Tujifunze darasa la haki kodi kutoka kwa wanaoisimamia

12Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Tujifunze darasa la haki kodi kutoka kwa wanaoisimamia

PROF. Mussa Assad, ana siku chache tangu aanze maisha ya ustaafu, akitoka kwenye wadhifu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Kabla ya hapo, alishika chaki kwa wanaosaka digirii mbalimbali za taaluma ya uhasibu au zenye somo hilo, alitafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu.

Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere (kulia), alipozungumza na walipa kodi katika banda la TRA katika Maonyesho ya 42 Biashara Kimataifa maarufu Sabasaba, jijini Dar es Salaam. Kwa sasa Kichere, ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akichukua nafasi ya Mussa Asaad. PICHA: MTANDAO.

Na Niko Kasera

Hili la mwisho alilostaafu nalo lilikuwa na unyeti wa kipekee kitaifa, kwani ni jukumu lenye dhamana ya kukagua na kusimamia rasilimali za kitaifa.

Alipokuwa amebakiza miezi mitatu ofisini mnamo Agosti 11, kwenye semina jijini Dodoma, Profesa Assad alipata fursa ya kutoa neno ndani ya mkusanyiko huo wa kitaaluma.

Hapo alitoa darasa kwa kutumia mfano uliowagusa wengi miongoni mwa waliohudhuria, hasa pale aliposema kwamba pamoja na kodi kuwa wajibu, ni muhimu kwa serikali yeyote kuwaonyesha walipa kodi kwamba kodi zao zinatumika kuboresha hali yao ya maisha.

Alieleza: “Chukua mfano wa eneo la makazi la Sinza Dar es Salaam. Ikiwa wakazi wa Sinza wataona wazi kwamba mitaa ya mle mle yanajengewa lami na huduma za upatikanaji maji inaboreshwa, itakuwa rahisi kupata walipa kodi wengi zaidi kujitokeza.”

Tafsiri aliyoiotoa Profesa Assad, inaangukia katika kilekile ambacho Rais Dk. John Magufuli, ameisisitiza mara nyingi, akihimza ulipaji kodi hata akatoa darasa kwa wanunuzi kwa kuwasisitiza kudai risiti, lengo kubwa ni kuhitimishiwa malipo ya kodi.

Anasema, kutokana na malipo ya kodi yakiwa vizuri, inaisaidia serikali kuwa na uwezo kuhitimisha majukumu yake na hasa ya kimaendeleo, ikitumia fedha zake za ndani.

Hapo anainisha miradi ujenzi wa reli ya kisasa, ununuzi wa ndege mpya zaidi ya 10 kwa ajili ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kutumia fedha za ndani, ikimaanisha makusanyo ya kodi na vyanzo mbalimbali.

Ni dhahiri ulipaji kodi wa hiari ni msingi muhimu kwenye dhana ya uwajibikaji wa mwananachi kila mmoja kwa nafasi yake. Kadri tunapoendelea kupanua wigo wa idadi ya walipa kodi, ndivyo kiasi kinachokusanywa kitaongezeka, hivyo kuiwezesha serikali kutimiza ndoto yake ya maendeleo kwa jamii.

Prof. Assad katika kauli yake amehimiza dhana hiyo kwamba ili jamii kuhoji matumizi ya serikali kuu na serikali za mtaa, ni vyema sote tuwe walipaji kodi wa hiari na sio kwa shuruti au kuwajibishwa.

Uwajibikaji ni msumeno wa haki, unaojikita pande zote. Ni wajibu Watanzania wakalipa kodi na hilo wala halina ubishi. Miaka 50 ijayo, vizazi vinavyozaliwa leo vikiwa watu wazima, watakuwa na cha kuhadithia namna babu zao walivyothubutu, wakajenga reli za kisasa.

Wakati huohuo, miradi ya serikali kuu na serikali za mitaa sharti zionyeshe kwamba sio tu fedha zimetumika, bali zimetumika kukidhi viwango vya ubora na kuridhisha.

Mifano ni mingi ambayo kwa kazi za ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa vipindi tofauti, namna anavyoibua kwa miaka nenda rudi kuhusiana na baadhi ya miradi kutotendewa haki, mathalan ujenzi usokidhidhi viwango, kutokamilika kwa wakati au upotevu wa fedha za miradi.

Huku tukiadhimisha miaka minne ya Rais Dk. Magufuli kuwa madarakani, daima tusiwe mbali na hotuba zake zenye maelekezo, pia kukemea mabaya mbalimbali kwa taifa, hapo tukigusa rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na watendaji na Watanzania kwa ujumla.

Iwapo tuna nia ya dhati kuandamanana kufikia dira ya taifa kuisaka uchumi wa kati, hatuna budi kuhakikisha tunawatumia vyema wataalamu wabobezi tulionao ambao nao ni muhimu wakawa waumini wa kulitakia mema taifa. Naamini sote tutafika.

•Kwamaoni na ushauri wasiliana kupitia: [email protected]

Habari Kubwa