Uchomaji mkaa unavyoteketeza mikoko nchini

10Sep 2016
Moshi Lusonzo
Nipashe
Uchomaji mkaa unavyoteketeza mikoko nchini
  • *Nje ya nchi unaitwa dhahabu nyeusi

KUSHAMIRI kwa biashara ya mkaa unaotokana na miti aina ya mikoko ambao una soko kubwa nje ya nchi, kumesababisha kasi ya ukataji wa miti hiyo katika maeneo ya pwani ya Tanzania.

mikoko.

Eneo ambalo limeathirika zaidi na uvunaji haramu wa miti hiyo kwa ajili ya uchomaji mkaa ni Pemba Mnazi na Tundwi Songani jijini Dar es Salaam.

Katika uchunguzi uliofanywa na Nipashe, mkaa unaotokana na mikoko una soko kubwa katika visiwa vya Zanzibar, Comoro, Shelisheli na nchi za Uarabuni.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kila siku zaidi ya tani 20 za mkaa wa mikoko unavunwa katika eneo la msitu wa Shungu, Tundwi Songani, sawa na tani 600 kwa mwezi.

Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa Mtaa wa Songani, Abdulmalik Ally, alisema kiwango hicho ni sawa na idadi ya miti 20 inayokatwa kila siku, ambayo kila mmoja una uwezo wa kutoa mkaa wenye uzito wa kilo 1,000 (tani moja).

Ally ambaye baada ya kuingia madarakani alijaribu kupambana na hali hiyo, lakini alishindwa kupata mafanikio baada ya kutishiwa usalama wake na watu wanaojihusisha na biashara hiyo.

MKAA WA CHUMA
Mwenyekiti huyo alisema sehemu iliyokithiri kwa kukata miti ya mkaa ni fukwe ya mto Mbezi na Shungu.

Anasema eneo hilo hakuna ukaguzi wa mara kwa mara unaofanywa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na kusababisha watu wanaojihuisha na kazi hiyo kuwa na uhakika wa kufanya kazi kwa uhuru.

Anaeleza kwamba watu hao wanaweka kambi maalum ambazo kazi yao ni kukata miti na kuandaa matanuru ya kuchomea mkaa, huchukua siku tatu hadi tano kuwa tayari kwa matumizi ya kupikia.

Mmoja wa watu wanaofanya kazi hiyo, Salim Kawambwa, mkazi wa Morogoro, alisema wanachoma mkaa kutokana na ukubwa wa mahitaji la mfanyabiashara husika.

Alisema kiwango cha malipo wanapata kila mmoja kwa tanuru moja lenye uwezo wa kutoa magunia 10 ya mkaa yenye kilo 100 inaanzia Sh. 100,000 hadi Sh. 200,000.

Alisema malipo hayo yanakuwa tofauti na gharama zingine kama kununua chakula, mboga na mafuta ya taa, ambazo mteja anawajibika kutoa.

“Tunapopewa oda kutoka kwa wafanyabiashara tunaanza kuchukua nusu ya malipo na tunapomaliza wanamalizia na wao wanachukua mzigo wao,” alisema.

Hata hivyo, alisema zamani walikuwa wakiingia zaidi ya watu 10 kufanya shughuli hiyo, lakini kutokana na miti kupungua na kuongezeka kwa vyombo vya doria, wanaingia porini watu watano ambao wanafanya kazi zote.

“Pamoja na boti za doria kuja msituni mara kwa mara, inatufanya tuwe makini sana. Tunakwenda watu wachache kwa kuhofia kelele za ukataji wa miti au kuzungumza pale tunapokuwa kambini,” alisema Kawambwa.

Mtu mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Ngayonga, alisema kila wiki jahazi linafika maeneo hayo kwa ajili ya kuchukua mzigo na kusafirisha kwenda Zanzibar na kisha kusambazwa katika nchi zingine.

DHAHABU NYEUSI

Mwanamke mmoja ambaye anafanyabiashara hiyo, ambaye kutokana na sababu za kiusalama jina linahifadhiwa, alisema biashara hiyo ni nzuri kwa kuwa ina soka la uhakika.

Alisema gunia moja la kilo 100 linauzwa kati ya Sh. 100,000 hadi Sh. 150,000 kutokana na ubora na aina ya mkoko uliotumika.

“Kitu kisichojulikana ni kwamba mkaa wa mikoko ni sawa na dhahabu nyeusi kwa kupendwa nje ya nchi, hautumiki sana hapa nchini kwani unahitaji vyombo maalum vya kupikia. Tunauza sana Zanzibar, Comoro, Shelisheli na Uarabuni kutokana wao kuuhitaji sana,” alisema.

Akielezea namna ya usafirishaji wa bidhaa hiyo, alisema baada ya kupakiwa ndani ya jahazi, njia wanayotumia katika kukwepa kukamatwa ni kupita wanapita bahari kuu na kisha kutokea katika kisiwa cha Chumbi, kabla ya kuingia Zanzibar kwa ajili ya kufanya biashara.

Wakati huo wamiliki wa bidhaa hiyo wanasafiri kwa magari hadi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupanda boti hadi Zanzibar ambako huko wanasubiri mizigo yao.

Baada ya kuwasili bandari ya Zanzibar, kazi ya kupakua inafanyika na shehena inayotakiwa kwenda nje ya nchi inapakiwa katika meli za mizigo ambazo wakati huo zinakuwa zikisubiri bandarini.

Mfanyabiashara mwingine alisema mzigo unapofika kisiwani Unguja, hakuna wasiwasi wa kukamatwa kwa sababu hakuna sheria inayokataza usafirishaji na uuzaji wa mkaa ya miti hiyo.

Aidha, alisema mkaa wa mikoko hauharibiki haraka hata ukiloa maji wakati wa usafirishwaji wake, jambo ambalo hausababishi hasara.

Kwa mujibu wa mfanyabiashara huyo, kinachofanyika ni kuziba kwa mifuko maalumu sehemu zote ili kudhibiti usiweze kutawanyika kama jahazi likijaa maji.

Hata hivyo, imeelezwa nchi hizo inahitaji mikaa hiyo kwa wingi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kazi za kuokea mikate katika viwanda vidogovidogo.

Ofisa wa Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS), Florian Kaaye, alisema nishati hiyo inafananishwa makaa ya mawe kutokana na kuwa mgumu na una uwezo wa kupikia vyakula vingi kwa idadi ndogo ya mkaa.

Anasema kwa mahitaji ya watu wa kawaida hawawezi kumudu kwani wanaweza kuharibu vyombo vyao kwa kuyeyuka.

“Mkaa wa mawe una moto mkali huwezi kupikia kwa sufuria za kawaida, lazima upate chombo kigumu chenye kuhimili hali joto kali ndio maana biashara kubwa inakuwa nje ya nchi,” alisema.

Vyombo vinavyopendekezwa kupikia kwa kutumia mkaa wa mikoko ni vile vilivyotengenezwa kwa kuhimili moto wa gesi na umeme.

Mtaalam huyo anasema Watanzania wengi hawana utamaduni wa kutumia gesi wala umeme katika kupata nishati ya kupikia, hivyo hata vyombo vyao ni vile vilivyotengenezwa kwa bati lepesi.

Kaaye anakiri kwamba kama juhudi hazitachukuliwa kudhibiti ukataji wa miti na uchomaji wa mkaa, hali inaweza kuwa mbaya katika mufa mfupi unaokuja.

KUKAMATA NI VIGUMU
Ofisa Ugavi na Misitu wa Manispaa ya Temeke, Boniface Mgaya, alisema ni rahisi kuwakamata watu wanaokata miti na kuchoma mkaa, lakini si wafanyabiashara.

Alisema ni jambo jepesi kuubaini mkaa wa mikoko pale unapoingia sokoni kutokana na rangi yake kuwa tofauti. Hata hivyo, jambo hilo haliwezekani kwani bidhaa hiyo haipo katika soko la hapa nchini.

“Mkaa wa mikoko si mweusi kama tulivyozoea kuona, una rangi nyekundu kidogo, ukiulamba una ladha ya chumvichumvi ni rahisi kuujua hata unapopakiwa katika gari, lakini hutujakamata kwa sababu hauingii katika soko watu hawawezi kuununua,” alisema Mgaya.

Kwa mujibu wa Mgaya, juhudi zinafanyika kuendesha doria katika misitu mbalimbali katika eneo hilo na kuwakamata watu wote wanaojihusisha na kazi hiyo.

“Tumewakamata zaidi ya watu 50 kwa mwaka jana na kuwafikisha mahakamani. Pia tumeharibu makazi yao na matanuru yao,” alisisitiza ofisa huyo.

NEMC KUANZA KAMPENI
Akizungumzia suala hilo, Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Manchare Saguti, alisema suala hilo wanalijua na wameanza kampeni maalum ya kutokomeza uhalifu huo.

Alisema takwimu waliyonayo Tanzania inapoteza kila siku eka 10 hadi 20 kwa kukatwa miti, sawa na hekta 80,000 kwa mwaka.

“Jambo hili ni baya kwa ustawi wan chi yetu, lazima sasa kama Nemc tufanye kazi ya ziada kuhakikisha watu wanaacha kuvuna misitu ikiwamo mikoko kama chanzo cha nishati,” alisema.

Aisha alisema wameanzisha kampeni kubwa kwa kushirikiana na TFS katika kutoa elimu kwa Watanzania wafahamu uhifadhi wa mazingira ni jukumu la kila mtu.

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa, upande wake alisema suala hilo litafikia tamati pale Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni itakapoanza kazi yake ya kupanga upya mipango endelevu ya ardhi.

Alieleza kwamba awali ilikuwa shida kufika katika maeneo hayo ambayo yapo mbali, lakini baada ya mgawanyo na kuzaliwa wilaya hiyo mpya, itakuwa rahisi kwao kuyafikia.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, aliliambia gazeti hili kwamba serikali imeanza kudhibiti uvunaji haramu wa misitu kwa kufuta vibali vyote.

“Serikali imefuta vibali vyote vya uvunaji wa mbao na magogo, jambo hili linahusu sekta yote ya misitu ili tuanze kujipanga kuhakikisha raslimali yetu hii inanufaisha nchi,” alisema Maghembe.

Kabla ya kuchukua hatua hiyo, Profesa Maghembe, alipangua uongozi mzima wa TFS kwa kile alichokieleza ulishindwa kufanya majukumu yake.

Aliyekuwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa TFS, Gerald Kamwenda, aliondolewa katika nafasi yake hiyo, badala yake Waziri Maghembe alimteua Profesa Dos Santos Silayo kushika kiti hicho.

Aidha, Kamwenda na maofisa wengine 41 walihamishiwa kwenda kufanya kazi sehemu mbalimbali nchini.

Habari Kubwa