TMDA yahamishia kampeni zake kusaka viwango vitakasa mikono

25Feb 2021
Devota Mwachang'a
Mwanza
Nipashe
TMDA yahamishia kampeni zake kusaka viwango vitakasa mikono

MATUMIZI ya vipukusi vitakasa mikono maarufu kama ‘sanitizer’ kama njia mbadala ya kutakasa mikono katika mahali pasipokuwapo na huduma ya maji na sabuni.

Kaimu Mkuu wa Maabara ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa, Mwanza Bugusu Nyamweru, akielezea namna mashine maalumu ya kisasa maabara, inavyofanya kazi kwenye vitakasa mikono. PICHA: DEVOTA MWACHANG’A.

Hivi karibuni kulivyozuka adha ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona nchini, wataalamu wa afya wanashauri hatua ya kwamba ni kuzingatiwa kila mara kukabiliana na usambaaji maambukizi hayo.

Kaimu Mkuu wa Maabara ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa, Bugusu Nyamweru, ana ufafanuzi kwamba matumizi ya vipukusi visivyo na ubora katika vitakasa mikono, yanahatarisha zaidi afya ya mtumiaji.

Ni matokeo yanayoangukia kwa mhusika kujisikia kichefuchefu, kutapika, maumivu ya kichwa, uoni hafifu, upofu wa kudumu, kifafa, kukosa fahamu, uharibifu wa kudumu kwa mfumo wa mawasiliano mwilini (neva), kuunguza mikono au hata kifo.

VINAVYOTENGENEZA

Nyamweru anasema, baadhi ya vipukusi vya kutakasa mikono, sehemu ya malighafi ya kuvitegeneza vina ‘vilevi’ kwa kazi maalumu ya kuua kabisa au kupunguza viini vya bakteria, ili kulinda afya ya binadamu mtumiaji.

Anataja mifano ya baadhi ya vipukusi vinavyotengenezwa viwandani ni kama hydrogen peroxide, iodine na methylated spirit.

"Wenye viwanda vinavyotengeneza malighafi ya kutengeneza vitakasa mikono (sanitizer), wazalishaji pamoja na wadau wengine wana jukumu la kushiriki katika kulinda afya za watumiaji wa bidhaa zao,” Bugusua anasema

Kwa namna gani? Anaendelea:“Kwa kuwafikishia zile zilizopimwa maabara na kuthibitishwa na mamlaka husika (TMDA) kuwa ni nzuri na haziathiri afya ya binadamu."

Akizungumza katika eneo la Buzuruga, kunakolengwa kuwapo maabara mpya ya TMDA jijini Mwanza hivi karibuni, Nyamweru anasema kuna maabara yenye mashine na vifaa vya kutosha vya kisasa, kuchunguza vipukusi, wapimaji na wataalamu.

"Sampuli za vitakasa mikono, lazima zipimwe kwa umakini kutokana na matumizi ya bidhaa hiyo, hasa maeneo ya utoaji huduma ya afya.

“Zipo ambazo zinalazimika kuzimuliwa, ili kupata kiwango kinachohitajika kwa matumizi, mfano kusafishia vidonda, mabenchi, kuta na vifaa vingine, lakini lazima ziwe na ubora," anasema Nyamweru. 

Pia, anafafanua kuwa maabara ya Kanda ya Ziwa ikiwa ndani ya miezi mitatu, imeshauchunguza sampuli 102 za vipukusi, vikiwamo vitakasa mikono vinavyotumika hospitalini.

Kaimu Mkuu wa TMDA anasisitiza kwamba vipukusi visivyokidhi viwango, vinachangia kuendelea kuwapo magonjwa yatokanayo na bakteria, kwa sababu wadudu hawafi.

Anasema: "Uhitaji wa ‘sanitizer’ (vipukusi) unaongezeka kwa wateja wa bidhaa hiyo. Ni pamoja na wajasiriamali wadogo, viwanda na kwa matumizi ya familia nyumbani.

“Sisi wataalamu tunaendelea kuboresha uchunguzi wa vipukusi Ili uwe katika kiwango cha juu, tunawashauri na kuwakaribisha Watanzania kuitumia maabara hii kwa matokeo mazuri na ya uhakika."

MCHUNGUZI TMDA

Jovinary Rwezahura, mchunguzi kutoka Maabara ya TMDA Kanda ya Ziwa, anaeleza ili kitakasa mikono kiwe na uwezo wa kuua viini vya bacteria, ni lazima kuwa na kiwango cha kileo chenye kufikia asilimia 60.

Katika hilo anasema, hiyo inafanya upimaji kupata umuhimu wa kufanyika upimaji kujidhihirisha namna kiwango hicho kimefikiwa kabla hata ya kuruhusu bidhaa kuingia sokoni.

Rwezahura anasema:"Tunafanya upimaji kutathmini na kuangalia ubora wa kiwango cha kilevi kinachopatikana katika kitakasa mikono kwa kutumia mashine maalumu ya kisasa inayoitwa 'Steam Distillation Unit’. Kilevi kinachopimwa ndiyo kiambata muhimu kinachotumika kuua viini vya bacteria au vijidudu."

Anasema, ili kuhakikisha ubora wa vipukusi, ni lazima kuwapo muda maalumu wa kuangalia wadudu waliowekwa wamekufa na tathmini ya muda wao kufikia vifo. Kufaulu ngazi hiyo, ni ishara ya kufaa kwa matumizi ya binadamu.

Waridi Msumari ni Mchunguzi wa Maikbrobailojia (wadudu wadogo) wa Maabara TMDA Mwanza, anayesema kuna njia za kuchunguza vipukusi, lakini zote lazima zifuate hatua ya awali ya kuandaa chakula cha wadudu waliooteshwa (culture media).

Pia, anasema kuna vitenganishi vitakavyotumika kabla ya kipimo cha maikrobailojia kujua uwezo wa sampuli kuua vimelea au kupunguza wadudu waliokusudiwa.

Anasema, upimaji ndani ya maabara ya maikrobailojia wadudu na kipukusi huchanganywa pamoja kwa kwa dakika 10, kisha mchanganyiko huo huwekwa kemikali maalum, kabla ya tathmini iwapo imefanya kazi ya kuua vijidudu.

Mtaalamu huyo anafafanua kuwa sampuli iliyochanganywa na wadudu waliooteshwa huwekwa kwenye kifaa maalumu mithili ya sahani na kuingizwa kwenye mashine ya atamizi inakoachwa kwa muda maalumu, kabla ya kuangalia kama wadudu wameota au la.

Anasema, wadudu kwenye ‘incubator’ huota baada ya saa 24 mpaka 48 kama vile bakteria, lakini fangasi huchukua siku tano. 

MKUU MAWASILIANO

Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma TMDA, Gaudensia Simwanza, anaeleza kwamba kabla ya mashine hiyo ya 'Steam Distillation Unit’ kununuliwa, wachunguzi walitumia mashine iitwayo ‘refractometer’ ambayo ufanisi wake pia ulikuwa mzuri.

Gaudensia kuwapo uhitaji mkubwa wa bidhaa ikanunuliwa yenye uwezo mkubwa zaidi, akifafanua:
"Kwenye Maabara yetu ya Dar, sampuli zilipimwa kama kawaida na ‘refractometer’ ambayo ilikuwa inapima lakini majibu yake yalikuwa yanatoka baada ya dakika 10, lakini hii inayotumika sasa inapima na kutoa majibu sahihi ndani ya dakika nne."

Anakumbusha kwamba hitaji la vitakasa mikono haliishi kwa matumizi kukabiliana na ugonjwa corona, bali ni la kila siku katika afya.

Habari Kubwa