Tumekwama maji, sakata linaloitesa vita vya moto tangu miaka ya 1970

22Jul 2021
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Tumekwama maji, sakata linaloitesa vita vya moto tangu miaka ya 1970

MOJA ya maeneo yanayoleta utatanishi katika kupima mifumo ya utendaji au usimamizi wa sekta tofauti serikalini ni uwezo mdogo wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini.

Gari la Zimamoto kwa ajili ya kuhudumia ofisi mpya, Kahama.

Ni chombo kilichobeba hadhi hiyo kuwa jeshi mwaka 1985, Bunge lilipopitisha sheria iliyoanzisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, hata kuifanya huduma hiyo itolewe katika nidhamu ya kijeshi, chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Pia, miaka 22 baadaye 2007, kulipitishwa sheria ya inayoboresha huduma za Zimamoto na Uokoaji nchini, iliyoviweka vikosi vya Zimamoto na Uokoaji chini ya kamandi moja, hata shughuli hiyo ikawa na sura ya kujitegemea zaidi kujiendesha.

Ndani ya mtazamo huo hadi sasa kuna uhalisia unaobaki kwamba huduma za Zimamoto na Ukoaji, ikilinganishwa na ndugu zao kama vile Polisi na Magereza, haijafikia kiwango cha mtu kulingana nao, hasa katika maeneo mawili kunakopigiwa kelele zaidi.

Kwanza siyo rahisi kufika eneo la ajali kwa wakati, kwa maana ya kuwa na gari lililosheni maji, likikimbizwa kwa gari lenye king’ora kuelekea kwenye tukio; pili uwezo wa kumaliza moto kwa nyenzo ilizoleta.

Kwanini hoja hiyo? Ni namna wanavyokwama katika tukio la kuzima moto kama sokoni Kariakoo, hoja inayodumu ‘uhaba wa maji.’

SIMULIZI YA 1970

Ipo picha ya marejeo zama za miaka ya 1970, iliposhuhudiwa mkasa kuungua ghala la katani katika Barabara ya Pugu (sasa Nyerere), jijini Dar es Salaam, katika eneo la viwanda vikubwa, nako kulijitokeza hoja ya kukosekana chanzo cha maji ya kutosha.

Vivyo hivyo, kuna sura ya pili iliyoacha swali, pakijulikana viwanda haviendeshwi kwa maji ya bomba ya kuchota na ndoo, bali mifumo mikubwa ya maji ya tanki katika maeneo yao.

Kiwanda hicho kiliungua kwa muda mrefu huku Zimamoto wakitafutila chanzo cha maji. Inaelekea walienda Uwanja wa Ndege ( sasa Julius Nyerere) walikopata maji.

Ujumla wake unaagukia, hadi sasa hakuna rekodi za kujitosheleza ni namna gani wahusika kwa Zimamoto na Uokoaji, wanavyokwama.

Hapo mkasa wa kilichoikuta ghala la Kiwanda cha Katani kuungua mwaka 1975, kwa maana ya miaka 46 baadaye kupitia picha ileile, kinashuhudiwa sokoni Kariakoo hakuna chanzo cha maji cha uhakika.

MWELEKEO NI UPI?

Utaalamu katika eneo hilo, maendeleo katika miundombinu ya maji na kudhibiti moto yanahitaji ufanisi, ikiwamo katika makao makuu ya Idara ya Zimamoto na ofisi zake zingine katika mtazamo wa kelele zinazojirudia: “haja ya kuwa na vyanzo vya maji karibu na tukio la moto.”

Linabaki kuwa jambo la kawaida, hata halisikiki likijadiliwa, kwa maana ya kukumbusha umuhimu na siyo kudadisi walakini uliopo.

Kuna maelezo ya Ofisa wa Zimamoto redioni kuhusu moto hivi karibuni Kariakoo, ni kasoro katika ujazo wa gari la kuzima moto na haja ya kuwa na vyanzo jirani.

MAHALI INAKONASA

Uhalisi uliopo ni kwamba, inachukua wastani dakika tatu kujaza ndoo au ‘dumu’ la maji endapo maji bombani yanatoka kwa kasi.

Pia, ukichukuliwa mpira kuelekeza kwenye chanzo cha moto, yana kasi kubwa kumalizika, kuliko usawa wake wa kutoa maji bombani.

Mipira ya kuzimia inatajwa kuwa tofauti na kujaza ndoo bombani, suala la gari lenye mpira kujaza maji ni zaidi ya mpira wa kawaida.

Wasemaji wote wanaohusika na uzimaji moto, wanataka kuwapo vyanzo vya maji katika eneo la tukio au jirani na siyo kutegemewa safari ya kwenda na kurudi na kisha ndio kuendelea kuuzima moto.

Hali inabakia ileile ya miongo minne na nusu imevuka sasa, kuanzia Dar es Salaam iliyopita ya viwanda, ya leo imepanuka maradufu, makazi na biashara, ugumu katika zimamoto na uokoaji.

Inajenga picha kwamba, tangu uhuru wa nchi bado hakuna kituo cha Zimamoto na Uokoaji, chenye uwezo wa uhakika kujaza gari maji kwenda ‘kazini’ endapo wanahitajika kukabili moto mahali fulani, gari moja liapoondoka, la pili liwe linajaza maji.

Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, kinapaswa kuwa na magari na wataalamu wa kuyatumia katika namna sahihi, mathalan kujua cha kufanya endapo kuna mazingira ya upepo mkali, au mabati yanayoeneza moto kwa haraka katika mkasa.

Aidha, kuna suala la muda na taratibu za gari kuwa na maji yanayopatikana kirahisi, ukweli wake unabaki mtihani kwa Zimamoto na Uokoaji, mithili ya kuwapo zahanati yenye waganga na wauguzi, maabara, dawa na vifaa muhimu.

Hivyo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, linapaswa kuwa na bajeti inayojitosheleza kuiwezesha iwajibike inapasavyo, ikiaminika bado ni kati ya maeneo wakuu serikalini ‘wanazeeka’ kukuna vichwa wakitafuta suluhisho kwa manufaa ya wananchi.

… SAFARI TANGU KUUNDWA RASMI 1945

Huduma za Zimamoto Tanzania Bara, zilianza wakati wa utawala wa kikoloni baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia mwaka 1945. Kipindi hicho kulikuwa na kikosi kimoja tu kilichoitwa ‘Police Fire Brigade’ kilichosimamiwa na Jeshi la Polisi.

Miaka mitano baadaye, 1950 huduma hiyo iligawanywa katika makundi mawili, ambayo ni Zimamoto ya Manispaa iliyokuwa chini ya usimamizi wa Manispaa na Zimamoto Viwanja vya Ndege, chini ya Idara ya Kazi.

Kutokana na kupanuka miji, viwanja vya ndege na bandari, vikosi vingine vya Zimamoto vilianzishwa. Kimojawapo ni cha Bandari, ikisimamiwa na Mamlaka ya Bandari.

Mwaka 1982, huduma ya Zimamoto ya Viwanja vya Ndege, iliwekwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na vikosi vya Zimamoto vya Manispaa na Miji, viliongozwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, vikisimamiwa na wizara, pia tawala za mikoa na miji.

Kutokana na majukumu ya Zimamoto na Uokoaji kusimamiwa na mamlaka tofauti, ufanisi wake haukuridhisha, hata serikali ikalazimika kufanya maboresho.

Mwaka 1985, Bunge lilipitisha iliyoanzisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ili kuifanya huduma hiyo itolewe kwa nidhamu ya kijeshi, chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Badaaye mwaka 2007 Bunge lilipitisha Sheria ya Zimamoto na Uokoaji, unaoiweka hadi sasa vikosi vya Zimamoto na Uokoaji chini ya kamandi moja.

Kwa kiasi kikubwa, ilitoa fursa kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kujipanga kimuundo na mgawanyo wa majukumu wenye tija ili kurahisisha utoaji huduma ya zimamoto na uokoaji.

Hadi sasa kiutawala linaongozwa na Kamishna Jenerali anayesaidiwa na Naibu Kamishna Jenerali, akifuatiwa na Makamishna watatu, wanaoongoza divisheni tatu za jeshi hilo; utawala na fedha, operesheni na tawi la usalama wa umma na mali.

Chini ya divisheni hizo, kuna vitengo vinavyoongozwa na Makamishna Wasaidizi, ili kutengeneza mfumo wa kiutendaji wenye kuleta tija katika utoaji huduma kwa jamii.

Divisheni ya Usalama wa Umma ndio hasa mahsusi linahusika na kuzuia na kukabiliana na majanga kama moto, matetemeko ya ardhi na mafuriko, pindi yanapotokea na kufanya uchunguzi wa mkasa, ili kubaini chanzo chake na kupanga mikakati ya kukabiliana nayo.

Ni divisheni inayohusika na kuelimisha jamii kuhusu majanga ya moto na uokoaji, kukagua majengo, kuzuia moto, kupanga na kukagua usalama wa ujenzi katika viwanda, vituo vya mafuta na kemikali na vituo vinavyozalisha gesi.

Divisheni nyingine Operesheni, mbia katika jukumu hilo la kusimamia mafunzo, kukagua huduma za zimamoto na uokoaji kwenye kanda na kufanya tahmini ya madhara kwenye majanga mbalimbali.

ZAO LA MUUNDO

Kupitia muundo huo tajwa, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeboresha chuo chake, kufanya mapitio ya muundo wake wa ndani, kutafiti kuhusu madhara ya matukio ya majanga na kulinganisha matokeo ya ndani na nje ya tafiti hizo.

Hadi sasa inaeleza jeshi hilo limeshasambaza huduma zake kwa wananchi, kwa kuweka vituo vya zimamoto katika baadhi ya makao makuu ya mikoa, wilaya na maeneo muhimu nchi nzima.

Ni hatua inayoendana na wasifu wa kuhirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, kuongeza wigo wa utendaji.

Hadi sasa, Jeshi la Magereza ni mbia wake katika kutoa mafunzo ya kijeshi ya awali, uongozi mdogo wa kati na uongozi wa juu, kuwajengea uwezo kiutendaji maofisa na askari wa Zimamoto.

Vivyo hivyo, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, limekuwa karibu sana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, katika matukio ya uokoaji mkubwa.

Kwa mfano, Desemba 3, mwaka 1989 JWTZ ilishirikiana nao kukabiliana na moto uliotokea katika kampuni ya kusafisha mafuta ya Tazama Tank Farm Dar es Salaam na walifanikiwa kuuzima.

Mwaka 2001 pia vyombo hivyo vilishirikiana tena kupambana na moto wa mafuta uliotokea katika kinu cha kufua umeme yaani cha TANESCO Ubungo, Dar es Salaam Dar es Salaam na walifanikiwa kuuzima na kuokoa maisha na mali za wakazi.
Maeneo mengine ni katika ajali ya meli MV Spice na MV Scagit, huko Zanzibar.

Hadi sasa inaelezwa, JWTZ limeridhia ujenzi wa vituo vya Jeshi la Zimamoto kwenye baadhi ya maeneo ya kambi zake za Lugalo, Mabibo, Kigamboni, Mbagala na Gongolamboto.

 Makala hii imechangiwa na sehemu ya taarifa ya historia ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Nimi Mweta na Chritina Mwakangale

Habari Kubwa