Tukatae ndoa za utotoni kwa kauli thabiti

21Feb 2016
Dar
Nipashe Jumapili
Tukatae ndoa za utotoni kwa kauli thabiti

NDOA ni taasisi ambayo wahusika wake nawafananisha na viongozi wa serikali, kwa maana ya rais wa nchi ni baba na mama ni Waziri Mkuu ambaye ndiye mtendaji mkuu wa shughuli zote za nyumbani katika kumsaidia baba.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

Ili taasisi hii iwe nzuri na kusonga mbele vizuri, kwanza kabisa hutegemea uongozi wa baba na zaidi sana utendaji wa mama ambaye ndiye kiongozi wa shughuli za ndani za kila siku ikiwamo kuhakikisha watoto wamepata huduma muhimu na malezi thabiti.

Kwa umuhimu wake ni lazima rais na Waziri Mkuu wawe watu makini, wenye ukomavu wa akili, busara na hekima ya hali ya juu katika kutatua mambo mbalimbali yanayojitokeza na hasa suala zima la kuwa na watoto na malezi yao kwa ujumla.

Nimeanza kwa kufananisha ndoa na viongozi hao ambao kwa namna moja au nyingine wanategemeana sana katika utekelezaji wa majukumu yao, kwa lengo la kuzungumzia tatazo kubwa la ndoa za utotoni kwenye jamii yetu.

Bado kuna mkanganyiko wa sheria na Katiba kwa kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa umri wa mtoto wa kike anayeweza kuolewa ni chini ya miaka 18 huku Katiba ikitaja umri wa mtu mzima ni kuanzi miaka 18, hivyo kuleta mkanganyiko kwamba msichana aliyeolewa chini ya miaka 18 anahesabika ni mtoto au mtu mzima?

Mkanganyiko huo nao ni kichocheo kikubwa cha ndoa za utotoni ambazo hufanyika kwa ridhaa ya wazazi au walezi na si muhusika, na lengo kubwa huwa ni wazazi kujipatia mali kwa haraka.

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), kwa kushirikiana na Ubalozi wa Canada nchini kupitia shirika lisilo la kiserikali la Internews Tanzania, wanaendesha kampeni ya kupinga ndoa za utotoni katika kumsaidia mtoto wa kike kupata elimu badala ya kutumika kama kitega uchumi cha ukoo au familia.

Takwimu zinaonyeshaa kuwa asilimia 28 ya watoto wako katika ndoa za utotoni nchini na kuifanya taswira ya Tanzania kuchafuka katika eneo hilo kwa kuwa watoto hawa walipaswa kuwa shuleni.

Aidha, kwa mujibu wa takwimu za Unesco, mkoa wa Shinyanga unaongoza kwa silimia 59 ukifuatiwa na mikoa ya Tabora (58), Mara (55), Dodoma (51), Lindi (48), Mbeya (45), Morogoro (42) na Singida (42).

Wengi wa mabinti hawa ni wale ambao baadhi wamefaulu kuendelea na masomo ya sekondari lakini kwa kisingizio cha kukosa ada, wakaishia kuozwa na wengine walikatishwa masomo baada ya kubainika wamevunja ungo na kukabidhiwa kwa waume zao kuanza majukumu ya familia.

Baadhi ya wazazi huwashawishi watoto wao kufanya vibaya mitihani ya darasa la saba kwa eneo ambalo serikali imeingilia kati na kuwalazimisha kusoma, ili wasifahulu na kuwa tiketi ya kuolewa.

Kama nilivyoeleza awali taasisi ya ndoa mtendaji mkuu ni mama, sasa tujiulize mama wa umri wa miaka 12-17 ana uwezo gani wa kukabiliana na changamoto za familia, kuzaa watoto wakati mwili wake haujapanuka vya kutosha na mbaya zaidi wengine huozeshwa kabla ya kuvunja ungo.

Binti huyu bado hajajitambua vizuri alihitaji kuwa chini ya uangalizi wa wazazi au walezi wake, kusoma vizuri ili aweze kusaidia familia yake kimawazo na sasa ameshakuwa mama kwa hiyo kinachoendelezwa ni kuunda familia ambazo zitakuwa na watoto walioshindwa kulelewa vizuri.

Binti huyu naye hataona umuhimu wa elimu kwa kuwa akili yake ilidumazwa na wazazi au walezi wake kuwa yeye si wa kusoma, ili aisaidie jamii yake au awe kiongozi katika mamlaka fulani bali aliandaliwa kama nguvu kazi ya familia na kiwanda cha kutotoa watoto ambao nao ni nguvu kazi.

Kwa jamii za kifugaji asilimia kubwa ya watoto wa kike hawasomi kwa kuwa inaaminika kumsomesha mtoto wa kike ni kupoteza muda na mali kwa kuwa mwisho wa siku atakwenda kuwa mke wa mtu, huku jamii za waswahili wao huozesha binti baada ya kuvunja ungo na kuchezwa kwa kuwa inaaminika mwanamke siku zote ni wa kumfurahisha mwanamume tu.

Haya yote ni kikwazo kikubwa katika kufikia malengo endelevu ya kumkomboa mtoto wa kike, ni lazima ushiriki wa jamii uwe mkubwa kwa kuwa yote yanatendeka ndani ya jamii zetu na yanaonekana kwa kuwa wanandugu, majirani na rafiki hushiriki katika ngoma na sherehe za kuozesha binti ambaye wamemuona tangu anazaliwa na kukua.

Hivyo ni lazima jamii ishiriki kusema hapana kama ambavyo Canada na Tamwa imeona tatizo hili na kuingia vijijini kupinga kwa vitendo.

Aidha, tupige kelele serikali ikubali kufanya marekebisho ya sheria ya ndoa katika kuondoa utata uliopo baina ya sheria na Katiba ambayo ndiyo sheria mama, tujue msichana anaweza kuolewa katika umri gani, na mila zilizopitwa na wakati kuwa mtoto wa kike hastahili elimu pia tuzikatae kivitendo.

Mungu ibariki Tanzania
Mungu ibariki Afrika
Kwa mawasiliano: [email protected]

Habari Kubwa