Ubongo wa mtoto unavyojengwa katika kipind cha ujauzito

17Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Ubongo wa mtoto unavyojengwa katika kipind cha ujauzito

WAKATI wa ujauzito kinamama wengi huwa na ‘presha’ kubwa ya kuhakikisha wanapata mtoto asiye na matatizo kiafya.

Kutokana na hali hiyo, wanawake hao wamekuwa wakitafuta ushauri kwa watangulizi wao, yaani wamama ambao wamepitia hali ya ujauzito na malezi na wengine huwasumbua madaktari, ili mradi tu kujikinga na hatari yoyote inayoweza kumpata yeye mwenyewe au mtoto aliye tumboni.

Mbali na kutakiwa kuhudhuria kliniki na kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu afya ya mama na mtoto; mama anapaswa kulinda mwenendo wake hasa kwenye suala la ulaji.

Wataalam wa afya wamethibitisha kuwa baadhi ya vyakula vina uwezo mkubwa wa kujenga uwezo wa mtoto kujifunza na kujenga akili yake na vingine vinaweza kuharibu akili ya mtoto hata kabla hajazaliwa.

Baadhi ya vyakula ambavyo mama anapaswa kula awapo mjamzito na vile anavyotakiwa kuviepuka katika kipindio hicho.

VITAMINI
Kula vyakula vyenye vitamini kwa wingi kila siku. Wataalam wa afya wanaeleza kuwa ili kumjenga mtoto mama anapaswa kula vyakula vyenye folic acid na vitamini B12 ili kujenga seli nyekundu za damu, vitamini C kuzalisha collagen, vitamini D kwa ajili ya kujenga mfupa, na zinki kwa ajili ya maendeleo ya ubongo.

Hata hapa nchini, kila mjamzito anapohudhuria kliniki amekuwa akishauriwa kupatiwa vidonge vya aina ya folic acid. Kwa bahati mbaya, baadhi yao huwa hawavimezi, jambo linalowakosesha watoto virutubisho muhimu kwa ajili ya afya ya ubongo.

PROTINI
Wataalamy wanashauri kuwa, mjamzito aanapswa kula vyakula vyenye utajiri wa protini kama vile samaki, vinaongeza nguvu ya ubongo wa mtoto aliye tumboni.

Utafiti kutoka Harvard Medical School, ambayo ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Havarad, Marekani unaeleza kuwa ulaji wa samaii kwa wingi wakati wa ujauzito, hasa katika miezi sita ya mwanzo, kuna mchango wa kuujenga ubongo.

“Vyakula vyenye protini kwa wingi hujenga seli muhimu kuufanya ubongo wa mtoto kufanyakazi haraka,” anasema Profesa Lisa Eliot wa Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Rosalind Franklin, kilichopo Chicago, Marekani.

Profesa Eliot, anashauri kuwa kama mama hapendi samaki, azungumze na daktari wake ili amshauri vyakula mbadala au vidonge vya mafuta ya samaki.

Hata hivyo, wataalam wanashauri mama achukue tahadhari kwani baadhi ya samaki wana madini ya zebaki ambayo yanaweza kumletea madhara.

Kazi nyingine ya protini ni kujenga seli na homoni kwa ajili ya ukuaji wa mtoto.

Baadhi ya vyakula vingine na ambavyo havina gharama kubwa, ni supu (mchuzi mzito) wa maharage au mboga za majani, siagi pamoja na karanga.

Vyakula vingine vyenye protini kwa wingi ni maziwa, nyama na mayai.

MATUNDA
Mtaalamu wa lishe, Elizabeth Somer, anapendekeza ulaji wa matunda kwa wingi kwa mjamzito.

“Matunda yana virutubisho kwa ajili ya afya ya ubongo kwa kulinda tishu za eneo hilo zisiharibiwe,” anasema Somer.
Baadhi ya matunda ambayo mama anaweza kula ni machungwa, papai, parachichi, ndizi mbivu na hata nyanya, huku akizingatia kuosha kwa maji safi kabla ya kula.

MADINI YA CHUMA
Kula vyakula vyenye chuma kwa wingi. Wataalamu wa lishe wanaeleza kuwa ulaji wa vyakula vyenye madini ya chuma wakati wa ujauzito, husaidia katika usambazaji wa endelevu oksijeni kwa mtoto na kukabili tatizo la upungufu wa damu.

Hata hivyo, Somer anasema wanawake wengi hupata ujauzito wakiwa tayari na upungufu wa madini hayo na anashauri kuwa mama mjamzito achunguze wingi wa madini hayo aendapo kliniki ili aweze kuchukua hatua stahiki.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), ni kwamba karibu asilimia 85 ya upungufu wa damu au anaemia wakati wa ujauzito husababishwa na upungufu wa madini ya chuma mwilini.

Upungufu wa madini ya chuma unaweza kusababishwa na kula chakula chenye kiasi kidogo cha madini haya au mwili wa mjamzito kushindwa kutunza madini ya chuma ya kutosha kutokana na ama mimba zilizopita au kupoteza kiasi kikubwa wakati wa hedhi, kabla ya kushika mimba.

Baadhi ya vyakula vyenye utajiri wa madini ya chuma ni nyama, samaki, kunde, dagaa, kabichi na jamii yote ya nafaka.

TAHADHARI
Jihadhari na pombe. Wataalamy wa lishe wanaeleza kuwa matumizi yoyote ya pombe yana athari kwenye afya ya ubongo wa mtoto.

Wanaeleza kuwa unywaji pombe unasababisha matatizo ya uwezo wa mtoto kujifunza, kutunza kumbukumbu na majukumu mengineyo ya kijamii.

Usiongezeke uzito kupita kiasi. Pamoja na kwamba mjamzito anakula zaidi anapaswa kudhibiti uzito wake kwani uzito mkubwa unamuweka kwenye hatari ya kujifungua kabla ya wakati yaani kupata mtoto njiti.