UKAGUZI WA CHOMBO CHA MOTO-1

14Nov 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
UKAGUZI WA CHOMBO CHA MOTO-1

CHOMBO cha moto kimeundwa kwa mifumo mbalimbali kama vile mfumo wa breki, umeme, maji, injini, bodi, mneso, usukani, magurudumu, mafuta, moshi na gia na kinaweza kuendeshwa barabarani au njiani kwa kutumia nguvu na akili ya binadamu ambaye ameruhusiwa kisheria.

Zipo aina mbalimbali za magari zenye matumizi tofauti tofauti.

Baadhi ya magari ni matoleo ya muda mrefu na yanahitaji uangalizi na umakini mkubwa katika utunzaji wake.

Utunzaji na uangalizi mzuri wa gari linapotumika barabarani unapaswa kuzingatiwa na mmiliki au dereva na anapaswa kulifanyia ukaguzi katika mifumo yote kabla, katikati au baada ya safari.

Sheria ya Usalama Barabarani, sura ya 168 kifungu 39 (1) kinaeleza kuwa, gari lolote halitaruhusiwa kutumia barabara iwapo mojawapo ya mifumo yake ina hitilafu.

Ukaguzi wa magari unafanyika kwa lengo la kulichunguza au kuliangalia gari kabla ya safari na baada ya safari ili kuona kama mifumo yake yote imekamilika na ina ubora.

Ukaguzi huu utabainisha mfumo ambao una ubovu ili ufanyiwe matengenezo kabla ya gari hilo kutumika barabarani.
Kuna aina mbili za ukaguzi wa magari ambazo ni ukaguzi wa hiari na ukaguzi wa lazima.

Ukaguzi huu hufanywa na mmiliki au dereva wa gari kabla ya kuingiza chombo chake barabarani.

Mmiliki au dereva wa gari hufanya ukaguzi huu ili kubaini kama kuna ubovu au tatizo lolote katika mifumo yote iliyomo kwenye gari na kuifanyia marekebisho mapema kabla ya kulitumia barabarani ili kuepuka kuvunja sheria na taratibu za nchi.

Sheria ya Usalama Barabarani sura ya 168 kifungu cha 39 (5) kinaeleza kuwa mtu yeyote ambaye atashitakiwa kwa kuendesha gari bovu barabarani anastahili kulipa faini au kifungo cha miaka mitano jela au adhabu zote mbili kwa pamoja.

Ukaguzi wa gari wa mara kwa mara husaidia kujiridhisha ubora wa gari lako, kuepuka kutenda makosa, kubadilisha matumizi ya gari, kuepuka kufanyiwa ukaguzi wa lazima (ambao huendana na faini za papo kwa papo au kupelekwa mahakamani).

Aina ya pili ya ukaguzi ni ukaguzi wa lazima ambao hufanywa na askari polisi kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 sura ya 168 kifungu namba 81, 82, na 83.

Sheria hii inampa askari Polisi mamlaka ya kusimamisha na kukagua gari.

Pia kifungu cha 83 kimempatia nguvu afisa mkaguzi wa polisi kukagua gari na kisha kutoa hati ya ukaguzi baada ya kukagua. Ikiwa kuna tatizo atakalolibaini, atatoa maelekezo likatengenezwe kisha lirudishwe kwa ajili ya ukaguzi mwingine baada ya matengenezo.

Endapo matengenezo yaliyofanyika hayaridhishi, afisa huyo anaweza kuliondolea namba za usajili na kuzirudisha kwa msajili.

Msajili anaweza kulifutia usajili gari hilo mpaka hapo afisa mkaguzi atakapomjulisha kuwa gari hilo limeshatengemaa.

Ukaguzi wa magari unaofanywa na Jeshi la Polisi hufanywa katika aina mbili ambazo ni ukaguzi wa ndani na ukaguzi wa nje ya eneo la polisi.

Ukaguzi wa ndani hufanyika katika eneo maalum la polisi ambalo limetengwa kwa ajili ya kukagulia magari.

Ukaguzi huu huhusisha ukaguzi wa mifumo ya ndani ya gari na ya nje na umegawanyika katika sehemu nne ambazo ni;
Ukaguzi wa Polisi baada ya mmiliki kupeleka gari kukaguliwa.

Ukaguzi wa aina hii wa mmiliki mwenyewe kupeleka gari lake kituo cha polisi bila kulazimishwa (owner request) hukusudia liweze kufanyiwa ukaguzi kwa nia ya kufahamu ikiwa gari lake lina hitilafu yoyote ili aweze kulifanyia marekebisho kulingana na ubovu uliogundulika.

ITAENDELEA WIKI IJAYO