UDSM wajitosa Tanzania ya Viwanda kupitia utafiti

19May 2017
Gwamaka Alipipi
Nipashe
UDSM wajitosa Tanzania ya Viwanda kupitia utafiti

KATIKA kuinua sekta ya kilimo ili kumuwezesha mkulima alete matokeo chanya katika kusaidia Tanzania ifikie karne ya viwanda ifikapo mwaka 2025-

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Ndaki (College) ya Sayansi Asilia na Sayansi Timilifu (CoNAS), imebuni teknolojia pandikizi ya mbegu ya magimbi na viazi vikuu katika maabara.

Teknolojia hiyo iliyofanyiwa utafiti UDSM, inayomuwezesha mkulima kupata mbegu za magimbi katika kipindi kifupi, tofauti na awali upatikanaji wake ulichukua muda mrefu, huku katika kila shina ikipatikana mbegu moja.

Akifafanua kuhusu utafiti huo na teknolojia hiyo kwenye Maonyesho ya Utafiti ya UDSM, iliyokuwa na kaulimbiu: “Utafiti kwa Tanzania ya Viwanda na Uchumi wa Kati,” Mhadhiri na Mtafiti Mkuu wa CoNAS, Dk. Gladness Temu, ana maelezo kuhusu mradi huo.

Anasema kuwa umefadhiliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia na kwamba wanashughulika na matatizo ya mkulima katika uzalishaji wa viazi vikuu na magimbi.

Dk. Temu anasema kuwa mazao hayo yana matatizo katika upatikanaji wa mbegu zake, kwa kuwa zimekosa mbegu halisi na mkulima analazimika kuharibu baadhi ya magimbi au viazi vikuu, wakati wa uvunaji, ili apate mbegu za kupanda tena.

“Tatizo kubwa la wakulima ni kupata mbegu safi. Mkulima anatumia shina moja kupata mbegu moja ya magimbi. Upande mmoja anakula na mwingine anapanda, sasa kwa kutumia teknolojia hii, itamkomboa mkulima,” anasema Dk. Temu.

Anafafanua kwamba kutokana na hali hiyo ndipo CoNAS iligundua teknolojia inayoweza kuzalisha mimea mingi ya magimbi na viazi vikuu katika maabara.

WANAVYOONGEZA UZALISHAJI

Dk. Temu anasema kwa kutumia teknolojia ya maabara, wanaukata mmea wa magimbi na kisha wanaupandikiza katika maabara kwa hatua hadi kufikia
uzalishaji wa mbegu zenye mizizi, tayari kwa kuwapeleka wakulima.

Mhadhiri huyo anasema, huwa wanatumia muda kati ya mwezi mmoja na miwili kuzitayarisha kwa ajili ya kutumiwa na mkulima.

Anasema kupitia teknolojia hiyo ya CoNAS, uzalishaji wa mbegu maabara huzalisha mbegu zaidi ya 500 katika kila miezi miwili, lengo ni kumsaidia mkulima azalishe mazao mengi ambayo yatasaidia uzalishaji viwandani.

“Mbegu hizo ni bora na hazina magonjwa kama vile minyoo na hadi sasa tumeshafanya majaribio katika mashamba ya utafiti yaliyopo Kibaha, Mkuranga, Unguja, Kibaha na Kibiti,” anasema Dk. Temu.

KUELEKEA VIWANDA

Wakati CoNAS ikiibua teknolojia hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango anasema serikali imeweka mkakati wa kutenga asilimia moja ya fedha za bajeti kuu kila mwaka, ili kuwawezesha watafiti wa kilimo na viwanda nchini kufanya kazi zaidi.

Akifungua maonyesho hayo, Dk. Mpango anasema nchi zote zilizoendelea zina uhusiano wa karibu kati ya utafiti wa Ukuaji Uchumi, Maendeleo ya Viwanda, pamoja na Maendeleo ya Teknolojia.

Anasema ili kufanikisha hilo, kila mwaka serikali katika bajeti kuu inatenga asilimia moja ya bajeti, kusaidia utafiti unaotarajiwa kukuza uzalishaji viwandani, pia kuboresha maendeleo ya Watanzania.

“Kama hufanyi utafiti, huwezi kuendeleza viwanda vyako. Kwa mfano, ukifanya utafiti katika zao la pamba, unaweza kutengeneza aina ya mbegu ya pamba ambayo haishambuliwi na wadudu au kuzalisha pamba itakayotumika viwandani yenye nyuzi nzuri zaidi. Vinginevyo, bila ya kufanya utafiti, utazalisha pamba mbovu,” anasisitiza Dk. Mpango.

Anakumbusha kwamba, ni lazima nchi zihusishe maendeleo kupitia utafiti wa viwanda na maendeleo yake, pia masoko.

Dk. Mpango anasema serikali iko tayari kupokea matokeo ya tafiti zilizowasilishwa katika maonyesho hayo, ambayo ya sasa ni mara ya tatu. Yalianza mwaka 2014.

Waziri anasema, hivi sasa Tanzania inasafiri kuelekea kwenye Uchumi wa Viwanda na kwamba taarifa iliyotolewa na Benki ya Dunia (WB) katika taarifa yake ya Aprili 17 mwaka huu, ilieleza Tanzania kuwa miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi, Afrika.

Dk. Mpango anasema hivi sasa pato la taifa linakua kwa asilimia saba, huku sekta ya usafiri ikiongoza kwa ukuaji ambao ni wastani wa asilimia 16.9.

Ripoti hiyo inataja sekta inayofuatia kuwa ni madini ambayo ni asilimia 15.6; Mawasiliano asilimia 13.4; Umeme asilimia 8.3; na uzalishaji asilimia saba.

WENYE CHUO WANENA

Naibu Makamu Mkuu wa UDSM (Utafiti), Profesa Cuthbert Kimambo anasema kuwa UDSM imeweka mkazo katika kufanya utafiti na ubunifu, kwa ajili ya maendeleo ya viwanda nchini Tanzania.

Anasema katika Wiki ya Utafiti inayoadhimishwa UDSM kila mwaka, lengo kuu ni kuimarisha tafiti za wanachuo na miradi yao ya kitaaluma, pia kazi za kibunifu.

“Inafahamika wazi kuwa utafiti, maendeleo na ugunduzi vinahitaji Fedha. UDSM hatuna uwezo wa kifedha katika kufanikisha hayo, lakini kwa msaada wa serikali na taasisi za sekta binafsi, zinaweza kutusaidia kufanikisha hili,“ anasema Profesa Kimambo.

Mkurugenzi wa Utafiti na Uchapishaji wa UDSM, Profesa Shukrani Mmanya, anasema katika maonyesho hayo kuwa, mbali na utafiti, pia kuna miradi iliyoandaliwa na wanafunzi na walimu wa UDSM.

Miongoni mwa miradi hiyo kwa mujibu wa Profesa Kimambo, ni ya ufugaji samaki, kilimo na masuala ya teknolojia.

Naye anaendeleza hoja kwamba UDSM inaiunga mkono serikali ya Awamu ya Tano katika kaulimbiu ya ‘Tanzania ya Viwanda Inawezekana.”

Ni jambo linalofanyika kupitia idara mbalimbali zilizopo chuoni hapo, mojawapo ni kwa kuanzisha masomo yanayohusu mafuta na gesi ambayo sasa yameshaanza kuchimbwa nchini.

Naibu Makamu Mkuu wa UDSM anayehusika na taaluma, Profesa Frolence Luoga, anasema maonyesho yamewakutanisha wataalamu mbalimbali waliowasilisha tafiti zao katika sekta tofauti.

Anasema idara inayohusika na utafiti imejidhatiti kuendeleza tafiti nyingi, ili kuzisaidia sekta muhimu zinazoendeleza viwanda, ikiwamo kilimo, madini na mafuta.

Msomi huyo anahimiza kwamba hakuna nchi duniani inayopata maendeleo, pasipo kufanya utafiti na mipango, ndiyo inafuata, ikielekezwa na utafiti.

Habari Kubwa