Tume Huru ya Uchaguzi, Sasa imetimia miaka 28 kulilia mabadiliko

25Mar 2020
Gaudensia Mngumi
Dar es Salaam
Nipashe
Tume Huru ya Uchaguzi, Sasa imetimia miaka 28 kulilia mabadiliko

SUALA la Tanzania kuwa na tume huru ya uchaguzi ni jambo ambalo limekuwa kwenye majukwaa ya wadau wa siasa takribani miongo mitatu sasa.

Jaji Joseph Warioba, Tume yake iliainisha namna ya kupata tume huru ya uchaguzi. PICHA: MTANDAO.

Madai ya tume hiyo yalianza tangu mwaka 1992 wakati mfumo wa vyama vingi ulipoanza kutumiwa nchini kwani ilionekana kuwa ni lazima kuwa na chombo huru kinachosimamia mchakato katika mazingira ya mitizamo tofauti ya kiitikadi.

Wadau wanaotaka kuwe na tume hiyo ni pamoja na vyama vya siasa, taasisi za kidemokrasia, wadau wa maendeleo wakiwamo wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU), Umoja wa Afrika (AU) , asasi za kirai na taasisi mbalimbali zinazohimiza masuala ya kidemokrasia.

Hata sasa, taifa linapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, vyama vya upinzani vinaendeleza dai hilo na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ameanza kuiibua tena haja ya kuwa na tume ya huru ya uchaguzi.

Mapema February 6, 2020 akiwa bungeni jijini Dodoma, Mbowe Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, anamuuliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, swali la papo kwa papo ni lini Tanzania itakuwa na tume huru ya uchaguzi?

Akijibu, Waziri Mkuu anasema tume iliyoko leo ni huru na hata kikatiba tume hiyo iko huru, hivyo itaendelea na kazi zake.

Wiki hii, watendaji na viongozi wa vyama vya siasa pamoja na Tume ya Uchaguzi (NEC) wameibua tena hoja ya tume huru, wakiitaka NEC ithibitishe kwa matendo, tamko la Rais John Magufuli, kuwa uchaguzi wa 2020 utakuwa huru na haki.

Pamoja na Rais kutoa ahadi hiyo kwenye kuukaribisha mwaka mpya wa 2020, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Profesa Palamagamba Kabudi, akiwa Uswisi, aliiahidi jumuiya ya kimataifa kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa haki na uhuru.

KUTAKA MABADILIKO

Pamoja na wapinzani hasa Mbowe kuzungumzia suala la tume hiyo zama hizi, ni wazi historia ya mabadiliko ya kutaka kuwa na tume huru hayajaanza leo wala si madai ya Chadema, hata Kamati ya Jaji Robert Kisanga ya mwaka 1998, ilipokusanya maoni ya wananchi kuhusu masuala ya katiba, ilitaka kuundwa kwa chombo huru cha kusimamia uchaguzi.

Hata hivyo, rais wa wakati huo , Benjamin Mkapa, hakutekeleza mapendekezo ya Kamati ya Kisanga na mambo yakabaki kama yalivyo.

TUME YA WARIOBA

Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, iliyofanyakazi mwaka 2013, ilipendekeza kuwa na tume huru ya uchaguzi na ikaanisha mchakato wa namna ya kuipata.

Ibara ya 190 ya rasimu ya Warioba inaainisha namna ya kuundwa tume huru ya uchaguzi ikionyesha taratibu za kuwapata wajumbe kwa uwazi kupitia utaratibu wa kuomba nafasi hizo na pia kuchujwa na Kamati ya Uteuzi kabla ya kuteuliwa rasmi na rais kuwa mwenyekiti makamu, au makamishna wa tume hiyo.

Aidha, kupitia Rasimu ya Warioba, wananchi wanatoa maoni ya muundo wa tume wakitaka mwenyekiti, makamu wake na makamishna au wajumbe wa tume hiyo wathibitishwe na bunge.

Aidha, rasimu hiyo inapendekeza kuwa pengine si jambo jema mbunge, wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, au la Tanzania au mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuteuliwa kuwa mjumbe wa tume huru.

Aidha, ibara ya 191 ya rasimu hiyo inawataja wajumbe wa kamati ya uteuzi ambao ni pamoja na Majaji wakuu wa Tanzania na Zanzibar, Maspika Bunge na Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Halikadhalika, ibara ya 194 inaeleza kuhusu namna ya kushughulikia kesi za uchaguzi na kupendekeza zifunguliwe Mahakama Kuu mapema iwezekanavyo baada ya tume huru ya uchaguzi kutangaza matokeo.

Aidha, ibara ya 195 inapendekeza namna ya kumteua Mkurugenzi wa Uchaguzi, ambaye atateuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Umma na kuthibitishwa na Bunge. Pia, inaweka vigezo na sifa za kuwa mkurugenzi wa uchaguzi.

Hata hivyo, rasimu ya katiba ya Warioba, haikukubaliwa na mchakato wa kupata katiba mpya haukukamilika hadi sasa na suala hilo likabakia kama lilivyo.

TUME HURU NININI?

Ibara ya 74(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo inayounda tume ya sasa na inatamka kuwa kutakuwa na tume ya uchaguzi na wajumbe wake watateuliwa na Rais, ambao ni pamoja na Mwenyekiti , Makamu na wajumbe wengine, lakini pia hata Mkurugenzi wa Uchaguzi anateuliwa na Ikulu.

Hilo ndilo wapinzani, wadau wa uchaguzi wakiwamo wapiga kura wanalolilalamikia wakisisitiza kuwa kuna haja ya mabadiliko na kwa ujumla kinacholalamikiwa kuhusu tume hiyo inayozungumzwa tangu mwaka 1992 hadi leo ni namna ya kupata wajumbe wa tume hiyo.

Kinachogomba kwa mujibu wa Mbowe na wadau wengine wa siasa ni namna ya kuwapata wajumbe wa tume hiyo, ambayo imeanishwa kwenye ibara ya 74 (1).

Wapinzani wanachokisimamia ni kutaka kuwe na utaratibu mwingine wa kuwapata wajumbe wa tume ya uchaguzi tofauti na huu wa sasa ambao, wote huteuliwa na Ikulu.

KUPINGA MATOKEO

Suala ambalo linazungumzwa na wadau wa siasa na wapinzani mara kwa mara ni pamoja na kutaka matokeo ya uchaguzi wa urais yapingwe mahakamani.

Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi na katiba ya Tanzania, matokeo ya urais yakishatangazwa na tume hayaruhusiwi kuhojiwa au kupingwa mahakamani kwa namna yoyote ile.

Lakini, kwa upande wa vyama vya upinzani vinasisitiza kuwa hakuna sababu ya kukataza matokeo hayo kupingwa mahakamani kwani yote hiyo ni michakato ya kidemokrasia.

Upinzani unaamini kuwa ni haki ya wapiga kura, wagombea wa urais kueleza malalamiko yao na kusema yale wanayodhani ni kasoro kwenye uchaguzi huo kwa vile yote hiyo ni michakato ya kidemokrasia.

UMUHIMU

Kwa mtizamo mwingine uchaguzi ni mchakato ambao una wadau wengi kuanzia, wapiga kura, wagombea, vyama vya siasa wapinzani na kinachotawala , taasisi za kidemokrasia, waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, jumuiya za kikanda na mataifa wahisani.

Iwapo wadau wengi wanataka kuwe na chombo hicho au tume huru pengine wanaona kuwa mchakato hauwafurahishi na wanafikiria kuwa tume iliyopo inatakiwa kuboreshwa zaidi hivyo pengine suala hilo linahitaji kujadiliwa.

Ni vyema kusikilizana na kufanya uamuzi kwani ni kilio cha miaka 30 sasa.

TAKWA LA AFRIKA

Baadhi ya masuala yanayotajwa kwenye mtangamano wa Afrika (AU) ni umuhimu wa kuzingatia demokrasia, utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu.

AU ina Mkataba wa Afrika wa Demokrasia, Uchaguzi na Utawala Bora (ACDEG) na suala la kuwa na tume huru za uchaguzi kwa wanachama wa AU linasisitizwa.

Sura ya Saba ya ACDEG, inawaagiza wanachama wa Umoja wa Afrika kuwa na tume huru na vyombo huru vya kusimamia uchaguzi.

Aidha, inaeleza kuwa vyama vya siasa viwe na wajibu wa kukubali matokeo au pale vinapoona mambo hayajakaa sawa vinaweza kuyakataa matokeo ya uchaguzi kwa kutumia taratibu na sheria zilizopo. Inataka yafikishwe mahakamani na kuhojiwa.

Kwa hiyo ni wazi kuwa dai la kuwa na tume huru ni kilio cha wadau wengi na si kwamba ni jambo linaloibuka sasa wakati taifa likielekea kwenye uchaguzi huo.

VIPI MUDA?

Wakati huu suala hili huchagizwa na upinzani hasa Chadema kwa kutaka umuhimu wa kipekee wa tume hiyo kabla ya Oktoba 2020 kwenye uchaguzi mkuu.

Kinachojiri ni je, muda unatosha kwa uchaguzi wa 2020, ikiwa imebakia miezi sita mchakato huo unaweza kufanyika? Na kwa vile hitaji la msingi la kisheria ni kufanya marekebisho ya katiba ili kuwa na tume hiyo ambayo msingi wake ni katiba itawezekana?.

Kwa vile kila mmoja anaona uchaguzi umekaribia pengine ni wakati wa wadau wa uchaguzi kuanzia vyama vya siasa, serikali,
chama tawala , bunge, baraza la wawakilishi na mihimili mingine ukiwamo wa sheria kukaa na kukubaliana kuhusu kusogeza mbele uchaguzi na kuboresha muundo wa tume au kueleza michakato mingine.

Ni jukumu la wadau hao kueleza iwapo wanaona umuhimu wa kusogeza mbele uchaguzi huo ili kuandaa muswada wa sharia wa kurekebisha katiba na kuuwasilisha bungeni na kwenye baraza la wawakilishi pengine kwa hati ya dharura ili kuandaa sharia ya kurekebisha katiba hiyo itakayosainiwa na Rais ili iwe sheria na mchakato uanzishwe.

Pengine ni vyema kujadiliana na kuona lipi linawezekana kwa wakati huu, kuliko kwenda kwenye uchaguzi huku baadhi ya wadau wakinung’unika na kutaka kuwe na mabadiliko ya tume ambacho ndicho chombo kinachosimamia uchaguzi huo.

Hata hivyo, hilo ni suala ambalo linawahusu wadau wote pamoja na baadhi ya wananchi wanaoona kuna umuhimu wa kuwa na marekebisho au viraka kwenye katiba ili kufanya marekebisho kwenye tume hiyo.

Je wadau hawaoni kuwa ni muda wa kushauriana na kutoa maelezo ya kilio hicho katika kusaka maridhiano na kujenga umoja na uvumilivu wa kisiasa na kitaifa?

Habari Kubwa