Ubunge kazi isiyohitaji elimu, uzoefu wala masharti

25May 2016
Restuta James
Dar es Salaam
Nipashe
Ubunge kazi isiyohitaji elimu, uzoefu wala masharti

UKICHUNGUZA kisa cha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, kutimuliwa kwa ulevi, utabaini ni kwa nini Tanzania inahitaji Katiba mpya leo, wala siyo kesho.

wabunge

Rasimu ya pili ya Katiba ambayo ilitolewa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, miongoni mwa vipengele muhimu vilivyokuwamo ni elimu ya mbunge isipungue kidato cha nne.

Kwamba ilitaka mbali ya mbunge kutakiwa kujua kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili na Kiingereza, awe na elimu hiyo.

Hata hivyo, ‘wajanja’ wachache waliokaa kwenye Bunge Maalum la Katiba, walikifuta kipengele hicho na kuacha sifa ya kujua kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza!

Sifa za mbunge kama zilivyo kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, anatakiwa awe raia wa nchi hii, mwenye umri usiopungua miaka 25 na awe ni mwanachama aliyependekezwa na chama cha siasa.

Sifa nyingine ni uadilifu na asiwe ametiwa hatiani kwa kosa la kukwepa kulipa kodi ya serikali, miaka mitano hadi tarehe ya kupiga kura.

Kitendo cha Bunge Maalum la Katiba kufuta sifa ya elimu ya sekondari kama moja ya sifa za msingi za mbunge kilizua maswali mengi, lakini mengine nitaeleza leo.

Awali ya yote nieleze tu kwamba, Naibu Katibu Mkuu wa Bunge, John Joel, ameliambia gazeti hili kwamba hakuna kifungu chochote cha kanuni za Bunge kinachomzuia mtu kuingia bungeni akiwa amelewa.

“Kanuni zinahusiana na uendeshaji wa shughuli za Bunge, hizi za maadili ni Kanuni za Maadili ambazo zinatakiwa kutungwa ili kudhibiti hali hiyo,” alisema.

Hapa ndipo msingi wa hoja yangu ulipo. Mbunge huyu ili awakilishe wananchi mathalani 200,000 bungeni anatakiwa ajue tu kusoma na kuandika (kwa ufasaha au vinginevyo), haijafafanuliwa.

Pamoja na kuwa ana majukumu lukuki ya kuchambua bajeti, kukagua miradi ya maendeleo, kutunga sheria, kuchambua na kupitisha mikataba ya kimataifa; hata akiwa amelewa ‘tilalila’ hazuiwi kutekeleza majukumu yake hayo!

Ubunge naweza kusema ndio kazi rahisi kuliko zote nchini Tanzania. Mathalani, hivi sasa, mtu akitaka msichana wa kazi za ndani anatamani sana ampate aliyemaliza angalau kidato cha nne pale St. Kayumba, anakuwa na uelewa zaidi kuliko ambaye ameishia darasa la saba.

Kama hivyo haitoshi, hakuna ofisi ambayo inaajiri mhudumu wa ofisi (office attendant), ambaye hajafika kidato cha nne, kampuni za usafi zinataka watu waliofika kidato cha nne hata kama walifanya vibaya, lakini angalau wamepita hapo.

Tuje kwenye dereva wa mbunge mwenyewe. Sifa namba moja ni lazima awe amehitimu kidato cha nne na awe amesomea udereva na kupata leseni ya daraja C; hili halina mjadala!

Pamoja na kwamba dereva atamwendesha mtu mmoja au mfanya usafi atakuwa na kazi ya kushika fagio, dekio au kitambaa kufuta meza; analazimika kuwa na angalau elimu ya sekondari, kwa mbunge hilo halipo.

Mfagiaji huyu naye anatakiwa awe na nidhamu ya hali ya juu awapo eneo la kazi. Kwanza kabisa hatakiwi kwa namna yoyote ile kuja kazini akiwa amelewa. Akithubutu kukiuka sharti hilo, atakuwa amemtangazia mwajiri wake nia yake ya kutoendelea na kazi.

Kumbuka pia kuwa mshahara wa mfagiaji huyu ni tone la posho ya siku ya mbunge.

Sasa tujiulize, mbunge haitaji kuwa na elimu zaidi ya kujua kusoma na kuandika, ‘hazuiwi’ kwenda kazini akiwa amelewa na mshahara pamoja na marupurupu yake ni lukuki! Akisinzia sawa, akikoroma bungeni sawa, akipiga soga sawa na hata akirusha vijembe ni sawa tu!

Ndio maana baadhi ya watu wanahoji heshima ya Bunge na hasa katika kuisimamia serikali.

Aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Prof. Mwesiga Baregu, anasema kwenye tume waliona umuhimu wa kuweka sifa ya kidato cha nne kwa mbunge ili kulinda hadhi ya Bunge na mbunge mwenyewe.

Mbali ya sifa hiyo, anasema tume ilipendekeza pia Mawaziri wasitokane na wabunge ili Bunge libakie kuwa mhimili huru unaojitegemea na ambao ungeweza kujenga nidhamu ya wabunge.

“Kwa hiyo utaona Kitwanga amefutwa uwaziri, lakini atabaki bungeni na ulevi wake,” anasema.

Anasema Bunge Maalum lilikataa pendekezo la rasimu: “Inaonyesha nia ya kutothamini ubunge kama kitu nyetu na kutoona kazi kubwa alizonazo.”

Anasema: “Tuliweka sharti ili kumfanya mtu anayetaka kuwa mbunge sharti afikie kiwango fulani cha uelewa…nadhani ingesaidia kujenga hadhi ya mbunge na Bunge.”

Prof. Baregu anasema: “Mbunge ana wajibu mkubwa na hadhi kubwa kwenye jamii kwa hiyo lazima wajiheshimu.”
Anasema walioondoa kipengele cha elimu walijenga hoja kwamba ni kuondoa haki ya kuchagua na kuchaguliwa, bila kuzingatia wajibu.

“Haki lazima iende na wajibu, tukasema kwamba wajibu ni angalau apate elimu ili aweze kuitumia vizuri haki ya kuchaguliwa na alete tija. Hii pia ingejenga mfumo wa nidhamu kwa Bunge lenyewe,” anasema.

Hivi kweli bado hatuoni umuhimu wa kuwa na Katiba mpya tena ya kuanzia kwenye Rasimu ya Pili ya Jaji Warioba?

Habari Kubwa