Ukame, njaa vyakoleza taabu Somalia mashambulizi Al Shabaab yakiendele

13Nov 2019
Ani Jozen
Dar es Salaam
Nipashe
Ukame, njaa vyakoleza taabu Somalia mashambulizi Al Shabaab yakiendele

WANANCHI wa Somalia wanatafuta njia ya kutokea kwa jambo ambalo kimsingi wamezoea lakini halizoeleki, yaani mchanganyiko wa ukame na vita vya kigaidi vya kundi la Al Shabaab.

Vikosi vya kulinda amani nchini Somalia, vikiimarisha ulinzi baada ya shambulizi la al Shabaab kwenye kambi ya mafunzo. PICHA: MTANDAO

Hali hiyo ni kama imepotea katika anga za kimataifa kwani hakuna majeshi ya nje ila vikosi vya Umoja wa Afrika (AU) vikisaidiwa na Umoja wa Mataifa (UN).

Hapohapo Marekani ina kambi ya kurushia ndege nyuki (drone) kufanya mashambulizi dhidi ya mikusanyiko inayohusu Al Shabaab kama maeneo ya kutoa mafunzo ya kijeshi, au mikutano ya makamanda.

Hata hivyo, uwezo wa kundi hilo wa kufanya mashambulizi ya kushtukiza haujapungua; mwaka huu imeleta simanzi nyingi.

Mashambulizi ya Al Shabaab yanasikika zaidi pale wageni wanaposhambuliwa, kwa mfano hapo Septemba 30 walishambulia msafara wa magari ya maofisa wa Umoja wa Ulaya (EU) na kambi ya jeshi la Marekani ya kuhifadhi ndege nyuki.

Mashambulizi ya ndege hizo, licha ya kuwa zinaruka na kurudi kambini kule zinapopiga, yanapangwa na makao makuu ya Jeshi la Marekani na kuongozwa kitaalamu kutokea vituo maalum huko Marekani.

Kuziweka kambini Somalia ni kuhifadhi tu kupunguza umbali wa kuruka, lakini ni vita ya kielektroniki inayopigiwa Marekani.

Karibu kila mwezi kuna mashambulio au angalau shambulio moja kubwa, na wakati mwingine wanayaunganisha endapo vipigo vya jeshi la Marekani vimezidi, halafu wanalipa kisasi kwa mfano Mogadishu ambapo wanapenda kushambulia ofisi za serikali au viongozi kama meya au waziri.

Inaweza kuwa mpaka wa Kenya ambako wanapenda kulipua magari ya polisi, au jijini Nairobi ambako zaidi wanapendelea kupiga mahoteli na kuua watalii, waandishi wa habari, n.k.

Taarifa zinasema mashambulizi ya ndege nyuki za Marekani yameongezeka kuliko mwaka jana.

Waliposhambulia mjini Kismayu hapo Julai 12 dhidi ya hoteli ya Asasey watu 26 walikufa na 56 kujeruhiwa, na miongoni mwa waliokufa alikuwepo raia mmoja wa Uingereza, raia watatu wa Kenya na watatu wa Tanzania.

Lakini aliyetajwa zaidi ni mwandishi wa habari wa Kisomali mwenye uraia wa Canada, aliyefariki pamoja na mumewe akaliliwa na waandishi wa habari maeneo mengi nchi za Magharibi.

Al Shabaab ilipeleka gari la kujitoa mhanga lililoshindiliwa mabomu kuvunja lango ya hoteli hiyo na kulipuka, kuharibu eneo hilo na kuleta mahangaiko, wakati wapiganaji wa Al-Shabaab waliovalia mikanda ya risasi wakipenya na kupiga kila kona.

Mitandao inasema kuwa taarifa za kiinteligensia zinasema kuwa Al Shabaab imekuwa ikiunda Mahakama maeneo inayoshikilia ili kuwanyonga inaokuta na makosa ya kukiuka sheria za jadi zinazosimamiwa na kundi hilo.

Baadhi ya wachambuzi wanaozungumza na maofisa usalama wa nchi za jirani wanasema sababu ni kuwa kundi hilo linataka kuonyesha kuwa lina nguvu, licha ya kupoteza mamia ya wapiganaji kutokana na vita ya ndege nyuki ya Marekani.

Pia kuna mfululizo wa mapambano na askari wa jeshi la Somalia linalojengeka taratibu katika miezi kadhaa sasa.
Al Shabaab pia inapata msaada wa kisaikolojia wa vyombo vya habari nchini Marekani na kwingineko.

Kuna mfano malalamiko kuwa mashambulizi ya ndege nyuki yanaua raia wa kawaida, rai iliyo na maana kuwa ndege hizo zisitumike. Marekani ipeleke askari, au iache vita.

Shirika la uandishi wa habari za upelelezi (Bureau of Investigative Journalism) lilisema kuwa mwendo wa mashambulizi kwa ndege nyuki umeongezeka kwa kasi mwaka huu, kuwa mwaka jana kulikuwa na mashambulizi ya Marekani 47 na mwaka huu yalishafika 50 na inaaminika yameua wapiganaji 300 wa Al Shabaab mwaka huu kwa data zilizokusanywa na kusanifiwa na shirika hilo.

Ni vita ambayo Rais Donald Trump wa Marekani anaiweza, ya kutumia pesa, si kupoteza maisha ya askari katika vita ambayo haina mwisho, kwani inapiganwa kama sehemu ya imani.

Al Shabaab inapata mapigo lakini imepeleka vilio visivyohesabika nchini humo, kwani mashambulizi yake yanapeleka misiba kila kukicha na mara nyingine ni misiba mikuu.

Mara baada ya Al Shabaab kushambulia hoteli moja Nairobi Januari 15 mwaka huu, Marekani iliinua mashambulio ya ndege nyuki dhidi ya vituo vya kundi hilo au mizunguko yao ardhini kama inavyoonekana kutoka angani, na kuua wapiganaji takriban 52 kwa wakati mmoja, lakini kuna raia wa kawaida waliopoteza maisha.

Ni hapo watetezi wa haki za binadamu wanalalamikia ndege nyuki wakati makundi ya kigaidi yanajua lazima yachanganyike na watu ili kujihami.

Katika miaka ya karibuni, shambulio kubwa zaidi la Al Shabaab lilifanyika Oktoba 14 mwaka 2017, linaloaminika kuwa shambulio kubwa zaidi la kundi hilo tangu kuundwa kwake.

Gari la mizigo lililosheheni baruti zilizotegwa kulipuka lililipuliwa katika makutano ya barabara karibu na hoteli ya Safari wilaya ya Hodan, halafu lori la mafuta lililokuwa limeegeshwa karibu na hapo likalipuka pia.

Mkanganyiko huo ukazusha moto mkubwa wakafa watu takriban 500.

Wachunguzi wa habari wanasema Al Shabaab wanafanya mashambulizi kwa kudhamiria na kuvizia, hivyo ingawa Kismayu inapakana na maeneo yanayoshikiliwa na Al Shabaab katika mashamba au mbuga, ambazo mara nyingi zina ukame wa kufa mtu, haushambuliwi sana.

Cha kushangaza ni kuwa alipokufa mwandishi wa habari Hodan Nalayeh, Wasomali walioko nje ndiyo waliopata nafasi ya kueleza masikitiko yao na maombolezo.

Imamu Omar Suleiman ambaye anasalisha huko Texas, Marekani akalaani tukio hilo na habari hizo zinatangazwa katika redio zilizoko maeneo huru Somalia. Inakuwa vita kati ya uhuru na udhalimu, siyo na Marekani.

Wakati Al Shabaab inanyonga watu vijijini na kushambulia mijini kuua maofisa wa serikali na hasa wageni wanaoendesha shughuli za kibinadamu au biashara, kutafuta habari inavyoendelea nchi hiyo, mabadiliko ya tabianchi yanaongezea taabu.

Raia wengi nchini humo wako katika makambi kutokana na vijiji na miji kuteketezwa kwa sehemu kubwa katika vita, halafu jitihada za kilimo zinaharibiwa na mafuriko, kuwahitaji kuhamia maeneo ya mwinuko zaidi.

Mwezi Septemba ulikuwa mbaya kutokana na mafuriko, kwani mawimbi ya vimbunga baharini sasa yanakuwa na uwezo wa kufika ndani ya Somalia kama ilivyo kwingine ukanda huu wa Afrika.

Maafa makubwa zaidi kwa upande huo yalikuwa mwaka 2010 hadi 2012 ambako taarifa zinasema watu karibu 260,000 walikufa katika ukame ulioipiga Somalia, na watu 220,000 walikufa kutokana na ukame mwingine mwaka 1992.

Ukiangalia unakuta kuwa mazingira ya ukame yanaleta maafa makubwa kutokana na udhaifu wa miundombinu kwa kuharibiwa mifumo ya utawala, na pia nchi za Magharibi kutokuharakisha misaada kwa kuhofia kuwa makundi ya wapiganaji nao watachota huko kwani wanashikilia sehemu nyingi zinazokumbwa na ukame.

Ni hali inayokumba nchi za Afrika zenye vita visivyoisha na kuathirika na mabadiliko ya tabia nchi, kuwa matokeo yake ni vifo vya mamia ya maelfu ya watu hasa nyakati za ukame, Somalia ikiwa inaungana na Nigeria (ya kaskazini) na Sudan Kusini.
Yemen inaikaribia Somalia janga hilo.

Habari Kubwa