Ujue mradi uliomaliza migogoro ardhi sugu iliyoshindikana vijijini

25Nov 2021
Christina Haule
Lindi
Nipashe
Ujue mradi uliomaliza migogoro ardhi sugu iliyoshindikana vijijini
  • Kilichogoma miaka 30, kimewezekana wiki

MRADI wa Kuhifadhi Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endelevu ya Mazao ya Misitu Tanzania (Coforest), umeonyesha ishara ya mafanikio kwa kutatua migogoro ya mipaka iliyodumu kati ya miaka mitano hadi 30 kwenye vijiji vitatu kati ya saba vilivyopo chini yake.

Elida Fundi, Ofisa Sera kutoka MJUMITA akimsikiliza Diwani wa Kata ya Mlembwe, Mohamed Hadid, kwenye msitu wa Hokororo, kijijini Nandimba, Wilaya ya Liwale. PICHA: CHRISTINA HAULE.

Coforest inaendeshwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) katika wilaya za Morogoro, Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro, Liwale, Ruangwa na Nachingwea mkoani Lindi, pia Kilolo ya mkoa Iringa.

Ofisa Mradi kutoka TFCG, Peter Ibrahim, anasema mashirika hayo kwa kushirikiana na wataalamu wa kiserikali ngazi za wilaya, wametatua migogoro iliyodumu muda mrefu katika vijiji vya mradi kwenye wilaya tatu, zikiwamo Ruangwa na Liwale mkoani Lindi.

Anaitaja migogoro ya mipaka ambayo imetatuliwa ni baina ya vijiji Malolo na Ng’alu wilayani Ruangwa, Mkoa wa Lindi, huku simulizi nyingine inaangukia kijiji cha Nambinda, kilichokuwa na historia yake ya mgogoro wilayani Liwale, Lindi tangu mwaka 2009, pale kilipozaliwa kutoka kijiji Mama Mlembwe.

Mgogoro mwingine wilayani Nachingwea ni kati ya vijiji Chimbendenga na Mbondo, ambao unaendelea kushughulikiwa kwa kushirikiana na mamlaka ya wilaya.

Aidha, anataja mgogoro wa kijiji Matuli na Diguzi wilayani Morogoro, uliodumu miaka 30 nao umekwisha kwa sasa.             
SIRI YA MGOGORO

Ibrahim anasimulia mzizi wa mgogoro vijijini Ng’alu na Malolo uliodumu miaka mitano, walitumia mfumo udadisi wa chimbuko lake na kubaini tafsiri ya ramani kwenye vijiji vyote na uhalisia wa mazingira wanayoishi jamii, ndivyo viliwachanganya.

Anasema katika utatuzi huo, pia wameangalia uhusiano wa vijiji na undugu uliopo kati ya vijiji hivyo viwili, wakabaini mgogoro utaleta mgongano na kuwakosanisha kindugu pande hizo.

Ibrahimu anaeleza wamebaini mfumo wa utawala na tafsiri ya ramani kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ndivyo vilivyogongana, akirejea kitongoji cha Namitende, kimsingi kipo kijijini Malolo, wakati kiramani inaonyesha ipo kijijini Ng’alu. Walitumia fursa hiyo kuwaelewesha wanavijiji usahihi uliopo.

Anasema tafsiri za kisheria zilitumika, ikiwamo Sheria ya Ardhi na Sheria Namba Saba ya Serikali za Mitaa ya Mwaka 1982, wakiwaunganisha viongozi wa dini zote mbili, wazee maarufu wanaoyajua maeneo tangu uanzishwaji vijiji hivyo, ndipo wakaleta upatanishi kwa kukubaliana wao wenyewe kimaandishi.

Ibrahim anaeleza shaka yake huko nyuma, kwamba huenda mgogoro huo haukuhusisha makundi yote muhimu ikiwamo katika ngazi husika kama vile vijiji, kata, wilaya na tarafa.

Anasema iwapo wangepata elimu stahiki kuhusiana na madhara ya mgogoro na faida za kuumaliza, kabla ya kukubaliana kwa amani, huenda msuguano ulioshuhudiwa usingetokea.

Pia, anataja baadhi ya madhara akijumuisha kurudisha nyuma maendeleo vijijini, wakati faida ya maelewano ya kudumu yanairuhusu serikali na hata wadau kuona namna ya kushirikiana nao katika kutatua magumu hayo.

Ofisa huyo anasema, haishii mtazamo katika suala kutatua mgogoro eneo msitu pekee, bali kikuu ni uwapo wa makazi ya kudumu, sambamba na sehemu ya eneo la msitu jirani na usalama wake.

Ushauri wake ni kwamba jamii inapaswa kutambua kuwa popote kwenye rasilimali, ifahamike ni lazima kutakuwa na dalili za migogoro ikiwamo mipaka, kati ya mtu na mtu au na kijiji, au baina ya vijiji akiweka angalizo kwa mujibu wa uzoefu wao kutatua migogoro.

MGOGORO MOROGORO

Hapo kuna mgogoro uliodumu miaka 30 kati ya kijiji cha Diguzi na Matuli wilayani Morogoro, tangu mwanzo wake mwaka 1990 wao Coforest waliutatua ndani ya wiki moja.

Imewezekanaje? Ibrahim anafafanua: “Mbinu tuliyotumia ni kuangalia kwa undani zaidi chanzo cha mgogoro na kuangalia wadau muhimu wataohusika katika kutatua mgogoro. Hatutegemei mgogoro kurudi tena hapo.”

Hivyo, anawaasa viongozi wa vijiji visivyo na miradi kuangalia namna ya kuepuka migogoro, kwa kukutana na kukaa pamoja kuangalia maslahi mapana ya pande zote, kwani penye migogoro hakuna maendeleo.

Anavipa mbinu vijiji vyenye migogoro ya ardhi, vyema vikakutana kuangalia suluhisho, huku kwa vijiji visivyo na migogoro ya ardhi, nao ni muhimu wakahakiki mipaka na majirani.

“Ushirikishwaji wa mara kwa mara na vijiji jirani utasaidia, sababu mgogoro hutokea sana kama pale rasilimali inakuwa na thamani kubwa kwa jamii,” anaeleza.

Ibrahim anaendelea kufafanua:“Kama migogoro haipo kwa sasa ni vyema kuweka kumbukumbu za kutosha ili baadae kusiwe na usumbufu.”

Anawashauri wanavijiji sasa waweke vikao vya kila mara na kuviandikia taarifa, ili kuwa na kumbukumbu sahihi inayoweka mbali migogoro ya kugombania rasilimali, hata pale inapotokea, inapunguza hitaji la nguvu kubwa ya viongozi wa serikali usuluhishaji migogoro ya vijiji.

Mzee Maarufu wa kijiji cha Malolo wilayani Ruangwa mkoani hapa, Anastas Maluma (62), anaushukuru mradi huo kufika kijiji kwao mwaka 2019 hata ukamaliza mgogoro wao, wakiwa na imani sasa wanaweza kuanza kunufaika na mazao ya msitu wao wenyewe, manufaa kufikia hata vizazi vyao vijavyo.

DODOSO LA MAOFISA

Ofisa Mtendaji wa Kata a Malolo, Abdalah Liuba, anasema kupita mradi huo, yanayotokea Malolo yanabaki historia na sasa vijiji vingine vimetambua uwepo wa miti zaidi ya aina 42 katika maeneo yao, baada ya kupewa elimu.

Pia, anataja kuwapo aina 22 za miti inayoweza kuvunwa kama mbao, hata kuleta faida kwa wavunaji, vijiji na serikali husika.

Ofisa Mawasiliano kutoka TFCG kupitia mradi wa Coforest, Betty Luwuge, anafafanua lengo ni kufikia usimamizi endelevu wa misitu ya asili, utakaoleta mabadiliko ya kiuchumi na kiutawala katika mnyororo wa thamani wa mazao misitu na kuchangia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Luwuge anasema, kupitia mradi wamekuwa wakielimisha umma kuongeza tija katika ushawishi wa utekelezaji sera za maendeleo ya misitu na mazingira.

Anakumbusha katika utekelezaji wa awali, ndiko walikokumbana na pingamizi za migogoro ya mipaka na kuzitatua kabla ya kuanza kutoa elimu, namna ya kunufaika na usimamizi shirikishi wa mazao ya misitu kwa jamii.

Habari Kubwa