TARI Mikocheni yaibua shangwe wakulima minazi

18May 2022
Gerald Kitabu
Nipashe
TARI Mikocheni yaibua shangwe wakulima minazi
  • *Yawasambazia miche ya kisasa inayozaa nazi 100

TAASISI ya Kituo cha Utafiti wa Kilimo -TARI Mikocheni Dar es Salaam, imemaliza hofu ya kutoweka kilimo cha minazi nchini baada ya kutafiti,  kugundua na kusambaza kwa wakulima mbegu mpya ya kisasa na himilivu ya  East African Tall (EAT), inayozaa nazi takribani 100.

Wakurugenzi wa TARI, Dk. Joseph Ndunguru (kushoto) wa Mikocheni, Mkurugenzi Mkuu, Dk. Geoffrey Mkamilo na Mratibu Dk. Fred Tairo, wakimkabidhi Asha Msangi wa Wilaya ya Mtama miche bora ya minazi aina ya EAT. PICHA: GERALD KITABU

Kuzorota kilimo cha minazi nchini, kulianza miongo takribani mitatu iliyopita baada ya wakulima wa ukanda wa pwani waliokuwa wanalima zao hilo kulalamikia kilimo hicho kuathiriwa na magonjwa na upungufu wa mazao.

 

Miti ya minazi iliyokuwa inalimwa zamani ilikuwa inazaa  kati ya nazi tano mpaka 18 wakati ya sasa inazaa matunda  30 hadi 90.

 

Hayo yanaelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini TARI, Dk. Geoffrey Mkamilo,  wakati wa kugawa miche bora na ya kisasa aina ya East African Tall (EAT), kwa  wakulima wa ukanda wa pwani kutoka mikoa ya Lindi, Tanga, Mtwara na Pwani.

 

Katika maeneo mengine ya ukanda huo, baadhi ya wakulima waling’oa  minazi na kupanda mazao mengine yenye faida kutokana na sababu mbalimbali kama miti  kuzeeka, ukame na magonjwa, anaongeza.

 

Anasema serikali inataka kuona zao hilo lenye manufaa mengi likirudi katika ubora wake na kuchangia vilivyo katika uchumi wa taifa na kipato cha wakulima.

 

Anasema nazi inachangia kupata  mafuta ya kupikia pia ni zao la biashara kwa watu wengi hasa kinamama na vijana, huongeza afya na virutubisho pamoja na kuhifadhi mazingira.

 

“Zao hili ni muhimu. Kina mama na vijana wengi hususani wa mikoa ya pwani wanafanya biashara ya kuuza nazi. Wengine wanazitumia kupikia, vijana nao wamejiajiri kuuza madafu. Kwa hiyo ni lazima tuhakikishe tunaliendeleza kwa kugawa mbegu bora aina ya EAT,” anasema.

 

Anawataka wakulima na wakazi wa mikoa ya pwani kuzingatia maelekezo ya watafiti ikiwamo kilimo bora, kuandaa mashamba kikamilifu, mapema na pia kuchukua mbegu bora kutoka TARI ili wasichukue ziizochakachuliwa na wauza mbegu ambao hawatambuliki.

 

“Wanawake na vijana wanaweza kujiingiza katika hatua mbalimbali za uzalishaji wa nazi kuanzia kulima, kufanya biashara au kwenye mnyororo wa thamani na kujipatia kipato na familia zao,” anaongeza.

 

Aidha, anazitaka halmashauri kuanzisha mashamba ya mfano na kutenga bajeti ya kutosha kuendeleza minazi hiyo katika maeneo yao.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti cha TARI Mikocheni, Dk. Joseph Ndunguru, anasema sababu kubwa ya kuweka juhudi kubwa katika kufufua zao hilo ni kuhakikisha upatikanaji wa mafuta ya kula nchini.

 

Hivi sasa nchi inapambana kupata mafuta ya kula ya kutosha. Tuna upungufu wa mafuta hali inayosababisha taifa kutumia fedha nyingi kuyaagiza nje. Tunataka zao hili lichangie upatikanaji wa mafuta hayo,” anasema.

 

Anaongeza kuwa juhudi hizo zinalenga pia kuwapatia kipato wananchi wengi wa maeneo hayo ya ukanda wa pwani.

 

Anasema kutuo cha ufafiti TARI Mikocheni kinagawa miche bora ili kubadilisha kilimo hicho kutoka kwenye kiwango  cha kujikimu kwenda kwenye kilimo cha kibiashara.

 

Anasema wananchi wana uwezo wa kupata mazao mengi na kuwekeza katika biashara za ndani na nje.

 

Akitolea mfano anasema mbali na  kupata mafuta ya kupikia, wananchi wanaweza pia kuuza mbao au  kutengeneza samani (fenicha) na kujipatia  fedha.

 

 “Kwa kushirikiana na halmashauri na serikali za mitaa tunataka kulifufua ili  lianze kuzalishwa hata katika maeneo ambayo miche ya zamani ilikufa kutokana na changamoto mbalimbali,” anasema Dk. Ndunguru.

 

Anaeleza kuwa kampeni hiyo imeanzia wilayani  Pangani mkoa wa Tanga, na sasa inafanyika Mkuranga mkoa wa Pwani na  Mtama mkoa wa Lindi.

 

Anasema katika wilaya hizo Kituo cha Utafiti wa Kilimo Mikocheni kitaanzisha vitalu ambavyo vitatunzwa na kuhudumiwa na halmashauri za wilaya kwa ajili ya wananchi wao.

 

Wakulima wanawake na vijana watatumia vikundi vidogo vidogo kuingia katika kilimo na biashara ya zao hilo.

 

Wakipokea mbegu hizo, wawakilishi wa Halmashauri za Wilaya za Mkuranga na Mtama, Julita Bulali na Asha Msangi wanashukuru serikali na  TARI Mikocheni kwa mbegu hizo na kuongeza kuwa zitakuwa na tija kwa wakulima wa maeneo yao.

 

“Zao la minazi lilianza kutoweka taratibu na kipato cha wananchi kushuka kwa baadhi ya maeneo kutokana na sababu za magonjwa na ukame wa wastani. Wananchi wanayo furaha kubwa sana kupata miche bora,” anasema Julita.

 

Anawataka wananchi wa Wilaya ya Mkuranga kuingia kwenye kilimo hicho hususani katika mlolongo wa thamani ili kupata fedha na kutunza mazingira yao.

 

Mwailishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama mkoani Lindi Asha Msangi, anawataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo ili kujipati kipato na kujiletea maendeleo.

 

TARI-Mikocheni ni moja kati ya vituo 17 vya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini, kilichoanzishwa kwa lengo la kufanya utafiti na kuendeleza minazi lakini kufanya majukumu mengine ya baioteknolojia.

Habari Kubwa