Ujue ugonjwa wa kiharusi na tiba yake

05Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Ujue ugonjwa wa kiharusi na tiba yake

KIHARUSI au ‘stroke’ ni hali inayotokea baada ya sehemu ya ubongo kukosa kupata mzunguko wa damu, hivyo chembe hai zake kufa, baada ya kukosa hewa safi yaani ‘oxygen’ na virutubisho vingine.

Sehemu hiyo ikiharibika, inasababisha kazi zilizokuwa zinafanywa na sehemu hiyo kutokufanyika. Kiharusi ni hali ya dharura inayohitaji matibabu ya haraka na ya umakini.

Kuna aina tatu za kiharusi:

KIHARUSI CHA KUKOSA HEWA

Kiharusi cha kukosa hewa kwenye ubongo yaani ‘Ischemic stroke.’ Hiyo inatokea baada ya mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye ubongo au mishipa ya damu ya ubongo kuziba au kusinyaa sana.

Hivyo basi, inasababisha sehemu iliyopo mbele ya huo mzibo ‘blockage’ kukosa hewa safi ya oksijeni na virutubisho vingine na kusababisha seli hizo kufa. Kama sehemu hiyo iliyoharibika ilikuwa inashughulikia misuli fulani, basi misuli hiyo utaona imeathirika, kama ni sehemu inayohusika na kuongea, basi mgonjwa atashindwa kuongea n.k.

Aina hiyo ya kiharusi, imegawanyika katika sehemu kuu mbili. ‘Thrombotic Stroke; Hiyo husababishwa na mzibo uliokuwepo ndani ya mshipa wa damu safi (artery), ambayo inalisha ubongo na kutengeneza ‘clots’ zinazoitwa ‘thrombosis’ zinazoweza kuwa katika mishipa mikubwa au midogo.

Mara nyingi, wagonjwa wenye ‘Atherosclerosis’ huwa wanapata kiharusi kwa njia hiyo.

KIHARUSI CHA MZIBO
Aina hiyo ya pili inaitwa ‘Embolic stroke.’ Hiyo inatokana na mzibo unaosababishwa na ‘clot’ ambayo hutokea sehemu nyingine ya mwili, mbali na ubongo na kuingia katika mishipa ya damu ya ubongo na kwenda kuziba ndani ya ubongo.

Mfano mtu mwenye matatizo ya moyo, damu inaweza kuganda kwenye moyo na baadae damu iliyoganda, ikasafirishwa kwenda kwenye ubongo na kiziba huko. Mtu mwenye ‘Atrial Fibrillation’ huwa ana nafasi ya kutokewa na hali hiyo.

KIHARUSI CHA KUPASUKA MISHIPA

Kiharusi aina hii, inatokana na mishipa ya damu ya ubongo kupasuka na damu kuvilia kwenye ubongo. Kitaalamu inaitwa ‘Hemorrhagic stroke.’ Matatizo makubwa yanayosababisha hali hii, kwanza ni inayoitwa kitaalamu Aneurysms’ na pili, ni mishipa ya damu kuzeeka.

Mingine na wengine ni ‘Arteriovenous Malformation’ (AVM),AVM ni matatizo ya kuzaliwa na sio kurithi. Mishipa ya damu safi na damu chafu inaungana bila ya kuwepo mishipa midogo midogo ya ‘capillaries’ kati yao.

Pia husababisha kuta za mishipa hiyo kuwa hafifu na endapo kutatokea msukumo mkubwa wa damu isivyo kawaida, basi mishipa hiyo huwa rahisi kupasuka na damu kuvilia ndani ya ubongo.

Aina hii ya pili ya kiharusi huwatokea mara nyingi watu wenye shinikizo la damu.

KIHARUSI CHA MUDA MFUPI

Aina ya tatu ni ‘Transiet Ischemic Attack (TIA).” Hii inafanana kidogo na ile aina ya kwanza, ila kwenye hii, dalili na madhara ya kiharusi hayakai muda mrefu.

Mtu anaweza kupata dalili hizi kwa muda wa dakika moja hadi tano hivi, na mara nyingi dalili hizo huwa zinapotea katika masaa 24.
Katika aina hii ya kiharusi, mtu huwa hapati madhara ya kudumu, madhara huwa ni ya muda mfupi.

Kikubwa cha kufanya ni kuzuia hali hiyo isitokee tena, kwani inaweza kurudia na kusababisha kiharusi kikubwa. Kitaalamu, hali hiyo ya TIA inaitwa ‘Mini-Stroke’

DALILI ZA KIRAHUSI
Dalili kuu za kiharusi ni kama zifuatazo;

• Kupata ganzi au udhaifu ambao mara nyingi unaanza ghafla. Mara nyingi huwa unatokea upande mmoja wa mwili, yaani kushoto au kulia. Mara nyingi, husababisha upande mmoja wa uso kufa ganzi au kuwa dhaifu.

• Kuchanganyikiwa na kushindwa kuongea, hali inayotokea ghafla.

• Kupoteza uwezo wa kuona. Kitu kimoja, kinaonekana kama vile vipo viwili, ukungu, kupoteza nguvu ya kuona inayoweza kutokea kwenye jicho moja au yote mawili.

• Ghafla, kichwa kinauma sana, bila ya kuwa sababu maalumu na mara nyingine huambatana na kusikia kichefuchefu au mtu anatapika.

• Kushindwa kutembea ghafla, kushindwa kusimama na kusikia kizunguzungu.

• Wakati mwingine mtu anapoteza fahamu.

NAMNA YA KUZUIA KIHARUSI

• Kuangalia au kupima msukumo wa damu yaani, ‘Blood Pressure’

Ni muhimu sana na hasa kwa watu wenye matatizo hayo, kuhakikisha misukumo yao ya damu inakuwa katika hali ya kawaida kila mara.

Msukumo wa damu kuwa juu, una madhara mengi, ikiwemo hilo la kupasuka mishipa ya damu ya kwenye ubongo na kusababisha kiharusi.

• Kuwa na tabia ya kupima wingi wa helemu ‘ Cholosterol levels’

Ni muhimu sana, kila mtu akawa na tabia ya kupima wingi wa lehemu ili kujua aina gani ya lehemu ambayo kwako ipo juu au chini.

Wingi wa lehemu mbaya yaani ‘bad cholesterol’ unasababisha lehemu hiyo kujishikiza au kukaa katika mishipa ya mtu ya damu na kusababisha kupungua tundu la kupitisha damu ndani ya mshipa wa damu.

Wakati mwingine, mafuta hayo huwa yananyofoka kutoka katika kuta za mishipa hiyo ya damu na kwenda kunasa katika sehemu nyingine ya mwili, kwa mfano katika ubongo na huleta madhara ya kiharusi. Hiyo ina maana, itazuia damu kupita kabisa au kupita kidogo sana

• Kuzuia uvutaji sigara na unywaji wa pombe uliopitiliza.

Utafiti mwingi umefanyika na kugundua madhara makubwa ya sigara. Uvutaji sigara na unywaji pombe uliopitiliza, husababisha kiharusi. Kemikali zilizokuwepo kwenye sigara zina uwezo mkubwa wa kuharibu kuta za mishipa ya damu.

Kibaya zaidi ni kwamba, kama mvutaji wa sigara ana mwili mnene uliopitiliza, ana ugonjwa wa shinikizo la damu au kisukari, inamuweka katika wakati mbaya zaidi.

Kwa wale wanaotumia dawa za kulevya, kwa mfano aina ya Herroin, wana hatari kubwa ya kupata kiharusi, kwani utegemezi wa kilevi hicho huzaa madhara makubwa katika moyo wake na kuharibu mfumo mzima wa msukumo wa damu, hali inayotishia maradhi ya kiharusi.

• Kufanya mazoezi; Mazoezi ni muhimu sana kwa afya ya mwanadamu. Mazoezi yanaweza kuzuia nafasi ya mtu kupata ugonjwa wa shinikizo la damu na kisukari.

• Kupunguza msongo wa mawazo; Ni muhimu sana kupunguza msongo wa mawazo hasa kwa mtu mwenye ugonjwa wa shinikizo la damu na kisukari.

Mtu anapokuwa kwenye msongo wa mawazo mwili wake unatengeneza homoni zinazosababisha kuongezeka kwa msukumo wa damu, pia kutengeneza homoni zinazosababisha mwili kutoa sukari katika ini ambako ilihifadhiwa na kuiingiza kwenye damu.

Hivyo, iwapo mtu ana ugonjwa wa kisukari, hapo ndio inaleta shida, maana sukari yake kwenye damu, itakuwa juu wakati yeye anatumia dawa. Hivyo, hali hiyo ya sukari kuwa juu mwilini anaweza asiitambue.

• Jifunze au uwe na tabia ya kula vyakula vyenye mafuta kidogo. Vyakula vyenye mafuta kwa wingi, husababisha mwili kuwa na mafuta mengi, hali ambayo si nzuri kiafya na inaweza kusababishia magonjwa ya moyo na hatimaye kiharusi.

• Kula vyakula vyenye chumvi kidogo. Asilimia kubwa ya chumvi inayotumiwa, ina madini ya ‘sodium.’ Hiyo ni kemikali ambayo ipo zaidi katika majimaji yaliyomo mwilini mwetu, hasa nje ya chembehai zilipo.

Mwili unakuwa na kiwango maalumu cha kemikali hiyo na iwepo wa kemikali hiyo kwa wingi, unasababisha kuongezeka kwa msukomo wa damu.

Hivyo basi, tukila chumvi kidogo maana yake tunaingiza hiyo ‘sodium’ kidogo na kutunusuru kwa kupanda kwa msukumo wa damu na maana yake kutupunguzia athari za kupata kiharusi.

Kwa ujumla, ni vizuri kubadili mfumo wa maisha tunayoishi ili kujinusuru na kupata kiharusi.

Habari Kubwa