Tuzidishiwe uelewa wa kudhibiti mifuko plastiki

08Jun 2019
Reubeni Lumbagala
DAR
Nipashe
Tuzidishiwe uelewa wa kudhibiti mifuko plastiki

TANZANIA tunaweza tukiamua. Hivi ndivyo unavyoweza kusema ndugu msomaji wa safu hii. Ijumaa ya Mei31, 2019, ilikuwa mwisho ya kutumia mifuko ya plastiki nchini.

Mwezi huu tulio nao, mifuko ya plastiki haikupaswa kutumika tena badala yake mifuko mbadala ichukue nafasi.

 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alitoa kauli ya serikali kuhusu marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki. Tafiti zinaonyesha kuwa na madhara makubwa kwa ustawi wa mazingira na maisha ya viumbe hai.

 

Mnamo Aprili 9, mwaka  huu alipokuwa akijibu hoja za wabunge katika mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

 

Waziri Mkuu Majaliwa, anatamka:“Ifikapo Mei 31 mwaka huu itakuwa mwisho wa kutumia mifuko ya plastiki kubebea bidhaa mbalimbali. Kuanzia sasa tunatoa fursa ya viwanda kubadili teknolojia yao, wauzaji kuondoa mizigo yao na kumaliza kuuza yote na kadhalika.”

 

Anaendelea kusisitiza: “Ofisi ya Waziri wa Nchi Makamu wa Rais itajiandaa kutumia kanuni chini ya Sheria ya Mazingira, ili kulifanya katazo hili kuwa na nguvu ya kisheria. Tunachukua hatua hii kulinda afya ya jamii, wanyama mazingira na miundombinu dhidi ya athari kubwa zinazotokana na taka za plastiki.”

 

Nukuu hiyo ni sehemu ya mkazo uliotolewa na serikali kupitia Waziri Mkuu Majaliwa, kuhusiana na nchi kuachana na matumizi ya mifuko plastiki, kuhamia mifuko mbadala ambayo ni rafiki kwa mazingira na maisha ya viumbe hai.

 

Mwanzoni, taarifa ya kuachana na matumizi ya mifuko ya plastiki ilionekana  jambo gumu kutekelezeka kutokana na mazoea ya kutumia mifuko ya plastiki kwa matumizi mbalimbali.

 

Kutokana na msimamo thabiti wa serikali wa kuachana na matumizi ya mifuko ya plastiki na nchini, hivi sasa kuna mkazo wa kuongeza uzalishaji wa mifuko mbadala na suala hili sasa limekuwa halisi, yaani limewezekana.

 

Tanzania inaungana na Kenya na Rwanda kwa nchi za Afrika Mashariki na nchi nyingine duniani, ambazo zimeachana na matumizi ya mifuko ya plastiki.

 

Mifuko ya plastiki imekuwa na madhara makubwa kwa maisha ya viumbehai. Mathalani, mifugo inapoteza maisha kama itakula plastiki. Viumbehai wa baharini, pia vinapoteza maisha kwa kukosa hewa, pindi mifuko ya plastiki inapotupwa baharini.

 

Hivyo, juhudi kubwa zinazofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi za kuinua sekta hiyo, zinaweza kushindwa kuzaa matunda ipasavyo kutokana na madhara ya plastiki kwa kusababisha vifo vya viumbe hai hivyo.

 

Aidha, mifuko hiyo ya plastiki imekuwa na madhara pia kwa mazingira. Mifuko hiyo imekuwa chanzo kikubwa cha kusababisha kushindikana kuozesha taka kwenye vituo vya kukusanyia taka.

 

Taka zinazotupwa katika mashimo na vituo vingine vya kukusanyia taka zimekuwa zikidumu kwa muda mrefu kutokana na mifuko ya plastiki kuwa na uwezo wa kukaa kwa muda mrefu bila kuoza.

 

Ni jambo linalosababisha kuendelea kudumu kwa taka na kuchafua kwa kiasi kikubwa mazingira yetu. Athari nyingine zipo katika miundombinu, mifuko ya plastiki imekuwa ikisababisha kuziba kwa mifereji, hali inayochangia mafuriko, kwani maji yanashindwa kupita katika mifereji.

 

Mifuko ya plastiki imekuwa chanzo kikubwa cha kuzuia maji kushindwa kupita katika mifereji, hivyo inasababisha kutokea kwa mafuriko kila ifikapo majira ya masika.

 

Kutokana na hali hiyo, kuna uharibifu wa miundombinu kama madaraja na barabara unaotokea katika kipindi cha mvua. Ijulikane, miundombinu ni moja ya maeneo yanayotumia fedha katika ujenzi na ukarabati wa miradi yake.

 

Hivyo, ni lazima wananchi wafahamu namna mifuko ya plastiki imesababisha hasara kubwa kwa sekta ya miundombinu, kutokana na mifuko ya plastiki kusababisha mifereji na mitaro kuziba, hatimaye kutokea mafuriko yanayoathiri miundombinu.

 

Niseme, mifuko mbadala ni mweleko mzuri wa kuokoa fedha nyingi, zilizokuwa zikikarabati miundombinu, kutokana na madhara ya mafuriko.

 

Pamoja na kwamba tumeshaanza kutumia mifuko mbadala, upo umuhimu wa kuendelea kutoa elimu zaidi kuhusiana na athari za mifuko ya plastiki na umuhimu wa matumizi yake kwa maendeleo yetu.

 

 Serikali nayo inapaswa ishirikishe sekta binafsi katika kutoa elimu hii, ili kujenga jamii ya watu wenye uelewa. Vyombo vya habari navyo vitumike kwa juhudia kuielimisha jamii.

 

Wananachi waone matumizi ya mifuko mbadala ni mkombozi kwa maisha yao wenyewe na si kwa faida ya serikali. Watoe ushirikiano wa kutosha katika kutumia mifuko mbadala ambayo ni rafiki wa mazingira na afya zetu.

 

Cha muhimu, wawekezaji zaidi wajitokeze kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa, ili bidhaa ya mifuko mbadala zipatikane kwa bei rafiki ambayo wananchi wa wafanyabiashara wataimudu. Tafakari.

 

    •   Mwandishi wa makala hii ni mwalimu katika Shule ya Sekondari Mlali, iliyopo wilaya ya Kongwa, Dodoma. Anapatikana kwa simu: (+255) 764 666349.

Habari Kubwa