Ujue mkaa mpya ulioingia sokoni kurithi nishati kuni na mkaa wake

25Feb 2021
Beatrice Philemon
Dar es Salaam
Nipashe
Ujue mkaa mpya ulioingia sokoni kurithi nishati kuni na mkaa wake

KIHISTORIA, sehemu kubwa ya vyanzo vya nishati vimejikita katika mkaa na kuni, Ni hali inayochangia kuharibu misitu na mimea kwa ujumla.

Takwimu kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), zinaonyesha mahitaji ya nishati ya mkaa nchini yanafikia tani milioni mbili hadi tatu kwa mwaka na ili kuzalisha tani moja ya mkaa, zinahitajika mita za ujazo 10 hadi 12 za miti.

Utafiti wa TFS unaonyesha jiji la Dar es Salaam peke yake, kunaingizwa zaidi ya magunia 500,000 ya mkaa kila mwezi, ikiwa ni kiashiria cha uharibifu wa misitu.

Ni hali inayoshinikiza haja ya mageuzi makubwa  kukabili athari dhidi ya vyanzo vya mimea, kwa kuhamia matumizi ya nishati mpya gesi na teknolojia mkaa mbadala, hata kuokoa mazingira, pia nafuu kiuchumi kwa watumiaji.

NISHATI MPYA

Hivi sasa kuna teknolojia bora ya nishati ya kupika kupitia mabaki ya misitu na taka za kilimo kuzalisha mkaa mbadala maarufu, ikiwamo majiko sanifu.

Vifaa tajwa ni kuandaa tofali ndogo zitokanayo na kukandamizwa taka za shamba, misitu au viwandani na kutumika kama chanzo cha nishati.

Hapo kuna taka kama randa za mbao, vumbi la mkaa, pumba za mpunga, vipande vya mbao na mashudu.

Meneja, Mradi wa Mashujaa wa Mkaa Mbadala, kutoka Taasisi ya Uongozi na Maendeleo ya Ujasilimali (IMED), Rotildis Massawe, anaiambia Nipashe, teknolojia hizo zinatumika kupunguza matumizi ya mkaa jijini Dar es Salaam.

Kutumia mkaa wa kawaida, maana yake ni kukaribisha ukataji miti katika maeneo mbalimbali, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, pia ni elimu kwa wanafunzi.

Mdau, kampuni ya Space Engineering katika jitihada za kupunguza utumiaji kaa, imeanzisha mpango maalumu wa kutoa majiko sanifu bure kwa washirika kama Mama Lishe na wakaanga chipsi wa Dar es Salaam, sharti watatakiwa kununua mkaa mbadala kwao.

Pia, inasema imejikita kuhudumia wenye kipato cha chini na kati katika teknolojia ya mkaa mbadala, rai ikienda mbali vyuoni, shule za bweni, hospitali, kambi za jeshi, ili wakabiliane na mabadiliko ya tabianchi.

Hadi sasa, imeshawekeza Sh. milioni 650 kwa ajili ya uzalishaji mkaa mbadala, majiko sanifu na huduma za usafiri na Massawe anasema, kuna jumla ya tani 3398 za mkaa zilizozalishwa kutokana na mabaki ya misitu, taka za kilimo.

Pia, kuna majiko sanifu 650 yaliyokwishatengenezwa na kusambazwa bure jijini Dar es Salaam, katika yake 450 imesambazwa kwenye kantini za Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Maji na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) katika hosteli za JPM na DUCE, kote pia wanasambaza mkaa.

Anataja kwingine, ni katika migahawa saba ya UDSM, Chuo Kikuu Ardhi na Chuo cha Maji, wanatumia mkaa mbadala, baada kupatiwa majiko sanifu bure.

Massawe anasema, ni uamuzi uliofikiwa baada ya kubaini jiji la Dar es Salaam, lina watumiaji wakubwa wa nishati mkaa wa kupikia kiwango cha asilimia 70, inayobeba maana ya kubana matumizi ya nishati nyingine na hasa mkaa wa kuni, uliotawala awali, kwa hiyo una manufaa kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa wa vyakula,

Pia, jitihada mbalimbali za kupambana na matumizi ya kuni na mkaa mwaka 2018 kampuni hiyo ilishiriki shindano liitwalo ‘Mashujaa wa Mkaa Mbadala’ iliyojumuisha kampuni 92 na Space Engineering iliibuka mshindi, ikijitwalia Sh. milioni 200 pamoja na ushauri kutoka taasisi ya IMED.

Akirejea shindano, lilikuwa la kueneza teknolojia bora ya nishati ya kupika kwa mabaki ya misitu na taka za kilimo, kuzalisha mkaa na kukuza nishati mbadala kwenye mazingira endelevu.

“Tunaamini teknolojia hii ya kutengeneza mkaa taka na majiko sanifu itakapoboreshwa itaharakisha maendeleo nchini hasa katika matumizi ya nishati majumbani na kibiashara,” anasema.

UHAMASISHAJI ULIVYO

Shindano hilo liliendeshwa na kampuni ya Shell Exploration and Production Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), lengo ni kuhamasisha utunzaji mazingira kitaifa.

“Fedha hizo zilitolewa ili kutumia kuzalisha kwa wingi mkaa mbadala, kupunguza mkaa unaotokana na kukata miti, kukuza ubunifu wa nishati mbadala na mazingira ya biashara, kuanzia vifaa vya kuendesha biashara zao, eneo la biashara, wafanyakazi na taasisi ya IMED kutoa mafunzo kwa wamiliki na wafanyakazi,” anasema.

MTIHANI ULIOPO

“Changamoto tunazokutana nazo sokoni ni nyingi, ila tunajitahidi kupambana nazo kama gesi, kuni, mkaa wa kuni na kadhalika,”anasema Massawe na kufafanua:

“Tunapambana nao kwa kuongeza ubora wa bidhaa yetu, kuwajali wateja, ikiwa ni pamoja na kuwatembelea mara kwa mara kujua kama kuna matatizo na kufanya huduma kwenye majiko yao. Pia tunajitahidi kuhakikisha wateja wanapata bidhaa yetu kwa wakati.”

Kwa mujibu wa makakati wao, hivi sasa wahamasishaji hao wanalenga kuongeza uzalishaji mara tatu ya sasa, yaani kutoka tani 4.5 kwa siku hadi tani 13.5 na kuongeza majiko kutoka 450 hadi 1500 kwa mwaka.

Pia, kutazalishwa majiko madogo majumbani kutoka mapya kufikia idadi 1000 kwa mwezi na huduma za kunadi bidhaa hizo.

FAIDA ZILIZOKO

Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi ya IMED, Dk. Donath Olomi, anasema mkaa mbadala hutofautiani mwonekano na umbo kulingana na taka zilizotumika kutengeneza na jinsi ilivyotengenezwa.

“Mkaa huu una faida nyingi ukilinganisha na mkaa wa kawaida, kwa sababu ina nishati joto kubwa  kuliko kuni au mkaa wa kawaida na huwaka kwa muda mrefu,”akifafanua kuwa, hauna moshi wala vumbi jingi, hali inayolinda mazingira.

Nishati inapaswa kutumia kijiti kikavu, mafuta ya taa inayochanganywa na mkaa wa kawaida, ili uwahi kuwaka.

Wakati wa mapishi, mtu unapaswa kutumia jiko lenye mlango wa hewa ulio wazi na kuwekewa kifaa ‘brikweti’ na sufuria lake halizimiki.

Kifaa hicho kinawekwa juu ya chombo cha bati na kinabebwa taratibu kuzuia kunyofoka kufikia ngazi ya jivu, wakati wa kubeba.

Mbali na hilo, mtu hapaswi kuvuruga wala kupondaponda ‘brikweti’ wakati wa kupika, bali atumie majivu kama nishati, kwa maana linatoa joto jingi.

Pia, kunaelezwa haja ya busara kutumiwa majivu kama mbolea au kifusi cha kujaza vibonde jirani, mahali mtu anakopika. Kitaalamu, inashauriwa, mtu anatakiwa kupangilia mapishi vizuri, katika vyakula vinavyochukua muda mrefu.

“Funika ‘brikweti’ inayowaka kwa majivu ili isichomeke haraka, uweze kutumia tena baadae,” anasema, na kuongeza wanaopika mlo kama wali au pilau, waweke bati juu ya mfuniko wa sufuria kuukausha, pia asimwage maji ovyo wakati wa kupika.

Hadi sasa watengenezaji maarufu wanapatikana Mafinga, Iringa, Tabora na Kigoma na Dar es Salaam.

Habari Kubwa