Uchumi China waporomoka  baada ya miaka 27

19Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Uchumi China waporomoka  baada ya miaka 27

KWA mara ya kwanza katika miaka 27 iliyopita, uchumi wa China umepungua kasi ya ukuaji wake katika robo ya pili ya mwaka.

Ukanda wa viwanda  wa Umoja wa Ulaya na China. PICHA:MTANDAO.

Kuanzia mwezi Mei mpaka Juni mwaka huu, uchumi wa taifa hilo kubwa duniani ulikuwa kwa asilimia 6.2 ikilinganishwa na mwaka mmoja uliopita. 

Matokeo hayo yanalingana na vile ilivyotarajiwa. Serikali ya China inajitahidi kuchochea ukuaji wa uchumi kwa mwaka huu kwa kupunguza kodi pamoja na kubana  matumizi. 

China pia ipo katikati ya vita vya kibiashara baina yake na Marekani ambavyo vimeumiza hali ya biashara na ukuaji wa uchumi. 

Data rasmi zilizotolewa na Ofisi ya Takwimu ya China zinaonyesha kuwa kasi ya ukuaji imeshuka kutoka asilimia 6.4 ya mwanzoni mwa mwaka. 

Rais wa Marekani Donald Trump, aliandika kupitia ukurasa wake wa twitter kuwa ushuru wa kibiashara kutoka Marekani "umeathiri pakubwa" uchumi wa China. 

Mamlaka za China zinasema takwimu hizo zinaonyesha hali ngumu ya kimazingira ndani na nje ya nchi. 

"Uchumi umekuwa katika ustawi wa kutegemewa katika nusu ya kwanza ya 2019, lakini kuna nguvu kubwa ya kwenda chini kadri siku zinavyosonga," inaeeleza Ofisi ya Takwimu ya nchi hiyo.

UCHAMBUZI

Andrew Walker, mwandishi wa biashara, anasema takwimu hizi zinaonyesha kwa namna gani jinsi ugomvi wa kibiashara baina ya China na Marekani ulivyokuwa na athari. Ukuaji umeshuka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na hali ambayo ingekuwapo kama kusingekuwa na ugomvi baina ya  mataifa hayo.

 Picha ya muda mrefu ni kuwa, uchumi wa China utaendelea kuwa imara japo utashuka kasi yake. 

Kasi ya ukuaji wa uchumi wa China katika miongo mitatu iliyopita mpaka kufikia mwaka 2010 ilikuwa ni asilimia 10. Lakini ilikuwa ni jambo la wazi miongoni mwa wachumi na hata baadhi ya viongozi waliozungumza nchini China walisema kuwa ukuaji huo usingelibaki hivyo milele. 

Lengo lilikuwa ni kuhakikisha uchumi hautegemei zaidi uwekezaji na biashara ya nje badala yake kukuza vipato na matumizi ya raia. Hatua, imepigwa katika eneo hilo, japo uwekezaji bado unachangia pakubwa uchumi wa Uchina. 

Kuna hatari zake hata hivyo, la zaidi ni madeni makubwa ya kampuni. Mamlaka zilichochea kampuni kukopa kwa kasi baada ya uchumi wa dunia kuyumba. Hiyo ilichangia pakubwa kuzuia anguko la ghafla la uchumi lakini ikaongeza hatari ya kifedha kwenye madeni. 

ATHARI DUNIANI  

Ukuaji wa uchumi ukiyumba nchini China unazalisha hofu kwengineko na mfumo mzima wa kidunia. 

Edward Moya, mtaalamu wa uchumi kutoka taasisi Oanda, anasema takwimu hizo za kiuchumi "zinaonyesha kuwa kuyumba kwa ukuaji wa uchumi wa China ni suala endelevu na masoko yategemee fedha zaidi za mikopo kutoka Benki Kuu ya China ili kuchochea ukuaji wa uchumi." 

Mgogoro wa kiuchumi baina ya China na Marekani pia ni suala lengine la kuliangalia na athari zake zipo wazi sasa. 

"Vita ya kibiashara ina athari kubwa sana kwenye uchumi wa China, na hakuna suluhu yeyote inayotarajiwa basi tutarajie kuona uchumi ukishuka zaidi," anasema. 

Japo pande zote mbili zilikubaliana kurudi kwenye meza ya mazungumzo walipokutana katika mkutano wa G20 nchini Japani, wametwangana ushuru katika bidhaa mbalimbali na kuumiza uchumi wa dunia.

AFRIKA IKOJE?

Afrika ni bara ambalo linategemea pakubwa biashara na Uchina. 

Ni nchi moja tu ambayo haina ushirikiano wa kibiashara na China ambayo ni eSwatini au zamani Ufalme wa Swaziland. 

China ndiyo taifa lenye ushawishi mkubwa kibiashara Afrika baada ya kuipiku Marekani zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Kwa ujumla thamani ya biashara baina ya China na Afrika kwa mwaka 2017 ilifikia kiasi cha Dola bilioni 170 kutoka Dola bilioni 10 mwaka 2000.

Ni dhahiri kuwa iwapo hali ya kusuasua kwa uchumi nchini China itaendelea basi Afrika nayo itaathirika pakubwa. BBC