Tatizo la kujiua linavyotesa fikra, maadili tangu zamani

14May 2019
Michael Eneza
DAR ES SALAAM
Nipashe
Tatizo la kujiua linavyotesa fikra, maadili tangu zamani

HAKUNA jambo ambalo linatesa fikra ya jamii kama tatizo la mtu kuamua kukatisha maisha yake mwenyewe, jambo ambalo katika sheria ni kosa la jinai, lakini sheria inachukua mkondo wake tu endapo jaribio hilo halikufanikiwa.

Mara nyingi zaidi dhamira ya kujiua inafanikiwa kwa hiyo inakuwa ni janga la kifamilia na kijamii kwa upande mwingine, kwani lawama hiyo ya kisheria na hata uvunjifu wa sheria siyo rahisi urudiwe katika ngazi ya familia na jamii, ila huzuni kwa yaliyotokea hadi mhusika au marehemu akashindwa kumudu maisha kiasi cha kuchukua uhai wake.

Kuna chembe ya kujiri kuonewa kwake, kupungua kimaadili kwa jamii.

Ina maana kuwa mtu anapojiua anaihukumu jamii kwa kilichotokea, kwani kwa kawaida kila mtu ana aina ya mzunguko wa watu ambao wanatazamiwa kumjali, na inapofikia hatua ambako mtu haoni faida ya kuonana na watu wengine, au kuendelea na kile kinachoitwa kwa kawaida ni kufurahia maisha, kuna tatizo kubwa mahali.

Huzuni na mkasa wa kimaadili katika suala hilo ni kuwa ni jambo linalotesa wahusika kijamii kimyakimya, kwani hapatakuwa na nafasi ya kuulizana kibagaubaga nani alikosea katika jambo gani, kama ingeweza kurekebishwa, na kimsingi hakuna anayetaka ahojiwe, na hakuna anayeweza kukubaliana na tukio. Pia hawezi kulaumiwa mfu.

Kuna tofauti kati ya kifo cha kujitakia na kile cha kutakiwa na wengine, lakini pale mhusika wa kifo cha kutakiwa na wengine anapokiruhusu, anaitia jamii husika katika majaribu makubwa kujitizama upya kimaadili, na mara nyingine mfumo mzima wa kimaadili wa jamii hiyo unaathirika.

Ndiyo ilivyokuwa katika historia, kwa watu wawili wanaofanana, na hata majina yao ni kama yanaendana, yaani mfikiriaji wa Kiyunani Socrates, na mhubiri wa Kiyahudi aitwaye Yesu, au yule Kristo.

Socrates alikuwa akipita maeneo mengi, siku hizi ingeitwa ni mihadhara, akifundisha watu jinsi ya kufikiri, hasa kujitambua na kutambua kinachokuzunguka, kwa usahihi.

Ni katika mazingira hayo ambako Socrates aliingia katika mzozo na wakuu wa mji wa Athens, zaidi kidogo ya miaka 300 kabla ya Kristo, na wakati mmoja akahukumiwa kifo kwani mafundisho yake yalikuwa yanapingana na maelezo ya makuhani katika mahekalu ya miungi ya Wayunani.

Alipotupwa gerezani ili hukumu ya kifo itekelezwe, alipewa nafasi ya kutoka gerezani kana kwamba ametoroka, halafu aondoke katika mji huo aende kuishi kwingine.

Sababu ilikuwa kwamba wengi kati ya wanajamii na hata baadhi ya watawala na askari wa mji huo walikuwa wanafurahia mafundisho yake, huku wakiona bayana kuwa yanahatarisha uimara wa dini yao.

Jambo la kushangaza ni kuwa Socrates aliamua kubaki hapo gerezani hadi hukumu hiyo itekelezwe, au uamuzi mwingine ufikiwe kisheria kuwa atoke, lakini siyo atoroke kwani hapo atakuwa amevunja sheria, kwa mantiki kuwa kutekelezwa kwa hukumu hiyo ilikuwa ni sehemu ya kuitii sheria.

Ikafika siku ya kutekelezwa kwa hukumu na Socrates bado yuko hapo gerezani hivyo hukumu hiyo ikatekelezwa kwa yeye kupewa kikombe chenye sumu (kinywaji) naye akijua hivyo, akanywa na akafariki dunia.

Sheria na dhana nzima ya uadilifu kisheria Uyunani ukatetemeka, mpangilio wa fikra ukaanza upya na alichosema Socrates kikawa ndiyo mwanzo wa fikra mpya.

Cha msingi kilichobadilika ni kuwa mizimu (au wao wanasema miungu) wakaondolewa kama mojawapo ya nyenzo za uthibitisho wa chochote kile ila fikra, na ndiyo mwanzo wa kuondolewa kwa dhana ya kuthibitisha maadili au usahihi wa chochote kile kwa kunukuu maandiko ya dini au dhehebu.

Mazingira hayo yalishamiri kwa kipindi kifupi kama mapokeo ya wasomi, na baada ya miaka 300 mazingira hayo yakaathiri kukua kwa msukumo wa aina tofauti unaofanana na ule wa Socrates, yaani kifo cha mhubiri wa Kiyahudi ambaye wengi walimtazamia awe Masihi, ila hakuiendea njia au mwelekeo waliotazamia.

Alipohukumiwa kifo na kukataa kufanya ishara au muujiza wowote ili asiuawe kikatili kwa mtindo wa kumpigilia mtu msalabani, dini ikayumba.

Suala la kujiua ni moja ya maeneo yaliyowezesha kuanza kwa taaluma ya miingiliano ya kijamii (sociology), kwani kuanzia miaka ya 1850 nchini Ufaransa wimbi la wasomi wa masuala ya jamii wasiotaka kuendea fikra zinazoelekea katika 'mabadiliko, maendeleo na mapinduzi' lilijengeka.

Suala lilikuwa mshtuko wa usomi nchini humo kutokana na mkasa wa Mapinduzi ya Ufaransa mwaka 1789 ambayo yalitokana na mivutano ya karne nyingi kati ya tabaka la watwana wanaotoa kodi ya ardhi kwa mamwinyi wanaoimiliki, halafu na wafanyabiashara ambao wakati huo walitaka wawe huru wasitawaliwe na kodi maridhawa zinazowekwa na mamwinyi, wakisimamia na utawala wa kifalme.

Halafu kukawa na mageuzi ya kidini Ulaya nzima, yakaleta maafa mengi.

Dhana ya weledi bila ukinzani (positivism) ilifuta hulka ya kutaka kujua chanzo cha hiki au kile, na badala yake kutafuta kama kuna uhusiano kati ya kitu kimoja na kingine.

Kwa mfano badala ya kuyakinisha chanzo cha kujiua na kutaka kuunda kanuni ya maadili kutokana na chanzo kinachofikiriwa, ni rahisi zaidi kuyakinisha ni aina gani za watu wanajiua, na kama kuna mazingira maalum ya mtu kujiua, kutafuta kama kuna chembe au taswira za kimazingira zinazoashiria hali hiyo, halafu zipimwe kuona kama zinaoana, kuendana.

Kwa njia hiyo mtu anapata picha ya aina ya watu wanaoweza kujiua, lakini haingii katika mtego wa kuyakinisha sababu husika.

Hivi karibuni mjadala ulikuwa unasikika katika moja ya vituo vya redio ambako mchangiaji mmoja kutoka Arusha alisema kuwa walifundishwa katika darasa la theolojia Chuo Kikuu Makumira kwamba wanaojiua zaidi ni watu wenye wake au wenza, kwa maana kuwa wanaume wanajiua zaidi ya wanawake. 

Kwa vile mchangiaji alisema walifundishwa darasani chuoni, ina maana kuwa tafiti zinaonyesha kuwa hali hiyo ina vielelezo vingi, lakini kuna suala la umri wa wanaojiua, hata kama ni wanandoa au wana unyumba, kuishi pamoja.

Pia kuna mazingira ya mahusiano ya vipato, umri wa kiuhusiano, kama ni wanandoa au wenza wenye umri unaofanana au kupishana kwa kiwango gani.

Vielelezo hivyo hutoa picha, hivyo mtu anaweza kutafakari mengine yaliyobaki.

Kutumiwa kwa vigezo vya mahusiano na idadi za watu wanaojiua ni njia ya kuondoa mkanganyiko wa kutoa sababu za watu kujiua, kila mtu akiongea ya kwake, na pia kutafuta kama kuna kanuni au mazingira ya jumla ambayo yakifikiwa huleta hatari ya mtu kukwama katika mahusiano, akwame pia kifikra, ajiue. Unaweza pia kuangalia hisia za kijinsia katika mjadala huo, kwani watangazaji walianza kubishana ambako mtangazaji wa kike alijaribu kuainisha kuwa tatizo ni kuwa mtu huyo (aliyejiua) alichagua sura na hakumfahamu mwenza kwa ndani.

Waliobaki hawakuwa na uhakika huo, kwani unakutana na mtu umpende; mengine utajua hapo baadaye.

Habari Kubwa