TASAF yawanusuru waliokata tamaa kuendelea na masomo

23Feb 2021
Marco Maduhu
Kahama
Nipashe
TASAF yawanusuru waliokata tamaa kuendelea na masomo

MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini, ulioanza mwaka 2002, una mengi ya kujivunia ikiwamo kusaidia watoto wengi kusoma.

Mwaka 2015 serikali ilitangaza kutoa elimu bure kuanzia wanafunzi wa shule za awali hadi sekondari kwa lengo la kusaidia kupata elimu bila ya kujali hali za uchumi wa familia zao.

Licha ya serikali kugharamia elimu zipo baadhi ya kaya zinashindwa kuwapeleka watoto shule kutokana na ukosefu wa fedha za kumudu mahitaji kama sare, daftari, kalamu na chakula.

Kupitia ruzuku yenye masharti fedha hizo zitumike kupeleka watoto shule na kuwanunulia mahitaji, hali hiyo ilianza kurudisha matumaini ya wanafunzi waliokata tamaa na shule kuendelea na masomo.

Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga, ni miongoni mwa maeneo ambayo shule za msingi zilikuwa na tatizo la wanafunzi wanaotoka kwenye kaya maskini kuwa watoro shuleni na wengine kuacha masomo.

Sababu ya changamoto hiyo inatajwa kuwa ni kukosa mahitaji muhimu ya shule na kwamba TASAF kuwa mkombozi.

Modesta Alphonce ni miongoni mwa watoto ambao wazazi wao ni wanufaika TASAF, anayesoma darasa  saba katika Shule ya Msingi Wichamike, iliyoko Kijiji cha Ntobo.

Anasema kabla ya wazazi wake kuingia TASAF, alikuwa mtoro shuleni sababu ya kukosa mahitaji muhimu kama sare na daftari.

Anasema baada ya kukosa mahitaji hayo alijiingaza kwenye kazi za kulima vibarua kwenye mashamba ya watu binafsi na wazazi wake, ili wapate fedha ya chakula, pamoja na na mahitaji mengine.

"Nilikuwa nimeshakata tamaa kusoma, kutokana na nyumbani kwetu kuwa maskini, na kushindwa kunitimizia mahitaji ya shule, sababu huwezi kwenda shule bila ya kuvaa sare, viatu wala kuwa na daftari, na ukizingatia mimi ni mtoto wa kike bado na mahitaji mengine yalikuwa yananisuburi " anasema Modesta.

"Baada ya wazazi wangu kuingia kwenye mpango wa TASAF, maisha yalibadilika na sikuweza tena kuwa mtoro shuleni. Ufaulu umeongezeka sababu sikosi masomo tena. Nimetoka kushika nafasi ya 40 na sasa nashika ya 10," anaongeza Modesta.

Mwanafunzi Faida Joseph, anayesoma darasa la saba katika shule ya Wichamike, anasimulia kuwa baada ya kukosa mahitaji hayo muhimu ya shule, alikata tamaa na masomo na kwenda kuchunga mifugo.

"Tangu nikiwa darasa la kwanza nimesoma kwa shida kutokana na wazazi wangu kuwa maskini na kushindwa kuninunulia mahitaji ya shule kama sare, viatu, madaftari, na baada ya kufika darasa la nne nikaona maisha ya shule ni magumu ikabidi nianze kuwa mtoro," anasema Sahani.

"Nilipokuwa nikiwaeleza wazazi wangu waninunulie sare za shule na madaftari wanasema hawana hela maisha yao magumu, ndipo na mimi ikabidi niwe mtoro shule na kwenda kuchunga ng'ombe," anaongeza Sahani.

Aidha, anaeleza baada ya familia yao kuingizwa kwenye mpango huo wa kaya maskini, alinunuliwa sare za shule na mahitaji mengine sasa anafanya vizuri kitaaluma akishika nafasi ya 13 kutoka ya 50.

Helena Mtaki ni mwalimu mlezi wa Shule ya Wichamike, anasema TASAF imekomboa wanafunzi wanaoishi kwenye umaskini baada ya kuwapatia mahitaji ya shule yaliyowawezesha kuacha utoro.

Anasema mara baada ya kuona kuna baadhi ya wanafunzi wamekuwa watoro sugu, alifuatilia taarifa zao na kugundua kuwa ni wale wanaoishi maisha duni, walioshindwa kwenda shule sababu ukosefu wa sare za shule na hata zile walizokuwa nazo zimechanika  na pia hawana fedha za kununua daftari kubwa kama kaunta zinazotumiwa na  wanafunzi darasa la saba..

“Watoto hawa wana akili na wanafanya vizuri darasani mara baada ya kuhudhuria masomo bila kukosa kumekuwa na mabadiliko.  Serikali inatoa elimu bure lakini baadhi ya familia maisha yao ni magumu na wamekuwa wakishindwa kuwahudumia watoto hasa upande wa mavazi, sare na hata chakula nyumbani.” Anasema.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Wichamike,  Restuta Respicius, anasema utoro shuleni umeisha kwa watoto hao wenye maisha magumu siyo kama zamani, mara baada ya TASAF kubadili mfumo wa maisha yao, ambapo wazazi wao kwa sasa wanajishughulisha na kilimo, pamoja na ufugaji mifugo kupitia fedha za TASAF.

Mmoja wa wazazi ambaye yupo kwenye mpango huo wa TASAF, Pili Maige mkazi wa Ntobo- Msalala, anasema kwa sasa maisha yake yamebadilika, ana miliki mbuzi sita, ana kuku na baadhi ameshauza, kwa ajili ya kuhudumia watoto mahitaji yao ya shule, pamoja na kununua chakula.

Anasema awali kabla ya kuingia TASAF mwaka 2015, maisha yake yalikuwa magumu na alikuwa akishindwa kuwatimizia watoto wake mahitaji hivyo kuamua kwenda nao kwenye mashamba binafsi kulima vibarua ili apate fedha za kuwanunulia sare za shule na madaftari, huku wakiwa tayari wameshakosa masomo kwa muda mrefu.

“Baada ya kupata ruzuku TASAF, nilianza kutunza akiba ya fedha huku nyingine nikitumia, ambapo baadae nilinunua kuku wawili, mbuzi jike ambaye ameshazaa. Nimeongeza mbuzi wengine na sasa wako tisa,” anasema Maige.

Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Msalala Elikana Zabloni, anasema kwenye halmashauri hiyo kuna walengwa 4,128, na mwaka jana (2020) kuanzia Agosti hadi Oktoba, wameshatoa Sh. milioni 256.

Anabainisha kuwa kabla ya kuwapa fedha hizo wanawapa elimu ya kuwekeza kwenye kilimo, na ufugaji ili wajikwamue kiuchumi.

Anasema kwenye utoaji wa ruzuku hiyo kuna masharti ya lazima ambayo ni pamoja na kuwa na  Bima ya Afya Iliyoboreshwa (CHF), pamoja na kuwapeleka watotoni, kuwapa  mahitaji yao, ikiwamo ununuzi wa sare za shule na mahitaji mengine ambayo Mwanafunzi anapaswa kuwa nayo.

Aidha anasema kutokana na fedha hizo mwisho wake, ndipo wanaamua kuwajengea uwezo walengwa namna ya kuzitumia kujikwamua kiuchumi, kwa kujikita kwenye shughuli za kilimo cha biashara na ufugaji wa mifugo, ili waendelee kupata fedha za kusomesha watoto wao licha ya mpango huo kufika kikomo.

“Hali ya maisha ya walengwa wa TASAF Msalala ni nzuri siyo kama zamani, ambapo kama ulivyoona kila kaya kuna mifugo na wengine  shamba la kilimo cha biashara yakiwamo machungwa na pamba. Mazao yanauzwa ili kujipatia pesa zinazojenga nyumba bora,”anasema Zablon.

Habari Kubwa