongezeka ambapo mwaka 2012/16 uzalishaji ulikuwa tani 500,000  wakati mwaka 2017/18 zilifikia tani 768,188 na mwaka 2018/19 tani 820,905 zilizalishwa na kwamba mkakati  wa 2020/22 ni kuzalisha tani 500,000 ambazo zitazalisha mafuta ya alizeti tani 600,000 na hivyo kumaliza tatizo la upungufu wa mafuta nchini.

Anasema kuwa ili kufanikisha mkakati huo wa uzalishaji wa mafuta ya alizeti kufikia tani 600,000 ifikapo mwaka 2020/22 na kuondokana na changamoto ya mafuta TARI Ilonga imejipanga kutoa utafiti mwingine wa mbegu za alizeti itakayokuwa na ubora kuliko mbegu yoyote iliyoko sokoni kwa sasa ili kuongeza uzalishaji maradufu.

“ Sisi watafiti hivi sasa tunaendelea kuumiza vicha kwa ajili ya mbegu nyingine nne za alizeti zitakazokuwa na uzalishaji mkubwa pengine zozote zilizopo sokoni. Tunataka kuongeza kasi ya uzalishaji wa mafuta wa ndani ili kuondokana na kutumia fedha nyingi kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi, ” anaeleza Reuben.

WAKULIMA WAELEZAMmoja wa wakulima wa alizeti na mzalishaji wa mafuta Khalifan Hamadi, kutoka kata ya Magomeni wilayani Kilosa, anasema mbegu ya alizeti ya rekodi iliyofanyiwa utafiti na kuboreshwa na TARI Ilonga imeleta mafanikio makubwa katika uzalishaji wa zao hilo na hivyo kuwaongezea mapato yanayotokana kuuza kwa wanaokamua mafuta ya kula.

Anasema kuwa mbegu ya alizeti ya rekodi imeweza kuwasaidia kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti mara nne zaidi ya uzalishaji wa awali ambapo kabla ya matumizi ya mbegu hiyo walikuwa wakipata gunia saba kwa hekali moja.

Anasema sasa wameona umuhimu wa kuwepo kwa taasisi hiyo ya utafiti wa kilimo licha ya kuzalishiwa mbegu mbalimbali lakini pia wamekuwa wakisaidiwa kupata ushauri na utalaam wa kilimo bora cha alizeti tofauti na awali walikokuwa wakipanda kwa mazoea , bila kutumia mbegu bora na hivyo kukosa mavuno ya kutosha.

Aidha, mkulima Lethisia Semwenda ,ambaye pia hulima mahindi na mpunga kwa mda mrefu anasema sasa ameanza kushawishika baada ya kuona mavuno ya alizeti yameongezeka kwa wakulima wenzake hivyo katika msimu ujao anakusudia kuanza kulima kilimo hicho kwakuwa kimeonyesha kina faida kiuchumi baada ya kuuza au kukamua mafuta.

KUSAIDIA WAKULIMATaasisi ya kuendeleza mifumo ya kimasoko katika kilimo iliyo chini ya Serikali ya Dernmak, Ireland na Sweden  kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania imeamua kuwasaidia wakulima wadogo ,vijana na wanawake ili kuongeza fulsa katika mnyororo wa thamani wa mazao matatu kufanya kilimo biashara na chenye tija.

Meneja usimamizi, maarifa na mawasiliano wa taasisi hiyo, Al-Aman Mutarubukwa,anasema kupitia mradi huo, wamelenga kuyasaidia makundi hayo kwenye mazao ya alizeti,mahindi,maharage na mbaazi ili waongeze mnyororo wa thamani kuanzia uzalishaji, usindikaji na masoko ndani na nje ya nchi.

Anasema kwa sasa wana miradi 11 iliyopo katika mikoa 15 na kwamba miradi mitatu inahusisha zao la mahindi katika mikoa nane ili kuongeza thamani ya nafaka.

Mutarubukwa anasema kwa zao la alizeti,mbaazi na maharage miradi hiyo ipo katika mikoa ya kusini ikihusisha Mtwara na   Lindi, Manyara, Mbeya, Njombe, Iringa, Dodoma na Singida na tayari makundi hayo yamenza kunufaika.

Anasema kupitia mpango huo wamelenga kubadilisha mifumo ya usambazaji na mifumo bora ya mbegu bora ya alizeti ambapo kwa miaka mitatu iliyopita hakukuwa na mbegu bora sokoni na taasisi hiyo kwa kushirikiana na kampuni ya uzalishaji mbegu ya alizeti ya ndani na nje wameingiza mbegu chotara zilizoboreshwa na kuwasambazia wakulima ambao wameongeza uzalishaji ili kupata tija.

“ Kwa miaka miwili iliyopita wakulima walikuwa wakitumia mbegu zilizozoeleka  na kutoa mavuno kidogo wastani wa magunia matatu kwa hekari lakini baada kuleta mbegu za chotara mavuno yameongezeka yamefikia wastani wa gunia 15-18,”anasema Mutarubukwa,Mutarubukwa, anataja ushirikiano kuwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti ya TARI, wameboresha mbegu yarekodi ya alizeti na kuweza kuongeza uzalishaji kwajili ya kukidhi mahitaji ya viwanda vya kutengeneza mafuta ya kula.

MKURUGENZI MKUU

Mkurugenzi TARI Dk Geofrey Mkamilo, anasema kuwa kabla ya kuanzishwa kwake Ilonga kilikuwa kituo cha Utafiti na kiliweza kuzalisha mbegu za alizeti wastani wa tani 2.3 ambazo zilikuwa zikitumika kwajili ya mashamba yake lakini kwa mwaka wa kwanza  baada ya kuundwa kwa taasisi hiyo uzalishaji wa mbegu umeongezeka na kufikia tani 7.5.

Dokta Mkamilo, anasema mkakati wa TARI ni kuwa ifikapo mwaka 2020 /22 wazalishe mbegu za alizeti tani 1.5 ambazo zitakuwa na uwezo wa kutoa mafuta wa kutoa mafuta ya kula ya alizeti tani 600,000 na hivyo kupunguza kwa kiwango kikubwa wa uagizaji wa mafuta kula kutoka nje ya nchi.

Mkurugenzi huyo Mkuu wa TARI anasema mabadiliko hayo makubwa yaliyofanywa inatokana na kuongezewa majukumu ya kuzalisha mbegu kwa wingi wa mazao mbalimbali  ili kuwauzia  wakulima waweze kuzalisha mazao yatakayotumika kama malighafi ili kusaidia juhudi za serikali katika kujenga uchumi wa viwanda hapa nchini.

Anasema kuwa kupitia mpango huo, TARI imelenga kuwabadilisha wakulima kutoka kilimo cha kujikimu na kwenda katika kilimo biashara ili kuongeza uzalishaji kwa taifa na hivyo kuwepo kwa uhakika na usalama wa chakula.

Mkamilo,anasema kuwa watalaam wa utafiti kutoka taasisi  18 nchini wamewekewa mkakati maalumu wa kuhakikisha wanazalisha teknolojia za mbegu bora za kisasa na zenye ukinzani na magonjwa kwa mazao ya kimkakati likiwemo zao la alizeti linalozalishwa Ilonga kwa ajili ya kutatua changamoto ya upungufu wa mafuta nchini.

Anasema chini ya mkakati huo wa miaka mitano teknolojia za  mbegu za kisasa  zitakazozalishwa ambazo zitakuwa na ukinzani na magonjwa zitasambazwa na kumfikia mkulima kwa muda mfupi na kuuziwa kwa bei ya chini ili kuwasaidia kutumia teknolojia hizo kuongeza uzalishaji.KUSAMBAZA MBEGU

Mkurugenzi wa TARI Ilonga, Dk Joel Meriyo, anasema kuwa wameanza kwa vitendo mkakati wakusambaza kwa wakulima teknolojia za mbegu za kisasa za alizeti, mkikunde na mazao ya nafaka kama mahindi,mtama na uwele ili kuwasaidia wakulima kuondokana na kilimo cha mazaea na kulima kisasa ili kuzalisha malighafi zinazotokana na mazao ya kilimo kwajili ya kulisha viwanda.

Anasema watafiti wa TARI Ilonga,tayari wameanza kuwakusanya watalaam wa kilimo na ugani kutoka katika kata zote kwa kuanzia Wilaya ya Kilosa na baadae kwenda katika wilaya nyingine katika mkoa wa Morogoro .

Lengo ni kuwapa mafunzo maalumu ya kuhusu teknolojia za mbegu za kisasa ili kwenda kutoa elimu kwa wakulima kwa kuwaelezea na kuwafundisha ili waweze kuzitumia ili kuongeza uzalishaji.

Dk Meriyo, anasema kuwa mpango huo utawafanya watafiti wa TARI Ilonga kuwafuata wakulima katika kata zote kwa kuanzia na Wilaya hiyo, kuwafundisha wakulima kuhusu kilimo bora cha kisasa na chenye kutumia teknolojia za mbegu za kisasa ili waweze kubadilika na kuachana na kilimo chenye mazoea na kufanya kilimo cha kibiashara ili kuwa na uhakika wa chakula na ziada.

Akizungumzia kuhusu mkakati wa zao la alizeti, anasema kuwa pamoja na TARI Ilonga kupewa majukumu ya kuzalisha mbegu za kisasa za alizeti ili kuongeza uzalishaji wa mafuta hapa nchini teknolojia zote za mbegu za kisasa zinazofanyiwa utafiti zikikamilika na kuzalishwa mbegu zitasambazwa haraka kwa wakulima katika mikoa inayolima zao hilo kwa wingi.

MRATIBU WA UTAFITIMratibu wa Utafiti Kanda ya Mashariki kutoka TARI Ilonga, Meshack Makenge, anasema jukumu kubwa kwao ni kuzalisha mbegu za teknolojia ya kisasa na kuzisambaza kwa wakulima ili waweze kufanya kilimo cha kisasa na chenye tija na cha kibiashara kwa ajili ya kulisaidia taifa liweze kuwa na uhakika na usalama wa chakula.

Makenge ambaye ni Mtafiti wa Kitaifa wa Mikunde anasema kuwa TARI Ilonga pia imepewa jukumu la kuzalisha mazao ya mikunde kama choroko, maharage, dengu na mbaazi ,mazao ya nafaka kama mahindi, mtama na uwele pamoja na mazao ya mbegu za mafuta kama alizeti na mazao ya mizizi kama mihogo na viazi lishe na kuhakikisha teknolojia hizo zinawafikia wakulima.

Anasema kuwa katika mpango wa serikali wa kuelekea uchumi wa viwanda,TARI Ilonga imejipanga kikamilifu kuhakikisha inakuwa injini ya kuwepo kwa viwanda hivyo na kwa sasa wameamua kuwasaidia wakulima kulima kwa kutumia mbegu za teknolojia ya kisasa ili kuweza kuzalisha malighafi zinazohitajika katika viwanda hivyo vilivyoanza kujengwa hapa nchini.

UMWAGILIAJI

Ofisa Kilimo, Umwagiliaji na  Ushirika wa Wilaya ya Kilosa Elina Danstun , anasema mkakati wa wilaya hiyo katika msimu ujao wa kilimo ni kuongeza uzalishaji wa chakula na ziada ili kusaidia mpango wa Serikali katika kuelekea uchumi wa viwanda hivyo mafunzo ya teknolojia hizo watayafikisha  moja kwa moja kwa wakulima.

Hata hivyo, anasema bado kumekuwapo na mitazamo hasi kwa baadhi ya wakulima kuendeleakufanya kilimo kisichofuata kanuni zilizowekwa ikiwemo matumizi ya mbegu bora na pembejeo kwa wakati na hivyo kupitia mafunzo hayo watahakikisha wanawabadilisha wakulima wa wilaya hiyo ili waweze kuongeza tija ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula.

WAZARA YA KILIMONaibu Waziri wa Kilimo ,Omary Mgumba,alipotembelea taasisi hiyo anasema TARI Ilonga inawajibu wa kuendeleza utafiti katika mazao yanayozalisha mafuta ili kuwapatia wakulima mbegu bora kama ya alizeti waweze kuzalisha mafuta na kutatua changamoto za serikali kutumia fedha nyingi kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.Anasema kuwa taasisi hiyo iendelee kufanya kama kwa mazao kama ya nafaka ikiwemo mtama,uwele,ulezi,mbaazi,kunde,choroko ,soya ,dengu na njugu mawe pamoja na alizeti ili kuwasaidia wakulima waweze kuyatumia kwajili ya kufanya kilimo biashara.

Aidha Naibu Waziri  Mgumba anaesema serikali  imeipa jukumu TARI kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za aina mbalimbali  ili kukidhi mahitaji ya wakulima  kuweza kupata mbegu za teknolojia ya kisasa ambazo zitatumika kwa ajili ya uzalishaji wa malighafi zinazohitajika katika uchumi wa viwanda.

Habari Kubwa