Uchimbaji holela madini unavyoharibu mazingira

17Jun 2021
Marco Maduhu
Kahama
Nipashe
Uchimbaji holela madini unavyoharibu mazingira

MIGODI midogo ya madini ya dhahabu, kwa sehemu kubwa inachangia kuharibu mazingira, kutokana na kutawaliwa na uchimbaji wa kukisia uwapo wa madini, inayoishia kuachwa mashimo.

Wanahabari waliozuru kwenye mgodi mdogo wa madini ya dhahabu, Mwanzimba Wilaya ya Kahama. PICHA ZOTE: MPIGAPICHA WETU

Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga ina migodi mingi midogo ya dhahabu na baadhi yake imeharibu mazingira kwa kiasi kikubwa.
 
Mgodi wa Mwanzimba uliopo Msalala wilayani Kahama, tayari mazingira yake yameshaathirika kutokana na awali kabla ya kupatikana leseni, kulikuwapo na uchimbaji holela wa madini.

MENEJA MGODI
 
Meneja wa Mgodi huo wa Madini, Mwanzimba Ndembuke, anasema mashimo yaliyopo mgodini humo yametokana na awali kila aliyekuwapo alijaribu bahati yake ya kupata madini na hatimaye waliishia kuharibu mazingira.
 
Anasema, walianza kuchimba mgodini humo mwaka 2007 na baada ya kupata leseni ya uchimbaji, sasa wanafuata sheria na kanuni, inayopafanya pasiwapo mashimo yanayobaki kama ilivyokuwa awali.
 
"Mgodi huu wa madini, awali kulikuwa na uchimbaji wa uvamizi na katika uchimbaji huo, lazima kutokee tu tatizo la uharibifu wa mazingira,” anaeleza Meneja Ndembuke.

Anaendelea na ufafanuzi: “Kila mtu anajaribu bahati yake ya kupata madini na ndio tatizo hutokea la kuacha mashimo ovyo na ukataji miti holela."
 
"Tunaishukuru serikali kututambua sisi wachimbaji wadogo na kuanza kutupatia leseni za uchimbaji madini, hali ambayo imeanza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia tatizo hili la uharibifu wa mazingira, sababu ya kuacha kuchimba madini holela," anaongeza.

OFISA UTAFITI

Evans Rubara, ni Ofisa Programu na Utafiti kutoka Taasisi ya Kuendeleza Uchimbaji Mdogo wa Madini Tanzania, anasema ili kuzuia uharibifu wa mazingira kwenye machimbo madogo, kuna haja Wizara ya Madini itoe leseni kwenye maeneo yaliyokwishatafitiwa uwapo wa madini yake.
 
Anasema wachimbaji wadogo siyo wataalamu wa jiolojia, hivyo wanachimba madini kwa kukisia kuwa, hata wanaharibu mazingira.
 
"Sisi kama Taasisi ya Kuendeleza Uchimbaji Mdogo wa Madini tunaiomba Wizara ya Madini, kabla ya kutoa leseni kwa wachimbaji wadogo wa madini, wahakikishe kama kweli sehemu hiyo kuna madini kwa kutumia vipimo vya kitaalamu, ili kusitokee uharibifu wa mazingira," anasisitiza.
 
Anafafanua kwamba, ni kawaida wachimbaji wadogo wamekuwa na tabia ya kuhama na kwenda kwingine, hasa wanapogundua mahali husika madini hayapatikani na hali inatokea wakati wameshaharibu mazingira kuwa na mashimo na eneo la jangwa.

OFISA MADINI
 
Marwa Geteny kutoka Ofisi ya Madini Mkazi wilayani Kahama, ambaye ndiye mtoaji leseni kwa wachimbaji, anafafanua kuwa sheria za madini zinazuia uharibifu wa mazingira, lakini kwa wachimbaji bado tatizo lipo.
 
Anasema kwa Wizara ya Madini inahamasisha wachimbaji wadogo wajiunge kwenye vikundi, ili wapewe lesseni ya uchimbaji madini yenye masharti ya kutunza mazingira.
 
"Utoaji leseni kwa wachimbaji wadogo wa madini utasaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia tatizo la uharibifu wa mazingira, kwa sababu kabla ya kupewa leseni ni lazima uje na mpango mkakati wa namna ya kutunza mazingira," anafafanua Geteny.
 
Pia anafafanua kwamba kwa sasa wanazuia wachimbaji wadogo kuvamia maeneo kuokoa mazingira, bali wachimbe kwenye maeneo yaliyofanyiwa utafiti. Anasema, hadi sasa wameshatoa jumla ya leseni 400 kwa wachimbaji wadogo.

DC KAHAMA
 
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Annamringi Macha, anawaasa wachimbaji wadogo wilayani kwake kufuata sheria za uchimbaji madini na kwa sasa serikali inawatambua rasmi wachimbaji wadogo wa madini.

Pia anasema serikali imeshawarasimisha, anaendelea: "Naomba Wizara ya Madini na taasisi ya kuendeleza uchimbaji mdogo wa madini. Toeni elimu kwa wachimbaji wadogo kuhusu namna ya kujua sheria ya madini, utunzaji mazingira, hasa kwa kupanda miti kwenye maeneo yenye mashimo."
 
WENYE ULEMAVU

Mwenyekiti wa Shirikisho la Chama cha Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) wilayani Kahama, Michael Mkanjiwa, anawataka wamiliki migodi wilayani humo kuwaajiri ili nao wafanye kazi ya kutunza mazingira.
 
Anasema, wenye ulemavu wametengwa sana katika migodini akijiteta bado wana nafasi ya kuajiriwa kwa kazi nyepesi, ikiwamo utunzaji mazingira.
 
"Sheria ya Ajira ya Watu wenye Ulemavu ya Mwaka 1982, inasema asilimia tatu ya wafanyakazi kwenye eneo lolote lile wanapaswa kuwapo na walemavu. Hivyo, tunaomba kwenye migodi ifuatwe sheria hii, ikiwa tunaweza kufanya kazi nyepesi," anasema Mkanjiwa.
 
"Mfano kwenye migodi mingi ya uchimbaji madini hasa hii midogo, kuna tatizo kubwa la uharibifu wa mazingira, lakini sisi watu wenye ulemavu tukipata ajira, tuna uwezo wa kutunza mazingira pamoja na kupanda miti, kitu ambacho hatuwezi kushindwa kufanya," anaongeza Mkanjiwa.
 
Hosea Mbusule, ni Katibu katika mgodi wa madini ya Dhahabu Mwanzimba, anasema kwa sasa wameshaajiri wenye ulemavu wawili, waliojikita kutunza mazingira.
 
Anasema shughuli yao kubwa ni usafi wa mazingira, huku wakiangalia namna ya kuajiri wengine wenye ulemavu, pia kupanga mkakati wa upandaji miti kwenye mashimo, ambayo awali yalisababishwa na uchimbaji holela kabla ya kupewa lesseni.
 
MTUNZA MAZINGIRA

Kaimu Ofisa Misitu na Mazingira mkoa Shinyanga, Perfect Mbwambo, anasema hali ya utunzaji mazingira kwenye migodi ya madini na mkoa Shinyanga kwa jumla ni upandaji miti.
 
Anashauri migodi midogo ya madini iige mfano wa mikubwa, ukiwamo wa almasi Mwadui Williamson Diamond, wenye programu ya kuotesha miti na kutunza mazingira.
 
"Hali ya uharibifu wa mazingira mkoani Shinyanga ni mkubwa sana na hii inatokana na shughuli za kibinadamu, ikiwamo uchomaji mikaa, na shughuli za uchimbaji madini," anasema Mbwambo.
 
Anasema katika mkakati wa kitaifa wa utunzaji mazingira, kila halmashauri nchini inatakiwa kupanda miti na kila halmashauri inapaswa kupanda miti kwa milioni 1.5 kila mwaka, lakini Shinyanga utekelezaji uko chini.
 
Takwimu za upandaji miti kwa halmashauri sita za za mkoa huo kwa 2019 hadi 2020; Manispaa ya Kahama ilitajwa kupanda miti milioni 1.5 lakini wamepanda 14,000.

Pia, anataja halmashauri nyingine kuwa Kishapu imepanda  160,180; Msalala  91,250; Ushetu 565,979; Shinyanga Manispaa 283,115, na Wilaya Shinyanga, miti 79,000.
 

 
 
 
 

Habari Kubwa