Tozoumiza miamala: Wabunge wavae uhusika unaotetea wapigakura wao

28Jul 2021
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Tozoumiza miamala: Wabunge wavae uhusika unaotetea wapigakura wao

MFUMO mpya wa tozo za miamala ya simu ulioanza kutozwa Julai 15, mwaka huu, ni matokeo ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2021/22 iliyopitishwa na wabunge kwenye bunge la bajeti mjini Dodoma mwezi uliopita.

Mabadiliko ya kisheria ya aina yoyote huanzia bungeni huku wawakilishi wakiwa tegemeo la wapigakura kuwa kile wanachokipitisha kinakuwa na tija na kulinda maslahi ya wananchi walio katika makundi na viwango mbalimbali.

Bunge limepitisha tozo hizo ambazo hadi kuwa sheria na kuanza kutumika zimelalamikiwa kupindukia na swali la kuwauliza wabunge hao linabakia kuwa walivaa uhusika wa mwananchi wa kawaida, hususan aliyepo kijijini wakati wanapitisha sheria hiyo? Au walitazama nini kwa vile tegemeo kubwa la Watanzania hao ni kupata huduma za kifedha kupitia simu za mkononi.

TISHIO KIBIASHARA

Tozo hizo ‘umiza’ , tayari zimetua kwenye Chama cha Waendesha Huduma ya Simu za Mkononi Tanzania (TAMNOA), wakitoa tathmini inayoonyesha kuwa huenda zikawa kitanzi kwa biashara za fedha kupitia simu za mkononi.

TAMNOA, imeanza wiki kwa kutoa tathmini ya athari zilizotokana na tozo za miamala kupanda, ikisema wateja zaidi ya 1,000,000 hususani walioko vijijini walisitisha kutumia huduma na kwamba miamala imepungua kwa asilimia 45.

Mwenyekiti wa TAMNOA, Hisham Hendi, ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa VODACOM, anasema kwamba Sheria ya Fedha ya mwaka 2021/22, iliyopitishwa bungeni ni namna mpya ya utozaji kodi katika kila muamala unaofanywa na mteja kwa njia ya simu za mkononi.

Hendi, anasema wateja walioko vijijini wamesitisha kutumia huduma za miamala ya simu, kutokana na ongezeko la makato, ambayo aliyataja kama tishio kwenye uhai wa biashara ya simu nchini.

Huduma za kifedha kwenye simu za mkononi, kutuma na kupokea zinakua, kwa mujibu wa Waziri wa Mawasiliano ya Teknolojia ya Habari Dk. Faustine Ndugulile, hadi Desemba mwaka jana kadi za simu milioni 51 zilikuwa zimesajiliwa na asilimia 48.6 kati ya hizo, zinafanya miamala mbalimbali.

Ripoti ya hali ya uchumi Tanzania ya Juni 2020 iliyotolewa na Benki ya Dunia (WB), inaonyesha asilimia 23.4 pekee ya wakazi wa mijini wana akaunti benki na asilimia 5.1 ya wanaoishi vijijini wana akaunti za benki, hivyo Watanzania wengi hujumuishwa kwenye huduma za kifedha kupitia simu za mkononi.

Kupanda kwa tozo katika kila muamala unaofanywa na wateja wa kampuni mbalimbali za simu, kumeibua mjadala miongoni mwa wananchi, huku wataalamu wa uchumi na viongozi wakilitolea suala hilo ufafanuzi na kuahidi kulifanyia kazi upya suala hilo.

Tozo hizo zinamtoza kila anayefanya muamala wa Sh. 100,000 zaidi ya Shilingi 6,000 kiwango hicho kinazidi kupanda kadri muamala wa fedha unavyoongezeka.

Kwa wananchi wa hali ya chini ambao hufanya miamala kila siku iwe kutuma au kupokea fedha na kulipia huduma za kijamii, wapo wanaofanya muamala mdogo kwa usiozidi Sh. 5,000 kwa mawakala, ili atekeleze majukumu yake, wote hao wameathirika na wameumia.

Mtaalamu wa masuala ya fedha kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) cha Dar es Salaam, Profesa Bill Kiwia, anadokeza kuwa ongezeko hilo la kodi ya tozo, litaleta athari za moja kwa moja kwa wananchi.

Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba, akiwasilisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 anasema jumla ya bajeti iliyotengwa ni Sh. trilioni 36.33, matumizi ya kawaida yatakuwa Sh. trilioni 23 huku ya maendeleo ikiwa Sh. trilioni 13.3.

Bajeti hiyo imepandisha takribani mara mbili gharama za muamala zilizokuwa zinatozwa awali hali inayolalamikiwa na sasa Dk. Nchemba, anaahidi tozo hizo zitaangaliwa ila amefafanua kuwa uwepo wake ni sheria ya bunge, ambayo yeye hawezi kuifuta na kitakachofanyika ni kupitiwa kwa kanuni na kuangalia utekelezaji wake.

Aidha, pendekezo la kutoza Sh. 10 hadi 200 kwa kila laini ya simu kulingana na uwezo wa kuongeza salio, ni mwiba na suala jingine ambalo linaigusa jamii.

MAMBO YA KUANGALIA

Wakati Waziri Nchemba anaongeza tozo za miamala ya simu , bunge hilo limetoa msamaha wa kodi kwa bia zinazozalishwa na shayiri ya Tanzania kutoka Shilingi 765 kwa lita hadi 620 kwa kipimo hicho.

Lakini, pia Waziri analitangazia bunge kupunguza kodi ya mabasi yanayoagizwa nje ya aina ya mwendokasi, kadhalika viwanda vya sabuni navyo vimepunguziwa kodi na michezo ya kubashiri au kamari zimepunguziwa kodi kutoka asilimia 25 mpaka 15.

Aidha, simu za janja aina ya vishikwambi , vimeondolewa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na pia vifungashio vya tumbaku vimefutiwa ushuru ili kuhamasisha viwanda vya kuchakata na kuzalisha sigara kwa wingi nchini.

Pengine katika orodha ya vitu vilivyopewa punguzo la kodi vingi vinahusisha masuala ya starehe kama pombe, sigara michezo ya kubashiri kununua simu janja za vishikwambi (ipad) na huenda ingefaa kodi zake ziwe juu zaidi badala ya msamaha.

Watanzania wanasubiri jopo la watalaamu wanaoangalia tozo za miamala kutoka Benki Kuu (BoT), Mamlaka ya Mwasiliano (TCRA), Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kuja na maelezo yatakayowaongezea amani badala ya machungu.

Serikali inashauriwa kuzifikia kampuni kubwa kama Netflix na Youtube zinatengeneza faida kwa kutoa huduma zao hapa nchini na wachumi wanashauri serikali kuzitoza kodi kampuni hizo na kwamba Kenya tayari inafanya hivyo.