TPA inavyoisuka Kigoma kuinua uchumi M/Makuu

05Jul 2019
Mary Geofrey
KIGOMA
Nipashe
TPA inavyoisuka Kigoma kuinua uchumi M/Makuu

WIKI iliyopita tulikuwa na makala inayoelezea utendaji kazi wa bandari za Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma ambayo ni kitovu cha biashara na uchumi wa mkoa huo tuendelee.

Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, ambayo ni sehemu ya Bandari Kuu ya Kigoma, Ajuaye Msese.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) katika mkoa wa Kigoma imepiga hatua za ukuzaji wa uchumi pamoja na kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inatekelezwa kwa lengo la kuongeza ufanisi wa sekta hiyo muhimu nchini.

Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, ambayo ni sehemu ya Bandari Kuu ya Kigoma, Ajuaye Msese, anabainisha miradi inayoendelea na kutekelezwa katika mwambao wa ziwa hilo kuwa ni mipango mikakati ya muda mrefu na muda mfupi ya TPA wakati akizungumza na waandishi wa habari, waliozuru mkoa huo kwa lengo la kujionea mafanikio ya TPA.

Anawaeleza wanahabari hao waliopata fursa ya kuzuru katika miradi hiyo kuwa, TPA katika mipango yake ya muda mrefu imepanga kufanya maboresho ya gati la mizigo na la abiria katika bandari ya Kigoma. Upembuzi yakinifu umefanyika na kukamilika katika gati la mizigo.

Anasema Shirika la Misaada la Japan (Jica), litaboresha gati la abiria na ghala la shehena ambapo ujenzi wake unatarajiwa kuanza mwezi huu.

Kuhusu bandari ya Katosho, Msese anasema TPA imechukua eneo lenye ukubwa wa hekta 68 kwa ajili ya ujenzi wa bandari kavu, itakayotumika kupunguza mlundikano wa shehena bandarini katika jitihada za kuimarisha miundombinu ya reli na barabara, kupunguza mlundikano bandarini Dar es Salaam na kusogeza huduma karibu na nchi majirani wanaowahudumia.

“Tunalenga nchi za Burundi na Kongo (DRC) kwa lengo la kuwezesha mizigo kuchukuliwa Kigoma badala ya safari kuanzia Dar es Salaam,”Msese anaeleza.

Anaongeza kuwa, ujenzi wa bandari hiyo unaenda sambamba na uendelezaji wa ukanda wa biashara wa Kigoma Special Economic Zone.

Msimamizi huyo wa bandari ya Kigoma anasema, pia wana mpango wa kujenga ukuta na walishafanya tathimini mwezi Aprili mwaka jana.

Anasema kwa sasa TPA imeanza na ujenzi wa ukuta na mkandarasi amepatikana na utajengwa kwa miezi tisa.

“Mkandarasi ameanza ujenzi huo kuanzia Machi 28, mwaka huu na mradi na amefikia asilimia 13 mpaka sasa,” anasema Msese.

Kadhalika anasema wana mradi wa ujenzi wa gati la Kagunga unaohusisha ujenzi wa gati lenyewe, jengo la kupumzikia abiria, ghala la kuhifadhi shehena , vyoo, ofisi na uzio.

Anasema mradi huo umetekelezwa kwa asilimia 100 na gharama yake ni zaidi ya Sh. bilioni 3.356.

Msese anasema mradi mwingine mkubwa ni ujenzi wa barabara ya kuunganisha bandari na soko la kimataifa ambao ujenzi wake unaendelea.

Anasema gharama za kazi hiyo ni Sh. milioni 553. 791, mradi ambao utachukua miezi sita hadi kukamilika kwake.

“Mkandarasi ameanza kazi ya ujenzi Mei Mosi mwaka huu na hadi sasa umetekelezwa kwa asilimia tano,” anasema.

Kiongozi huyo anasema pia wana mradi wa ujenzi wa soko la kimataifa unaotarajiwa kugharamia  Sh. milioni 190.

Anasema muda wa mradi huo ni miezi sita na mkandarasi alianza kazi Januari 31 mwaka huu na hadi sasa mradi huo umetekelezwa kwa asilimia 25.

Msese anasema mradi mwingine ni ujenzi wa gati la Sibwesa (Kakya) ambao pia unahusisha kujenga gati, ofisi, jengo la kupumzikia abiria, ghala la shehena

Anataja gharama ya mradi huo kuwa ni Sh. bilioni 3.452 na hadi sasa utekelezaji wake umefika asilimia 96 na unatarajia kukamilika mwezi huu.

“Kama ilivyo katika mradi wa ujenzi wa gati la Kagunga na mradi huu pia unahusisha ujenzi wa gati, ofisi, jengo la kupumzikia abiria, ghala mizigo na uzio kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa TPA katika bandari hii muhimu,” anasema Msese.

 Mradi mwingine wa TPA katika mwambao wa Ziwa Tanganyika ni ujenzi wa gati la Lagosa unaohusisha usanifu na ujenzi wa gati.

Msese anasema ujenzi huo unafanywa na kampuni mbili unagharimu Sh. bilioni 12. 459 na kazi ilianza Mei 17 mwaka huu na umeshafikia kiwango cha asilimia 25.

Kadhalika anasema kuna mradi wa ujenzi gati katika bandari ndogo za Kibirizi, Ujiji na ofisi ya mkuu wa bandari na gati la kibirizi, kwa gharama ya Sh. bilioni 32.525 na kazi ilianza Februari 28 mwaka huu ambapo ujenzi umefika asilimia 15.

Msese anasema pia wanatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa gati katika bandari ya Kabwe, barabara na maegesho ya magari katika bandari ya Kipili kazi inayogharamiwa na TPA.

Anasema huo unahusisha usanifu, ujenzi wa gati, jengo la kupumzikia abiria, jengo la mgahawa, ofisi, ghala la kuhifadhia mizigo, nyumba za wafanyakazi na uzio.

Anataja gharama ya mradi huo ni Sh. bilioni 7.498 na mradi huo ni wa miaka miwili ambapo kazi ya ujenzi ilianza Aprili Mosi mwaka hana na umefika asilimia 40.

Msese anasema mradi mwingine ni wa ujenzi wa bandari ya Kasanga uliotiwa saini Aprili 15 mwaka huu.

“Mradi huu unahusisha upanuzi wa gati kutoka mita 20 za sasa na kufikia urefu wa mita 120 ambalo litakuwa na uwezo wa kuhudumia meli mbili kwa wakati mmoja,” anaeleza Msese.

Anasema gharama za mradi huo Sh. bilioni 4.764 na mkandarasi alikabidhiwa eneo la mradi Aprili 28 mwaka huu.

Msese anasema pia wana mradi wa ujenzi wa bandari ya Karema ambao umehusisha ujenzi wa gati, majengo, njia za reli na ‘wind breakers’ ndani ya bandari kwa gharama ya Sh. bilioni 63.

MIKAKATI

Msese anasema mbali na utekelezaji wa miradi hiyo katika mwambao wa Ziwa Tanganyika wana changamoto ambazo wameziwekea mikakati ya kuzitatua ili kuboresha usafiri katika bandari zote.

Anasema kuna changamoto ya kupungua kwa shehena inayoenda nchi jirani za Kidemokrasi ya Kongo (DRC) na Burundi.

Anaeleza mkakati walioweka wa kukabiliana na tatizo hilo ni kutafuta masoko mapya na kuvutia yalipo.

Pia anasema wanakabiliana na changamoto ya ufanisi mdogo wa Kampuni ya Reli (TRC) na kwamba wapo katika mazungumzo ya pamoja kati ya Bandari ya Kigoma na TRC.

“Lengo la kuwapo kwa mazungumzo haya ya pamoja ni kuweza kuboresha miundombinu ya reli kwa nia ya kuboresha huduma ya usafirishaji,” anasema Msese.

Anaeleza pia uwapo wa bandari bubu ambao wameweka mikakati ya kuzichambua ili zirasimishwe na kufunga zile ambazo hazipo kwa mujibu wa sheria.

“Tukifunga hizi bubu zile zilizopo zifanye kazi kulingana na kanuni na taratibu za kiesheria na hivyo kuimarisha ulinzi na usalama kwenye mipaka ya nchi na kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato.

YATENGA BILIONI 500

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TPA, Deusdedit Kakoko, anasema kwa mwaka mamlaka hiyo inatenga Sh. bilioni 400 hadi 500 kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo ya maendeleo.

Anasema wanatumia fedha za TPA kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo ikiwamo ya ujenzi wa gati za kisasa, upanuzi wa bandari zote nchini, ujenzi wa ofisi na maghala ya kuhifadhia mizigo ili kufungua milango ya kibiashara na nchi za jirani.

Anasema miradi hiyo inatumia zaidi ya Sh. bilioni 500 ya fedha za ndani na hufika hadi Sh. bilioni 600 kama wakipata na fedha za  nje.

Kakoko anasema kati ya fedha hizo ambazo zinatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ya TPA asilimia 30 ya fedha hizo wanalipa mrahaba serikalini.

“Kukamilika kwa miradi yote ya kimkakati ya TPA kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza mapato yatokanayo na shughuli za bandari mara dufu," anasema Kakoko.

Habari Kubwa