Tuilinde amani kuelekea uchaguzi mkuu 2020

06Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Tuilinde amani kuelekea uchaguzi mkuu 2020

TANZANIA ikiitwa Tanganyika ilipata uhuru Desemba 9 mwaka 1961 kabla ya kuungana na Zanzibar mwaka 1964 na kuwa Tanzani

Na Magambo Masambu

Historia inaonyesha kwamba kabla na baada ya Uhuru, Tanzania imeongoza harakati za ukombozi barani Afrika na hasa nchi zilizoko Kusini mwa Afrika kuhakikisha zinapata uhuru wa nchi zao, amani pamoja na maendeleo ya kiuchumi.

Wanapotajwa viongozi mashuhuri katika harakati hizo hatuwezi kukwepa kulitaja jina la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama muasisi wa harakati hizo, kuhakikisha waafrika wanajitawala.

Kwahiyo Mwalimu pamoja na viongozi wenzake wa Afrika wakahakikisha mapambano yatatulia tu pindi nchi karibu zote za Afrika zitakapokuwa huru na ikawa hivyo.

Tanzania kwa miongo kadhaa sasa imetambulika kama kisiwa cha amani. Inapotajwa mahali popote duniani picha ya kwanza ni amani yetu, taifa la watu waungwana, wenye utu, wenye kujali haki za wengine na utambulisho mkubwa ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hata kama watu hawaifahamu nchi sawasawa unapomtaja yeye fikra zinakwenda kwenye harakati za ukombozi.

Sifa hii ya amani ambayo imekuwa ikitutambulisha kila mahali tunapaswa kuilinda kama msingi mkuu wa umoja wetu. Waswahili wanasema “Ukiona vyaelea ujuwe vimeundwa”.

Maana yake ni kwamba chochote kinachoonekana kina chanzo chake. Amani tuliyonayo kama taifa haikutokea tu tukawa nayo kazi na juhudi kubwa zimefanywa na viongozi wetu waliyotangulia, si jambo dogo kwa nchi kama yetu hii yenye makabila zaidi ya 120, kuwa pamoja, kuzungumza lugha moja kama Watanzania.

Nchi ambayo ina dini na madhehebu mbalimbali na kuheshimiana kwa misingi yetu ya imani, si jambo la kawaida sana kwani tumeona katika nchi nyingine wakitofautiana.

Wapo wanaofikiri kwamba sisi tumependelewa sana na Mwenyezi Mungu, lakini ukweli ni kwamba tulitangulia kupata viongozi wenye busara na hekima ambao walituweka pamoja kama taifa moja, tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia viongozi wa aina hiyo.

Kama amani hujengwa pia hubomolewa na watu na chenye kujengwa ili kiwe imara sharti kiwe kina msingi imara na msingi wa amani mahali popote huwa ni “Haki” haki ikitawala amani hutamalaki, haki inapovunjwa kuna uwezekano mkubwa pia wa amani kuvunjika.

Kuelekea uchaguzi mkuu 2020, kila mtu ndani ya nchi hii anawajibu wa kuhakikisha amani inakuwa zaidi ya uchaguzi wenyewe, kwani kuna maisha baada ya uchaguzi kwa vyovyote vile maisha lazima yaendelee.

Wanasiasa (wagombea) na wananchi (wapiga kura) matendo yetu katika kipindi hiki cha kampeni tunayoyasema na kuyatenda lazima yawe ni ya kujenga umoja wetu zaidi kuliko kutukosanisha, amani ikivunjika huvunjika kwa kila mtu na hakuna atakayebaki salama ni muhimu kuhakikisha amani yetu inakuwa kipaumbele katika matendo yetu sio maneno tu.

Wapo watu wanaodhani kwamba siasa haiwahusu kabisa na hawataki kusikia habari ya siasa, lakini ukweli ni kwamba siasa ni mfumo wa maisha haitamhusu marehemu tu, lakini tukiwa bado hai siasa inatuhusu kwasababu ndiyo mfumo unaotupatia viongozi wa serikali, hao ndiyo huamua namna gani ya kuendesha maisha yetu katika uchumi, elimu, biashara, kilimo, uvuvi, na mambo mengine yote, lakini pamoja na ukweli huu haimaanishi kila mtu ndani ya nchi hii ni mwanasiasa.

Nafikiri wanasiasa hasa ni hawa wanaotafuta ajira majukwaani hivyo basi ni muhimu kutambua kwamba ajira hizi zisiathiri shughuli za wengine ambao wanajiona si wanasiasa japo siasa inawahusu, maana yangu ni kwamba mnaoomba ajira za siasa hubirini amani zaidi kwenye vinywa vyenu kuliko chuki na matusi.

Kwa upande mwingine ni wale wenye mamlaka ya kutoa haki, kama unajiona upo kwenye upande huu basi ni muhimu kuhakikisha kwamba haki mahali popote inatendeka na sio kutendekana tu bali ionekane kwasababu amani ni matokeo ya haki, usawa na ukweli tunaweza kuhubiri sana lakini tukishindwa kutenda mahubiri yetu yanaweza kuwa yananyakuliwa na ndege wa angani.

Sisi ni ndugu, tumeoleana tena bila kujali makabila yetu, rangi zetu wala imani zetu za dini, hatuna sababu yoyote ya kudhalilishana, kutukanana, kutwezana kwani baada ya uchaguzi Oktoba 28, 2020 inaweza kuwa ni aibu hata kutazamana. Madaraka ya kisiasa yasitufanye tuvuane nguo majukwaani hayo si mambo ambayo wananchi wanatarajia kusikia kutoka kwa wagombea.

Wananchi wa Tanzania wanataka kusikia hatima yao ya leo, kesho na keshokutwa, wanataka kusikia sera nzuri zinazotokana na ilani za vyama vyao vya siasa hawahitaji kusikia mambo ambayo yatawajengea chuki na kuhatarisha amani yao.

“Now that you got what you wanted; you don’t even know my name. Haya yamesemwa na mwana mziki nguli wa rege kutoka Afrika ya kusini Luck dube katika wimbo wake unaoitwa The Way It Is (jinsi ilivyo) kwa tafasiri isiyo rasmi sana anasema

“Kwakuwa umepata kile ulichokitaka, hata jina langu hulijui tena”. Katika vipindi hivi vya uchaguzi watu wengi sana hasa vijana hutumiwa kufanya uhalifu na maovu mengi ili kuhakikisha tu kwamba wale wanaowatuma wanapata madaraka.

Tunahitaji sote tupendane na tuwe wamoja, hatuna nchi nyingine bali ni Tanzania zaidi tuendelee kuilinda heshima ya nchi hii, majirani zetu wanatutazama tu kwasababu sisi mara zote tumekuwa walimu wao na wasuluhishi wao katika migogoro ya kisiasa, litakuwa jambo la aibu na fedheha kwa mwalimu kufanya mambo anayofanya mwanafunzi.

Amani ya Tanzania ni amani ya majirani zetu pia, utulivu wa Tanzania ni utulivu wa bara la Afrika, upendo wetu ni upendo wao pia hivyo lazima tukumbuke kwamba tunatazamwa kila mahali.

Mungu ibariki Tanzania, ibariki Afrika na ulimwengu kwa ujumla.

0689157789
[email protected]

Habari Kubwa