Tuzo hizi ni chachu kwa wote walimu, wanafunzi

30Nov 2019
Reubeni Lumbagala
Dodoma
Nipashe
Tuzo hizi ni chachu kwa wote walimu, wanafunzi

MOTISHA ni kichocheo katika kuchagiza ufanisi na utendaji kazi mahiri na wenye kutoa matokeo chanya. Ni hatua ya kuthamini kazi nzuri iliyofanywa na mtu mwingine katika kuleta mabadiliko ambayo ni chachu ya mwendelezo wa mambo bora zaidi ya sasa na baadaye.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jafo, picha mtandao

Hivi karibuni, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jafo, amekuwa shuhuda wa utoaji Tuzo za Elimu kwa wanafunzi na walimu na shule zilizofanya vizuri kwenye matokeo ya mitihani ya kidato cha sita na darasa la saba kwa mwaka 2019, na kusema kuwa ni chachu ya kuendeleza kazi za kutukuka.

Katika hafla hiyo, Waziri Jafo anatoa fursa kwa wanafunzi waliofanya vyema katika mitihani ya darasa la saba kuchagua shule za sekondari wanazozipenda ili kuendelea na masomo yao.

Anasema kwa wa kidato cha sita Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, iliachiwa wanafunzi wa kidato cha sita ili iweze kuwasaidia kujiunga na vyuo vikuu wavipendavyo. Waziri anasema “Yule kijana Tanzania One nilimsikia anasema anatamani kwenda Shule ya Sekondari Ilboru nitashangaa sana kama hatakwenda huko, hawa ni vijana spesho waambieni wachague shule wanazotaka waende kusoma.

“Naomba niwahakikishie, Rais John Magufuli na serikali anawapenda sana, mtachagua shule zile mnazotaka ninyi kwenda kusoma, Katibu Mkuu shughulikia hilo”.

Uhuru waliopewa wanafunzi kuchagua shule na vyuo wanavyovitaka ni motisha kubwa kwani wakati mwingine licha ya kufanya vizuri wanasoma katika shule ambazo hazikuwa matarajio yao na hilo huenda linawavunja moyo kwa sehemu.

Tuzo na zawadi hizo zilizotolewa kwa walimu na wanafunzi zitachechemua kwa kiasi kikubwa ukuaji wa taaluma mashuleni. Wanafunzi na walimu, kila mmoja ataongeza ari katika usomaji na ufundishaji ili kuendelea kupata tuzo na zawadi hizo mara nyingi zaidi.

Ni vyema tuzo hizi zikawa ni jambo endelevu ili kuendelea kujenga shauku kwa walimu na wanafunzi kujituma zaidi. Motisha ni eneo muhimu linalohitaji uwekezaji ili kuongeza tija ya kazi.

Katika sehemu mbalimbali kama maeneo ya kazi, taasisi za elimu, kampuni za umma na binafsi na katika familia utoaji wa motisha ni jambo jema ambalo linahamasisha matokeo chanya na utendaji kazi wenye kasi na viwango. Ndiyo maana katika katika kuziangazia nafasi za tuzo na zawadi katika kuchochea ukuaji wa taaluma kwa shule za msingi na sekondari nchini ni jambo muhimu.

Sekta ya elimu ni muhimu kwa maendeleo ya kila nyanja kama vile kijamii, kiuchumi na hata kisiasa. Kutokana na umuhimu wa elimu, kumekuwa na mikakati ya kuifanya itoe matokeo chanya hasa kwa wanafunzi ambao wapo shuleni kwa ajili ya kusaka maarifa, ujuzi na stadi mbalimbali.

Mkakati mmojawapo wa kuchagiza ukuaji wa taaluma ni pamoja na utoaji wa tuzo kwa wanafunzi na walimu kama njia ya kuwahamasisha kujifunza na kufundisha kwa bidii, nidhamu na weledi ili matunda ya elimu hiyo yaweze kuonekana kwa wahusika.

Pamoja na kuwa mwanafunzi anao wajibu wa msingi wa kusoma kwa bidii, kujifunza bila kuchoka na kujituma katika masomo, lakini upo umuhimu wa kuthamini kazi nzuri iliyofanywa na wanafunzi hadi kufanya vizuri katika masomo yao kwa kutoa tuzo na zawadi kwa wahitimu wetu.

Halikadhalika, walimu nao wanao wajibu wa msingi wa kufundisha kwa bidii, kujituma katika majukumu yao, aidha, ipo haja ya kuthamini kazi za walimu kwa kutoa tuzo na zawadi kwa wale ambao masomo yao yamefanya vizuri katika mitihani ya taifa.

Katika hafla hiyo ya utoaji tuzo iliyoratibiwa na Taasisi ya Elimu ya Global Education Link kwa kushirikiana na Baraza Mitihani Tanzania (Necta) na kufanyika jijini Dar es Salaam, Jafo anasema tuzo hizi ni chachu ya ukuaji wa taaluma na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.

“Hizi ni tuzo za kwanza kutolewa na serikali kwani vijana na walimu waliofanya vizuri kwenye mtihani hiyo wanastahili pongezi ili waendelee kufanya vizuri. Tunaamini itaongeza ubora zaidi kwa shule zetu kuendelea kufanya vizuri” anasisitiza Jafo.

Jambo la kipekee katika tuzo hizi ni kwamba wanafunzi na walimu kwa pamoja wanathaminiwa kwani hawa wawili wanategemeana katika kufikia mafaniko ya kitaaluma. Kama walimu watajituma kufundisha kikamilifu na kwa mujibu wa mitaala, huku wanafunzi wakishindwa kujisomea kwa bidii, juhudi za walimu hazitazaa matunda yanayotarajiwa.

Vivyo hivyo kwa wanafunzi ambao wanapenda kusoma huku wakikosa walimu wa kuwafundisha watashindwa kufikia malengo yao ya kufaulu masomoni kwa viwango vya juu. Kwahiyo, ni vyema matokeo mazuri yanapotokea, kila mmoja yaani mwalimu na mwanafunzi kutambuliwa mchango wake katika mafanikio hayo kwani kwa pamoja watakuwa wamewezesha kufikia mafanikio hayo.

Tafakari.

Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.
Maoni: (+255) 764 666349.

Habari Kubwa