Ujenzi wa miundombinu wanyanyua taaluma Mlowa, Lyamkena Njombe

14May 2019
Elizaberth Zaya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ujenzi wa miundombinu wanyanyua taaluma Mlowa, Lyamkena Njombe
  • • Mchango wa TASAF wazisaidia sekondari hizo

UPUNGUFU wa vyumba vya madarasa pamoja na mabweni ya kulala wanafunzi ni miongoni mwa changamoto zinazozikabili shule nyingi nchini.

Baadhi ya nyumba za walimu zilizojengwa kwa msaada wa TASAF, Shule ya Sekondari Mlowa.PICHA: ELIZABETH ZAYA

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kutatua changamoto hizo kwa mustakhabali mzima wa ubora wa elimu inayotolewa kwa watoto wa Kitanzania na hivyo ustawi wa jumla wa taifa.

Kama ilivyo kwa mikoa mingine, mkoa wa Njombe una baadhi ya shule zinazokabiliwa na changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa, ukosefu wa mabweni na nyumba za walimu, hivyo kuathiri wanafunzi na walimu kwa kiasi kikubwa.

Shule za Sekondari za Mlowa na Lyamkena zilizopo katika Kata ya Mlowa, Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe ni miongoni mwa shule zinazokabiliwa na changamoto hizo pia.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mlowa, Raymond Kyando, anasema shule hiyo ilianzishwa mwaka 2014 ikiwa na wanafunzi 52 na madarasa matatu.

Hata hivyo, anasema ilipofika mwaka 2015 walibaini maendeleo ya wanafunzi kitaaluma hayakuwa ya kuridhisha, mojawapo ya sababu ikiwa ni baadhi yao kuishi katika makazi ya kupanga nje ya shule yaliyokuwa mabovu.

 “Tulilazimika kufanya ukaguzi katika makazi yao mwaka 2015 kwa kushirikiana na kamati ya shule, ndipo tuligundua wana changamoto kubwa ya usomaji,” anasema na kuongeza:

“Makazi yao hayakuwa rafiki kwa maana mazingira waliyokuwa wakiishi kwa usomaji na tulipata kesi ya watoto wanne kupata ujauzito.”

Kyando anasema walichukua hatua ya kuwashirikisha wazazi wa wanafunzi wakiwa kidato cha pili na wakakubaliana kuanzisha kambi ya kuishi wanafunzi.

“Walikuwa wanaishi shuleni wakilala katika madarasa, huku wakisimamiwa na viongozi wa shule,” anasema na kuongeza:

“Mwaka huo tulipata matokeo mazuri ya ufaulu na kesi za utoro zilipungua tofauti na ilivyokuwa wakati wanafunzi wakitokea nyumbani.”

HOSTELI

Anasema mwaka 2016 kupitia bodi ya shule walianzisha hoja ya kufanya harambee ya ujenzi wa hosteli za wanafunzi baada ya kugundua kwamba wakiwa katika mazingira ya shule, muda mwingi walikuwa wanafanya vizuri kitaaluma.

Mwalimu Mkuu anasema walifanikiwa kufanya harambee na kupata kiasi cha fedha ambacho walianza kuchimba msingi kwa ajili ya ujenzi wa mabweni hayo.

Hata hivyo, anasema waliishia njiani kwa sababu wazazi hawakuchangia tena pesa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi waliouanzisha.

TASAF

Kyando anabainisha kuwa mwaka 2016 kuelekea 2017, TASAF iliwatembelea na kujionea mazingira ya miundombinu ya shule hiyo yasivyoridhisha.

Anasema kwa maombi ya uongozi wa shule pamoja na wazazi, TASAF ilikubali kuwasaidia kuwajengea madarasa, nyumba za walimu, mabweni na vyoo kupitia miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Anabainisha mwaka huo huo wa 2017 ndipo TASAF ilipoanza ujenzi huo na kuukamilisha mwaka 2018.

“Kufikia Oktoba Mosi 2018, wanafunzi wa kidato cha nne walianza kutumia hosteli hizo, kwa sababu walikuwa wanajiandaa na mitihani ya Taifa,” anasema na kuongeza:

“Ilikuwa msaada mkubwa kwetu kwani ulitusaidia kuwaweka wanafunzi katika mazingira salama hasa katika kipindi hicho muhimu cha mitihani ya taifa kwao.”

Kyando anasema baada ya kidato cha nne kumaliza mitihani, waliwahamishia wanafunzi wa vidato vingine katika hosteli hizo.

“Kwa hiyo tangu wanafunzi wahamie hosteli, hatuna kesi za utoro wala mimba… hivyo hosteli kwetu sisi ni msaada mkubwa wa kujenga mazingira bora ya kitaaluma kwa kuzingatia mazingira wanayotoka wanafunzi,” anasema.

NYUMBA ZA WALIMU

Anabainisha mbali na changamoto ya hosteli, pia shule hiyo ilikuwa na changamoto ya uhaba wa nyumba za walimu na kwamba TASAF imesaidia kujenga nyumba tatu za walimu pamoja na jengo la utawala na ofisi za walimu.

“Nimezungumzia hosteli kwa upande wa wanafunzi, lakini pia katika hii shule kuna jumla ya walimu 20, wa kiume 14 na wa kike sita…hakuna nyumba shuleni, tunapanga mtaani tena ni mbali na maeneo ya shule, zaidi ya kilomita 15,” anasema na kuongeza:

“Kwa hiyo tulipokaa katika vikao vya wazazi, tuliona kwamba kunahitajika nyumba za walimu lakini pia na jengo la utawala kwa sababu tulikuwa tunatumia darasa kwa ajili ya ofisi ya walimu… kwa hiyo tuliwaomba pia TASAF wasaidie kwa hili na wakakubali.”

Kyando anasema kuna uhitaji wa nyumba 20 za walimu katika shule hiyo na kwamba katika kipindi ambacho wanasubiri kupata nyumba zote zinazohitajika, watazitumia vizuri walizojengewa na TASAF.

“Kwa sababu nyumba ziko tatu na kila moja ikiwa na vyumba vitatu vya kulala, hivyo nimepanga nyumba moja kuweka walimu ambao hawajaoa ili walau kila mmoja apate chumba kimoja cha kulala,” anasema na kuongeza:

“Na nyumba moja nzima moja miongoni mwa hizo, nitaweka mwalimu mmoja mwenye familia…kwa hali hiyo walimu kama saba watakuwa wamepata mahali pa kukaa… nitabaki nahangaikia walimu waliobaki.” anasema.

TASAF

Kwa upande wake, Ofisa Mfuatiliaji wa Miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Mji wa Makambako na Wanging`ombe, Edwin Mlowe, anasema mbali na kuwa na miradi inayolenga kaya maskini, pia wamekuwa wakiboresha miundombinu ya shule.

“Kwa hiyo tukipata fursa ya kifedha huwa tunajenga vyumba vya madarasa, majengo ya utawala, mabweni ya wanafunzi pamoja na kuboresha vyoo,” anasema.

Mlowe anabainisha kuwa majengo yanayojengwa na TASAF huwekewa kila kitu cha ndani ikiwamo samani, mfumo wa maji na umeme katika kila darasa.

SEKONDARI YA LYAMKANA

Mbali na shule ya Sekondari Mlowa, Mlowe anasema pia TASAF wamejenga madarasa mawili, ofisi ya walimu pamoja na matundu nane ya vyoo kwenye Shule ya Sekondari ya Lyamkana.

Mkuu wa Shule hiyo, Sebastian Simtitu, anasema kwa kipindi kirefu wamekuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa na kwamba wamekuwa wakishirikisha kamati za shule mara kwa mara kutafuta mbinu za kutatua changamoto hiyo.

“Tumekaa vikao vingi na wazazi pamoja na kamati ya shule kwa ajili ya kutafuta mbinu mbadala za kutatua changamoto hii… tuliendesha harambee na kufanikiwa kupata pesa ambayo ilituwezesha kujenga madarasa mawili, lakini hayakuwa yakitosheleza,” anasema na kuongeza:

 “Mwaka 2016 tulitembelewa na TASAF na tukawaomba watusaidie kujenga madarasa na baada ya tathmini yao  waligundua kweli tulikuwa na uhitaji…mbali na madarasa,  wametujengea ofisi ya walimu na vyoo, wakiweka kila kitu ndani yake.”

Habari Kubwa