Tuusikie mwenge tutunze mazingira

20Jul 2019
Reubeni Lumbagala
Dar es Salaam
Nipashe
Tuusikie mwenge tutunze mazingira

MWENGE wa uhuru unaendelea kukimbizwa katika maeneo mbalimbali ukizindua miradi ya maendeleo na kutoa elimu ya uraia kwa wananchi.

Kauli mbiu ya mbio hizo kwa mwaka huu wa 2019 ni “maji ni haki ya kila mtu. Tutunze vyanzo na tukumbuke kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa”.

Mbio hizi za mwenge ni muhimu kuendelezwa kutokana na umuhimu wake katika kuchagiza maendeleo kwa kuzindua miradi ya maendeleo na kuzungumzia masuala mbalimbali yenye tija kwa taifa  na kutoa elimu kwa  wananchi.

Sekta ya mazingira ni muhimu katika upangaji wa maendeleo. Bila kuwa na mazingira bora, juhudi za kimaendeleo zitakwama. Changamoto kubwa inayoikabili sekta ya mazingira ni kukosa utunzaji kutoka kwa wananchi wenye jukumu la kuyalinda ili kuwapo na ustawi na  maisha ya binadamu na viumbe hai wengine. Hivyo, juhudi kubwa zimekuwa zikifanywa na serikali pamoja na wadau wengine wa mazingira katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa sehemu salama ya kuishi kwa kutunza mazingira kwa maendeleo endelevu ya vizazi vya sasa na vya baadaye.

Kauli mbiu ya mbio za mwenge mwaka huu, imebeba ujumbe wa elimu kwa umma juu ya masuala mawili yaani utunzaji wa mazingira na uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu. Makala hii inaangazia eneo la utunzaji wa mazingira lililobebwa katika kauli mbiu ya mwenge wa uhuru. “Maji ni haki ya kila mtu. Tutunze vyanzo vyake”, hii ni sehemu ya ujumbe uliopo katika kauli mbiu hiyo ambayo inasomeka kwenye mikoa yote mwenge unapopita.

Maji ni uhai. Upatikanaji wa maji safi, salama na yenye kutosheleza unategemea namna mazingira yalivyotunzwa na kuhifandhiwa.

Bila kutunza vizuri mazingira pamoja na vyanzo vya maji, usambazaji wa huduma ya maji kwa wanachi utakwama kwani upatikanaji wa maji hautakuwa wa uhakika na hivyo kukwamisha juhudi za kuwafikishia wananchi huduma hiyo muhimu kwa matumizi ya viwandani na uzalishaji.

Wananchi ambao ni watumiaji wa maji wana wajibu wa kutunza mazingira ili maji yawafikie wale ambao bado hayajawafikia na huduma ya hiyo .

Viongozi wa mbio za mwenge wanapoendelea na shughuli zao za uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo, hutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na umuhimu wa wao kuwa mstari wa mbele kutunza mazingira ili kila mwananchi aweze kupata huduma ya maji.

Maji yataendelea kububujika kutoka katika vyanzo vyake kama vyanzo vya maji hayo vitatunzwa kikamilifu. Wananchi wahakikishe wanatoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa wale wanaofanya shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji.

Wapo wananchi wanaoendesha shughuli za kilimo na ukataji miti karibu na vyanzo vya maji ambavyo vinawahudumia wananchi wengi katika kuwapatia maji. Pamoja na ukweli kuwa wananchi wanayo haki ya kujishughulisha na shughuli za kiuchumi ili kujenga nchi, lakini ni muhimu shughuli hizo zisivunje sheria za nchi. Mwendelezo wa shughuli hizo za kilimo na ukataji miti kwa ajili ya mbao na kuni, ni kuharibu vyanzo vya maji na kusababisha wananchi kukosa huduma muhimu ya maji.

Maji yanahitajika sana kutokana na umuhimu wa wananchi kushiriki kilimo cha uhakika cha umwagiliaji ili kuwa na uhakika wa kuvuna badala ya kutegemea kilimo cha mvua.

Upatikanaji wa maji ukiwa wa kusuasua, utakwamisha juhudi za serikali za kuhamasisha wananchi kutumia kilimo cha umwagiliaji. Maji yakiwa hayapatikani au hayatoshelezi, itakuwaje kuhusu uanzishwaji wa kilimo cha umwagiliaji.

Maji pia ni bidhaa muhimu katika shughuli za viwandani kwani yanahitajika sana katika utengenezaji wa bidhaa mbalimbali na kwa matumizi ya huduma kuanzia hospitalini, shuleni na kwenye hoteli na migahawa.

Kuharibu mazingira ambapo kutasababisha uhaba wa maji ni kurudisha nyuma juhudi za serikali za ujenzi wa viwanda na ukuzaji uchumi.

Haya yote yanathibitisha namna ambavyo mazingira yanapaswa kulindwa kwa nguvu zote na kila mwananchi ili mipango mbalimbali ya kimaendeleo iweze kutekelezeka kwa urahisi.

Kabla ya wananchi kulalamikia ukosefu wa maji katika maeneo yao, wanapaswa kujiuliza kwanza juu ya ushiriki wao katika utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla.

Hakuna namna ambayo wananchi wanaweza kupata maji safi, salama na yenye kutosheleza kama vyanzo vya maji vitaharibiwa na wao wenyewe.

Hivyo basi, wananchi wazingatie elimu inayotolewa na viongozi wa mbio za mwenge kuhusiana na utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira ili kila mwananchi aweze kufaidi huduma ya maji.

Wote wanaohujumu sekta ya mazingira na vyanzo vya maji wachukuliwe hatua kali ili kuwa fundisho kwa wengine wanaocheza na uhai na maisha ya binadamu kwa kuharibu mazingira.

Kongole Mwenge wa uhuru, 2019 kwa kumulika utunzaji wa mazingira. Tafakari.