Uhondo mbio za Tigo Kili Half Marathon

21Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Uhondo mbio za Tigo Kili Half Marathon

NI zaidi ya faida kwa wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro, hususan mji wa Moshi na vitongoji vyake, kwa kuwa Machi 3, mwaka huu itakuwa ni fursa ya kipekee kunufaika kupitia mbio fupi za Tigo Kili Half Marathon wakati zitakapotimua vumbi mkoani hapo.

Meneja wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Lilian Mwalongo, akizungumzia kuhusu udhamini wa Tigo katika mbio maarufu za Tigo Kili Half Marathon, zitakazofanyika mjini Moshi Machi 3, mwaka huu. MPIGAPICHA WETU

Mbio hizo za kilometa 21, mwaka huu zinatarajiwa kuleta fursa nyingi kwenye sekta ya utalii na kukuza vipato vya wananchi wa mjini Moshi.

Ikumbukwe kwa mwaka wa nne sasa, Tigo inakutanisha Watanzania zaidi ya 5,000 mjini Moshi kushiriki mbio hizo ambazo zimekuwa zikijizolea umaarufu mkubwa ulimwenguni mwaka hadi mwaka.

Meneja wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Lilian Mwalongo, akizungumza kwenye hafla ya kutangaza kuanza kwa usajili mjini Moshi juzi, alisema kupitia udhamini huo pamoja na mambo mengine utasaidia kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii.

“Kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, mbio hizi zitaongeza idadi ya wageni watakaotembelea mji wa Moshi na vivutio vya utalii vilivyopo. Tigo Kili Half Marathon inalenga kukuza vipato vya wananchi.

“Hapa tutaibua fursa mbalimbali za hoteli, wauza vinywaji, chakula, kumbi za starehe, vocha za simu, sekta ya usafirishaji; mabasi, daladala, bodaboda, teksi na biashara nyingine zitafaidika kutokana na uwepo wa mbio hizi,” anasema Mwalongo.

Meneja huyo anaongeza kuwa, kampuni ya Tigo inadhamini mbio hizo kama njia mojawapo ya kuchangia juhudi za serikali kuinua viwango vya michezo na kujenga afya bora za Watanzania kupitia ushiriki wao katika michezo.

“Katika eneo hili tunatarajia kuwa na wanamichezo wa kimataifa, kitaifa, wapenzi wa mchezo wa riadha na pia wanafamilia watakaoshiriki katika mbio hizi za Tigo Kili Half Marathon,” anasema Mwalongo.

Anazitaja zawadi za fedha taslimu kwa washindi 10 wa kwanza, tuzo za medali, vyeti vya ushiriki na fulana za kumbukumbu kwa washiriki wa kwanza 5,500 watakaomaliza mbio hizo.

Meneja huyo wa Kanda alisema Tigo inawahakikishia washiriki wa mbio hizo kupata mawasiliano ya uhakika kwa kuwa tayari kampuni hiyo kwa kutambua, imepanua huduma ya Tigo 4G kufikia miji zaidi ya 22 nchini ukiwamo mji wa Moshi.

“Kupitia mtandao wetu wa 4G+, washiriki wote wa Tigo Kili Half Marathon watakuwa na fursa ya kutuma picha, video na kumbukumbu zao kupitia mtandao wenye kasi ya juu,” anasema Mwalongo.

Akizindua mchakato wa kujisajili, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira,  alisema Tigo Kili Half Marathon huleta wageni kuanzia 12,000 hadi 15,000 wanaoutembelea mji wa Moshi.

“Hii ni njia muhimu ya kuimarisha utalii na uwekezaji wa kibiashara unaofanywa na wananchi wetu,” anasema RC Mghwira.

Naye Mratibu wa mbio hizo, John Bayo, alisema mbio za Tigo Kili Half Marathon zimekuwa na mvuto wa aina yake kutokana na kushirikisha watu zaidi 5,000.

“Niwaombe Watanzania waanze kujisajili huko huko walipo kwa kutumia Tigo Pesa wanamaliza kila kitu kwa kubonyeza *149*20# itawaletea maelezo yote.

“Mwaka huu usajili umekuwa tofauti, miaka iliyopita ulifanyika mpaka siku ya Jumamosi, hatua iliyosababisha kukosekana namba kwa baadhi ya washiriki.

“Kwa mwaka huu tumerahisisha zaidi mfumo wa kujisajili, Mtanzania mwenye kushiriki atalipia kwa mtandao wa Tigo Pesa ili kufanya usajili wake.

“Tigo wataturahisishia kujua mahitaji kamili ya washiriki wa Tigo Kili Half Marathon mapema, usajili utafungwa Februari 7, mwaka huu ili kuandaa namba na fulana za washiriki.

“Tunashukuru washiriki wengi wameanza kujisajili kupitia Tigo Pesa na tunaomba waendelee kujitokeza. Utaratibu wa kufunga mapema usajili unafanywa duniani kote kwenye mbio za kimataifa ili kurahisisha kukamilisha maandalizi yote," alisema Bayo na kufafanua zaidi:

“Usajili kwa njia ya Tigo Pesa ulianza Oktoba Mosi kwa bei ya punguzo yaani Sh. 12,000 mpaka Desemba 7, mwaka jana. Kuanzia Desemba 7 mpaka Januari 7 ilikuwa ni Sh. 15,000 na baada ya hapo hadi kufikia Februari 7, mwaka huu Kilometa 21 itakuwa ni Sh. 20,000.

“Licha ya burudani, mbio hizi zitakupa wakati mzuri kuepuka magonjwa kama sukari, shinikizo la damu, wengi wanashauriwa kufanya mazoezi niombe waje kushiriki Tigo Kili Half Marathon wapunguze mafuta na sukari mwilini.”

Aidha, Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya, amewapongeza Tigo kwa kudhamini Tigo Kili Half Marathon kwa sababu zimeufanya mji wa Moshi na Kilimanjaro kupaa kimataifa.

“Kilometa 21 zimekuwa na mwitiko mkubwa wa wageni pamoja wazawa, ni dhahiri si wote wanaokuja kukimbia bali wengine huja kwa ajili ya kujiburudisha.

“Ujio wa watu zaidi ya 5,000 ni neema kwa mji wetu na mkoa kwa sababu wafanyabiashara watauza bidhaa, hoteli zitapokea na kulaza wageni maeneo yote yatafanya biashara,” alisema Meya Mboya na kuongeza:

“Tigo wamefanya jambo jema, niwapongeze, lakini niwaombe waongeze kitu kingine kipya cha tofauti mfano kuwapo mbio za wazee kuanzia miaka 60 kwenda juu.

“Hao wawe na fungu lao la kukimbia, hii italeta kitu kingine kipya kitakachohamasisha zaidi watu kujitokeza. Kwa upande wangu nitajitahidi kukimbia Tigo Kili Half Marathon.”

Katika hatua nyingine kwenye uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro (KAA), Listone Metacha, anasema kwa mbio za Tigo Kili Half Marathon tegemeo la Watanzania kushinda ni kubwa.

“Vijana wanaendelea na mazoezi mbalimbali, lakini pia wameshiriki mashindano tofauti ndani na nje ya nchi, nina hakika wanariadha wetu kina [Emanuel] Giniki, Gabriel [Geay], Fabian Nelson na wachezaji wengine watafanya vizuri Kilometa 21.

“Changamoto kubwa iliyopo ni ufadhili, niwaombe Tigo wakiweza kutoa msaada wa kuwaweka vijana wakimbiaji wetu kambini, hakika tunaweza kuleta matunda wanayoyatarajia Watanzania katika riadha,” anasema Metacha.

Habari Kubwa