Tofauti 5 kati ya Messi na Ronaldo

25Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Tofauti 5 kati ya Messi na Ronaldo

LIONEL Messi na Cristiano Ronaldo wametawala mazingira ya mpira wa miguu kwa miongo miwili kama vile hakuna wengine.

Wawili hao ambao ni wapinzani wakubwa kwenye soka, walichomoza katikati ya miaka ya 2000, wana jumla ya tuzo 11 za Ballon d'Or kwa pamoja, viatu kumi vya Dhahabu Ulaya, na mataji tisa ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, kati yao.

Wote wawili wana rekodi nzuri za kufunga mabao. Ni wachezaji wa mchezo mkubwa na wamekuwa wakifanya tofauti kwa klabu na nchi kwa miaka kadhaa sasa. Muhimu zaidi, wameonja mafanikio katika kiwango cha klabu na kimataifa, na kuwafanya kuwa wachezaji bora zaidi katika historia ya mpira wa miguu duniani.

Licha ya kufurahia kiwango sawa cha mafanikio kwenye mchezo huo, Messi na Ronaldo kuna vitu vingi hawafanani kabisa. Kuna mambo mengi ambayo huwatofautisha wawili hao.

Kwenye makala haya tunaangalia tofauti zao tano, zifahamu hapa...

#5. Mbinu za kimchezo

Jambo moja kubwa linalomtofautisha Messi na Ronaldo ni mbinu ya mchezo. Kwa miaka mingi, tumeshuhudia wawili hao wakitumia mbinu tofauti kabisa.

Ronaldo ni mshambuliaji wa moja kwa moja, wa haraka na mkali ambaye anaweza kuumiza safu ya ulinzi wa upinzani kwa urahisi zaidi kutokana na staili yake. Ronaldo anafanikiwa zaidi wakati anapotokea upande wa kushoto akikimbia kwa kasi kuelekea eneo la boksi na kutengeneza hatari.

Kwa upande wa Messi ana mtindo wa kiufundi zaidi. Nahodha huyo wa zamani wa Barcelona anategemea uwezo wake binafsi wa kumiliki mpira na kupiga chenga kuelekea eneo la hatari. Yeye pia hupenda kuingia eneo la sanduku, lakini akitokea upande wa kulia.

#4. Uwezo wa kumalizia/Staili ya kushambulia

Messi na Ronaldo bado ni wachezaji wawili ambao wanaogopwa zaidi wanapokuwa eneo la hatari. Mreno huyo ana wastani mzuri zaidi wa kufunga bao kwa mchezo.

Wote wawili kila mmoja amefunga mabao zaidi ya 700 kwa kipindi chao cha uchezaji.

Wakati Ronaldo ni mwepesi zaidi wa kumalizia na kufunga bao, Messi anafunga na mara nyingine kutengeneza nafasi ya kufunga kwa mchezaji mwingine.

Ronaldo anafanya kazi kama mchungaji katika sanduku, akitumia fursa, wakati Messi mara kwa mara huangalia nani aliyepo kwenye nafasi nzuri ya kufunga na humtengeneza pasi nzuri. Ukweli ni kwamba staili ya Ronaldo ina msaada mkubwa wa kuhakikisha timu inapata mabao, tofauti na Messi.

#3. Uwezo wa mguu dhaifu

Hii ni moja ya tofauti kubwa kati ya Messi na Ronaldo. Mmoja hutegemea mguu wake wa kushoto ambao hauwezi kuzuiliwa kuvunja ulinzi wa upinzani, lakini mguu wake wa kulia hauna ubora huo.

Kwa mujibu wa takwimu, mshambuliaji huyo wa PSG anafunga mabao nane kati ya kumi kwa mguu wa kushoto, wakati anafunga bao moja tu kati ya nane kwa mguu wa kulia.

Ronaldo anafunga zaidi kwa mguu wa kulia, lakini ana uwezo mkubwa wa kufunga kwa mguu wa kushoto.
Kitakwimu raia huyo wa Ureno amefunga mabao 790 katika maisha yake ya soka, huku 145 akifunga kwa mguu wa kushoto.

#2. Uwezo angani

Ronaldo anatawala kabisa eneo hili. Kwa kweli Messi hana uwezo mkubwa kwenye eneo hili, huku urefu wake ukiwa ni mita 1.69, ikilinganishwa na mwenzake ambaye anasimama mita 1.87.

Kwa kuongezea, Mreno huyo ana uwezo mkubwa wa kuruka juu na kufunga mabao kwa kichwa.

Kwa takwimu, Messi amefu mais nga mabao 26 ya kichwa katika ha yake ya soka, wakati Ronaldo amefunga mara 137 kwa kichwa.

#1. Uchezaji kitimu

Linapokuja suala la kuchambua jinsi Messi na Ronaldo wanavyocheza kitimu, ni wazi kuna tofauti kubwa sana kati yao.

Raia huyo wa Argentina ni wazi kwamba ni mchezaji anayecheza sana kitimu na hupenda kuunganisha timu nzima.

Messi ni mtu anayeunganisha timu kuanzia nyuma hadi mbele. Anashuka chini kupanga uchezaji wa timu yake kabla ya kusonga mbele kubadilishana pasi na washambuliaji.

Ronaldo ni mchezaji wa kibinafsi anayeweza kusaidia timu kwa uwezo wake binafsi hata kama timu yake inacheza vibaya.

Tofauti na Messi, supastaa huyo wa Manchester United ana ushiriki mdogo katika kujenga uchezaji, kwani hutumia muda mwingi kuzunguka sanduku la upinzani.

Habari Kubwa