Tija mazao bila mmomonyoko milimani, rutuba na kupendezesha ardhi

10Jun 2021
Gideon Mwakanosya
Mbinga
Nipashe
Tija mazao bila mmomonyoko milimani, rutuba na kupendezesha ardhi

UNAPOTAJA ngoro, ni aina ya kilimo kinachohifadhi mazingira kwa njia ya asili, kikiaminika kuanza kutumiwa na wakulima kabila la Wamatengo wilayani Mbinga, mkoa wa Ruvuma, zaidi ya miaka 300 iliyopita.

Mbunge Mstaafu wa Mbinga  Ngwatura, Ndunguru akielezea mfumo wa kilimo cha ngoro, unaonendeshwa na jamii ya Wamatengo, kwa namna tofauti. PICHA: MTANDAO.

Ngoro inatajwa kuanzishwa na wazee maarufu wa kabila la Wamatengo waliotoka nchini Malawi katika karne ya 17. Historia inaonyesha ni vizazi zaidi ya 10, tangu kilimo cha Ngoro kilipoanzishwa Mbinga.

Elineus Ndunguru, Mbunge Mstaafu wa Mbinga, anataja dhumuni la kuanzishwa kilimo hicho ni kuudhibiti udongo ardhini, ambao kwa kawaida huondolewa na maji au upepo kutokana na mmomonyoko wa ardhi.

Kimsingi, ni sehemu ya ardhi iliyoshiba rutuba ya kufanyia kazi mimea istawi na hatimaye kutoa mavuno mengi na bora. Nduguru anafafanua:

“Tunajua kuwa udongo ulio chini ya tabaka la juu hauna rutuba ya kutosha ya kuwezesha mazao kustawi vizuri, kutoweka kwa udongo wa juu kutoka shambani au bustani kwa njia ya mmomonyoko ni hasara kubwa, kwa vile kunasababisha upungufu wa mavuno.”

Mbunge huyo ambaye pia ni Mkurugenzi Mstaafu wa Wanyamapori nchini, anazitaja njia za kuhifadhi ardhi zinazoweza kutumiwa, inaendana na uhalisia wa hali ya hewa, miinuko, pia tambarare, zikibeba njia kuu mbinu za kienyeji na kisasa ambazo zimefanyia utafiti wa kina.

NASAHA ZA DARASANI

Hapo kuna maandiko kama ya wataaluma ambao kila mmoja anajulikana kwa jina moja, Bike katika mwaka 1938, Stenhouse  mwaka 1994,  pia Temu na Bisanda  mwaka 1966, wanaoeleza jamii ya Wamatengo walilazimika kutumia kilimo ngoro  kuhifadhi udongo mzuri kwenye miteremko ya milima yao.

Katika mashimo ya ngoro, yanapandwa mazao kama maharagwe, mahindi na ngano kwenye kingo za mashimo hayo na mkulima hufyeka shamba lake na kisha mkulima anazipanga kwenye mashimo ya ngoro.

Pia, mkulima huyo anawajibika kupindua udongo wa chini kwenda juu, anakata nyasi penye udongo wenye rutuba, anaugeuza kuwa mboji, hapo rutuba ikiongezeka.

Kitaalamu, maji ya mvua yanaposimama katika mashimo ya ngoro, yana kawaida kulinda unyevu ardhini yakikinga mmomonyoko wake na inaaminika ngoro inahusishwa na kuwapo mapango ya kuishi binadamu.

Hadi sasa, historia ya Mbinga inaonyesha kuwa zamani wananchi wa wilaya humo walikuwa na kilimo cha kuhama.

Staili yao ni kwamba, ngoro inaendeshwa sehemu moja na wanapogundua rutuba imeisha, wanahamia kwingineko kwenye rutuba na wanaendesha kilimo pasipo kujali athari za kimazingira zilijitokeza, kutokana na aina hiyo ya kilimo.

ILIKOANZIA NGORO

Historia ya kilimo hicho ni kwamba, wazee wa kabila la Wamatengo waliamua kuanzisha kilimo cha kufukia majani, ili kupata mbolea ya asili. Hapo ndipo penye mwanzo wa kilimo cha ngoro.

Walimaji waliendelea pasipo kuhama, huku wakirutubisha ardhi na kuzuia mmomonyoko wa udongo kutokana na ardhi ya Mbinga kuwa na milima yenye miteremko mikali.

Mbunge Mstaafu Ndunguru, anafafanua kuwa tangu jamii ya Wamatengo waanzishe kilimo ngoro miaka 300 iliyopita, hadi sasa wamekuwa na tija ya kuzalisha vyakula vingi na wanahifadhi mazingira kwa njia ya asili, wakizuia mmomonyoko wa udongo kutoka kwenye miteremko ya milima inayowazunguka.

Anasema kwamba wakati wanaendesha kilimo hicho cha ngoro, unapofika msimu wa mvua, maji huingia kwenye mimea na majani yaliyowekwa chini yanaoza.

Ndunguru anasema, inapofika hatua msimu mwingine, ni kawaida majani yanayoota kwenye mashimo yanafyekwa na mazao yaliyosalia yanavunwa na kutandazwa kwenye shimo, yanafukiwa tayari kuwa mboji.

Mzee John Mbunda, mwenye umri miaka 80, mkazi wa Kijiji cha Kilanga Juu wilayani Mbinga, anasema jamii ya Wamatengo walianzisha mfumo maalum wa kilimo Ngoro, zama za ujana wao walipoibatiza jina Ingoro.

Anasema, ni mfumo uliowawezesha kuendelea kulima kwenye maporomoko ya milima pasipo kusababisha mmomonyoko wa udongo au kuathiri vibaya rutuba mashambani.

Alex Ndunguru, mkazi wa kijiji cha Ilela, anasema wenyeji wa Mbinga walilazimika kubuni kilimo ngoro, ili kuhifadhi udongo kwenye miteremko ya milima Matengo na ukawa mkombozi kwa kuwa kilimo endelevu na mbadala wa mfumo wa zamani, Wamatengo walipokuwa wanaha.

FAIDA MKAKATI

Utafiti umeonyesha kwamba,   teknolojia imetoa majibu kwamba ngoro ni bora zaidi katika kilimo na wakulima wa maeneo mbalimbali wamekuwa wakifika wilayani Mbinga kujifunza namna inavyohifadhi ardhi na kutunza mazingira kwa muda mrefu.

Faida mojawapo, ni pale mvua zitanyesha na panaendelea kuwa na unyevu kutokana na maji yaliyomo kwenye shimo, huku Mbunge  Mstaafu Ndunguru, anasema wameshaanza kutangaza kilimo na kukiingiza kuwa miongoni mwa vivutio vya utalii vinavyopatikana katika Wilaya ya Mbinga pekee.

Baadhi ya wageni ambao wamekuwa wakitembea kwenye magari kupitia barabara ya Mbinga hadi Mbambabay Wilaya ya Nyasa na maeneo mengine ya milima ya Umatengo, wamelazimika kuisimama kila mara, kushangaa milima hiyo na kuchukua picha za kawaida na video.

Ndunguru anasisitiza, kilimo cha ngoro kina mvuto kwa wengi wa  ndani na nje ya nchi, hasa katika mimea  inayochomoza na kuonekana mfano wa mapambo katika milima ya Umatengo.

MRADI WA WIZARA

Wizara ya Kilimo imeanzisha mradi wa Kufufua Mifumo Muhimu ya Asili ya Kilimo Duniani (Global Importance Agricutural Heritage System- GIAHS), ili kuendeleza Kilimo asili na kumpunguzia mkulima gharama za uzalishaji.

Taarifa ya Idara ya Matumizi Bora ya Ardhi wizarani, inaeleza mradi huo unatekelezwa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), ukilenga kutambua mifumo ya asili na endelevu ya kilimo na ufugaji, ili kumsaidia mkulima.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo katika Afrika Mashariki, Tanzania na Kenya zilichaguliwa kufufua mifumo hiyo kwa kuwa zina sehemu muhimu za kuendeshea na Tanzania ilipendekeza mifumo mitatu ya kilimo asili ukiwamo, mfumo wa ngoro.

Mifumo ya asili ya kilimo ilianza kupendekezwa duniani tangu mwaka 2002 na baadhi ya zinazotumia katika kilimo ni Japan, Ufilipino,China na Ujerumani.

Habari Kubwa