Uchakataji kizamani malighafi ghali upanga unaozichana bidhaa za ngozi

26Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
Tarime
Nipashe
Uchakataji kizamani malighafi ghali upanga unaozichana bidhaa za ngozi

WATU wanajiuliza inakuwaje bidhaa zinazozalishwa nchini zinauzwa ghali wakati zinazotoka nje zinapatikana kwa bei nafuu na kununuliwa kwa wingi kuliko za hapa nyumbani?

Bidhaa za ngozi vikiwamo viatu hukosa soko baada ya wateja kukimbilia mitumba. PICHA: DINNA MANINGO

Jibu linaweza kuangaliwa kwenye sekta ya ngozi. Takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 zinaeleza kuwa idadi ya Watanzania ni milioni 44. 9.

Wakati takwimu za mifugo zinafahamisha kuwa ni nchi ya tatu kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo barani Afrika, wanaokadiriwa kufikia milioni 30.5, na mapato yake yakichangia asilimia 7.4 ya pato la taifa. 

Licha ya kuwapo kwa mifugo mingi bado taifa halijaweza kuwa na bidhaa za ngozi za kutosheleza mahitaji na badala yake, mitumba kuanzia viatu, mikanda, mifuko na nguo vinavyouzwa kwa bei ya chini ndiyo, inayotamba.

Kutokana na kukosekana teknolojia na bei inayovutia wateja wa viatu kikundi cha TAREPA kilichokuwa kinatengeneza viatu vya ngozi kimesambaratika baada ya bidhaa zake kudoda sokoni, anasema Marwa Tongori mmoja wa wana kikundi.

"Nilikuwa msindikaji wa sabuni, mvinyo, baadaye 2009  Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), walitupa mafunzo ya kutengeneza chaki mjini Musoma kwa siku 14, tukatengeneza chaki na kuzipeleka shuleni kupitia waratibu elimu kata, lakini wakazikataa kwa madai ya kuwaumiza macho, wakati huo maduka yalikuwa na punguzo la bei tukakosa wakumuuzia,” anasema Tongori.

"SIDO ilitukusanya tena tuliopata mafunzo ya chaki tukafunzwa kusindika ngozi tukajifunza siku 14, ilitutafutia walimu wakafika Tarime wakatufundisha kutengeneza bidhaa za ngozi," anaongeza.

Anasema biashara ya kutengeneza bidhaa hizo inalipa lakini, imeathiriwa na mtumba huku malighafi za ndani zikiuzwa ghali ikilinganishwa na zinazoagizwa nje na kuongeza: "Tunatoa ngozi kwenye machinjio ya Tarime kilo moja ni Sh.1,200, ya mbuzi ni kati ya Sh. 500-1,500, usindikaji wake ili ukamilike unachukua siku 22. Tunatumia chumvi, chokaa na kuziloweka siku tano, tunaondoa chokaa kwa pumba za mahindi, lakini pumba nazo tunaziondoa kwa kutumia maji ya mapapai ili kuzilainisha na kuzipaka mafuta ya karanga.”

"Ngozi ikilainika inapakwa unga wa magome ya mti ili kuiimarisha, magome hayo yanapatikana Mbeya yakiuzwa kilo 50 kwa Shilingi 150,000, halafu hatua za usindikaji zinaanza, ukiwamo umaliziaji wa kuondoa manyoya na nyama zilizosalia kwenye ngozi kwakutumia panga …. " anasema Tongori.

Kinachofuata baada ya hatua hiyo ni kuandaa viatu, kuweka soli, namba, rangi, magongo ya kuweka shepu ili kutengeneza viatu. Pea ya kiatu inauzwa Sh.20,000, gundi ya moto lita tano Sh.3,000,000 inayozalisha viatu pea 50, gundi ya kuunganishia viatu kwenye jointi lita tano Sh.20,000 nyuzi na vifaa vinginevyo,” anatoa mchanganuo wa hasara.

MAUZO YALIVYOKUWA

Tongori anasema ukosefu wa soko la viatu vya ngozi uliwavunja moyo wanakikundi kutokana na kukaa muda mrefu bila kuuzika, kulikosababisha hasara na kwamba walikuwa wanauza pea nane au 10 kwa mwezi. Viatu vya ngozi vinaogopwa vina bei kubwa hivyo watu kukimbilia mitumba.”

Anaongeza kuwa Sh. 5,000 inatosha kununua viatu vya mtumba wakati vya ngozi ni ghali huuzwa Sh. 20,000.

TEKNOLOJIA DUNI

Bhoke Marwa mkazi wa mtaa wa Bomani anasema teknolojia za kizamani kutengeneza ngozi hadi kuzalisha viatu hauwavutii wateja, inatoa bidhaa duni na kuchangia wateja kukimbilia viatu vya mitumba.

"Mtumba ina miundo mbalimbali inayomvutia mnunuzi ukitaka cha staili fulani huwezi kukikosa, lakini hivi viatu vya ngozi miundo yake haivutii ni kama vinafanana,ukitaka kiatu cha muundo fulani mpaka ukaweke oda kiwandani, mimi nataka kiatu unaniambia nisubiri wakati kwenye mitumba unakuta kila fasheni," anasema Marwa.

Utaalamu na ujuzi katika kutengeneza bidhaa zitokanazo na ngozi nayo imeelezwa kuwa ni sababu inayochangia kushuka kwa soko la viatu vya ngozi kutokana na utaalamu usioendana na wakati na vitendea kazi vya kizamani vilivyopitwa na wakati.

John Chacha mkazi wa mtaa wa Rebu anasema: " Leo tunafanya mambo ya kidijitali lakini bado tunachakata ngozi kwa kuilainisha kwa mapapai, nyama inaposalia kwenye ngozi tunaitoa kwa panga haya ni mambo ya kizamani.”

" Matokeo yake kiatu kikitengenezwa baada ya miezi kadhaa kinakuwa kigumu, kinakakamaa kama ngozi iliyokuwa imechunwa ikatupwa juani ikakauka na kukakamaa, nchi haina chuo cha kujifunza uchakataji wa ngozi na utengenezaji wa viatu kwa teknolojia za kisasa ili hawa wenye viwanda vidogo wapate utaalamu wa kisasa ?" anahoji.

MITUMBA NI TISHIO

Deo Ching'wa muuza mitumba mtaa wa Serengeti anakiri vimeua soko la viatu vya ngozi vinavyotengenezwa na viwanda vidogo nchini.

"Uzuri wa viatu vya mtumba vina bei zote ya chini ya juu kumwezesha kila mtu kununua kulingana na pesa yake, lakini vya ngozi bei zake si rafiki kwa wenye maisha magumu.

"Ukienda mnadani unapata kiatu hadi cha Sh. 2,000 mwenye kipato cha chini hawezi kushindwa, japo siyo imara lakini ni nafuu atatumia kwamuda akitafuta pesa nyingine, lakini ngozi ni ghali tena kiatu cha hapa Tarime hata kwa Sh. 10,000 hupati. Mtu una watoto watano kipato chako ni cha chini hawezi kununua, unaona hiyo pesa akienda kwenye mitumba anapata viatu pea tano,” anasema Ching'wa.

Gharama kubwa za malighafi za kutengeneza ni chanzo cha bei kubwa na kwamba zingepungua wazalishaji wangemudu na wateja wangepatikana, viatu vya ngozi ni imara na vinadumu, anasema.

"Kiatu cha mtumba kimetumika kinaweza kuwa cha ngozi, plastiki au kitambaa lakini vimeshavaliwa kwenye nchi za wenzetu halafu tunaletewa tunauziwa kwa bei ya chini.”

"Kuna viatu vya ngozi vya mtumba vinauzwa mpaka Sh. 100,000  au zaidi, watu wananunua lakini ni wachache, wanaovielewa na wenye kipato kikubwa, wanaotengeneza viatu vya ngozi wajitahidi viwe imara na mwonekano mzuri, muundo unaovutia na unaokwenda na wakati," anashauri Ching'wa.

Ramadhani Khalfan ni fundi bidhaa za ngozi katika Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT) tawi la Mwanza, anasema taasisi hiyo ina chuo kinachotoa mafunzo ya kuchakata ngozi na kutengeneza bidhaa zitokanazo na ngozi.

" DIT tunachakata ngozi zikiwamo za wajasiriamali, kama wanaweza kukusanya ngozi wanaruhusiwa kuzileta wakati wowote, gharama ya kuchakata ni ya ng'ombe Sh. 25,000, mbuzi 5,000 na tunafundisha kuanzia kuchakata na kutengeneza bidhaa za ngozi," anasema.

Kuna kozi fupi, zipo za miezi miwili na za kutengeneza viatu, zote hutolewa kwa miezi miwili na kila kozi hugharimu Sh. 300,000, anasema.

Anaongeza kuwa zipo kozi za muda mrefu ambazo ni ya kuchakata ngozi na kutengeneza bidhaa inyoanza mwaka huu nakwamba DIT Mwanza ni chuo pekee nchini kinachotoa mafunzo ya ngozi kwa ngazi ya diploma.

Godfrey Chasama ni mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) anasema kuwa Tanzania inazalisha ngozi ghafi na kwamba bei ya ngozi ghafi ni 4,500 inayotoa jozi tano   za viatu, bei ya jozi ni Sh.14,000 uwezo wa kuzalisha ni jozi 240  kwa mwezi.

Habari Kubwa