Ukatili kijinsia unavyoweka maisha ya wanawake wa Zanzibar rehani

07Jan 2017
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Ukatili kijinsia unavyoweka maisha ya wanawake wa Zanzibar rehani

MIAKA miwili tangu Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kuzindua kampeni ya kutokomeza vitendo vya ukatili na udhalilishaji kijinsia, kinachotizamwa leo ni kwa kiasi gani kampeni hiyo imefanikiwa?

Akizundua kampeni hiyo mwaka 2014 Dk. Shein, pamoja na viongozi wa dini na wanaharakati mbalimbali wa kutetea haki za wanawake na watoto, kulikuwa na matarajio makubwa ya kushinda vita hivi.

Katika kutathimini mafanikio kwa miaka miwili ya kampeni hiyo, inaonekana kuwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto vinatisha visiwani Zanzibar.

Uzinduzi huo wa kitaifa ulikuwa na matarajio ya kupunguza au kutokomeza ukatili na udhalilishaji kwa kutumia njia mbalimbali kama mikutano ya hadhara na elimu kupitia shehia (serikali za mitaa), wilaya hadi taifa.

Leo cha kusikitisha ama kushangaza ukatili unapamba moto na unyanyasaji unaendelea.

Hata takwimu ambazo zimekuwa zikitolewa na vyombo vya sheria ikiwemo mahakama, polisi, hospitali na madawati ya kijinsia, zinaonyesha ongezeko kubwa la udhalilishaji waathirika wakifikia karibu 200 kwa mwaka 2016.

Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa) Zanzibar kinaripoti kuwa kilipokea kesi 66 kwa mwaka jana.

Katika hospitali ya Mnazimmoja kesi 65, Idara ya Watu Wenye Ulemavu wa 96, polisi 35 na Ofisa ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini 33.

Japo takwimu hizo pia zinatafsiriwa kuonyesha mwamko wa kuripoti udhalimu huo polisi kutoka upande wa wanajamii.

Miongoni mwa matukio ambayo yameshtua Wazanzibari tukio la msichana aliyeunguzwa moto katika Kijiji cha Paje na mpenzi wake aliyemtegemea kuwa mtu wake wa karibu kwa raha na shida.

Desemba 15 mwaka jana, ndiyo siku wa mkasa huo uliripotiwa huko kijijini Paje mkoa wa Kusini Unguja.

Samira Abasi Amir (26) aliiunguzwa moto na mpenzi wake Omar Said (28) baada ya Omar kumkataa mpenzi wake huyo.

Samira ambaye ni mfanyakazi wa hoteli ya kitalii iliyoko Paje alimwagiwa mafuta ya taa na kuwashwa moto kwa kibiriti cha gesi mithili ya taka taka ambazo zinahitaji kuteketezwa.

“Ilikuwa saa 8:00 usiku, alikuja mpenzi wangu ambaye ndiye aliyenisababishia majeraha haya. Alipoingia alinikuta naweka nguo zangu katika begi ili niondoke baada ya kuchoshwa na vituko anavyonifanyia.

Aliniambia huondoki hapa na kuchuku jiko la mafuta ya taa na kunimwagia pamoja na nguo zangu na kuniwasha moto,”anasema Samira.

Anazungumza na Nipashe akiwa hospitalini anapoendelea na matibabu.

Akizungumza kwa sauti ya huzuni huku akiwa na maumivu makali, anasema wakati mpenzi wake anafanya tukio hilo alifunga mlango ili ateketee.

Anasimulia , “baada ya kunichoma moto alitoka nje na kunifungia ndani nilipiga kelele na kumuomba anifungulie mlango.”

Anasema alifanikiwa kufungua mlango na kujimwagia maji na kukimbilia kituo cha polisi wakati aliyemjeruhi ameshakimbia, akimwachia ajifie mwenyewe ndani.

“Nilitoka hapo na kukimbilia polisi kwa kuwa kituo cha polisi kipo mbali nilipokuwa barabarani niliomba msaada hadi kituo cha polisi Makunduchi,”anasema.

Baada ya hapo alifikishwa hospitalini hapo na kupatiwa matibabu huku akiwa na majeraha kuanzia usoni, mikononi na kifuani.

Mganga Msaidizi wa Hospitali ya Makunduchi , Asha Salum, anasema tukio hilo la moto ni kubwa na ni la mwanzo kufikishwa hospitalini hapo kwa mwaka wa 2016.

Aidha anasema wakati majeruhi huyo alipofikishwa hospitalini hapo alikuwa ameunguzwa mno na moto.

“Hivi leo ni siku ya tano tangu tumempokea Samira na hali yake inaendelea vizuri ana nafuu si kama alipofikishwa hospitalini hapa,”anasema.

Mama mzazi wa Samira Mwajuma Rajabu mkaazi wa Kibaha Dar es Salaam, anasema alipokea simu ya taarifa ya mtoto wake kupata ajali ya moto, ndipo alipoanza safari ya kwenda kumuuguza.

Anaeleza kuwa baada ya kufika Zanzibar alimkuta hospitalini amelazwa na hali yake si nzuri kutokana na majeraha makubwa aliyopata.
“Kwa kweli nilikuwa sijui chanzo cha ajali baada ya kufika hospitali nikasimuliwa hivyo, naviomba vyombo vya dola kuhakikisha haki inapatikana na mtuhumiwa vinamtia hatiani aliyemsababishia mwanangu majeraha haya,”anasema.

Waziri wa kazi, Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Modlene Castiko, alisemea tukio hilo na kusema kuwa, halipaswi kufumbiwa macho ni lazima mtuhumiwa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Hakuna nchi yenye sheria bora kama Zanzibar, lakini hizi zilizopo kusimamia masuala ya udhalilishaji hazitekelezwi kutokana na muhali (aibu) kwa wanajamii, anasema Kastiko.

Anasema vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa wanaovitenda vimekuwa ni kama mazoezi ya kuwatendea ukatili wengine kwa sababu hakuna sheria zinazofuatwa kuwatia hatiani.

“Wanaume wasidhani kuwa ukimpata mwanamke ndiyo iwe mali yako na kumfanya vyovyote utakavyo sivyo.

Kama mwezako ameshakukataa ni vyema umuwache kwa salama na si kujichukulia sheria mikononi na kumdhalilisha,”anaonya.

Polisi Zanzibar inamshikilia mtuhumiwa Omar Said aliyemuunguza kwa moto mpenzi wake na uchunguzi utakapokamilika atafikishwa mahakamani.

Hivi karibuni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yussuf Masauni, alilitaka Jeshi la Polisi Zanzibar, kuweka mikakati madhubuti kuhakikisha wahalifu wa vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia wanatiwa hatiani.

Akizungumza na maofisa wa jeshi hilo akiwemo Kamishna Hamdani Omar Makame, Masauni anasema kuongezeka kwa vitendo hivyo hakupaswi kushughulikiwa kirafiki au kuoneana aibu.

Analitaka Jeshi la Polisi kuanza kutoa elimu ya udhalilishaji kuanzia ngazi za shehia, wilaya hadi taifa ili kuibua changamoto mbalimbali zinazohusiana na mambo ya unyanyasaji huo.

Anasema kutokana na wimbi kubwa la vitendo hivyo Zanzibar, hakuna njia nyingine ya kuvitokomeza zaidi ya kuchukua hatua madhubuti na zisizokuwa na muhali (aibu).

Masauni anasema inasikitisha kuwa pamoja na wingi wa vitendo hivyo, bado wahalifu wa matukio hayo wanaranda mitaani kwa sababu mbalimbali.

Naibu waziri huyo alisema wakati umefika kwa wabakaji na wadhalilishaji kuanikwa hadharani ili kuvikomesha vitendo hivyo.

“Kuna mambo mawili makubwa lazima tuyafanye kwa nguvu na tulichukulie hili ni janga la kitaifa kwani takwimu za ubakaji zinatisha na kunaongezeka zaidi ya asilimia 84,”anasema Masauni.

Kamishna wa jeshi hilo Makame, anasema kuwa watahakikisha kuwa janga la udhalilshaji wa kijinsia watapambana nalo na hawapo tayari kuwavumilia wapatanishi wa kesi za ubakaji.

Anaongeza kuwa wakati umefika kwa jeshi hilo kusaidiwa katika masuala ya uchunguzi wa nasaba (DNA) na mambo yote yanayohusisha ofisi ya Mkemea Mkuu wa Serikali .

Anasema hatua hiyo ni muhimu kwa sababu jeshi hilo lina madeni mengi kuhusiana na kesi zinazohitaji uchunguzi kutoka kwa mkemia mkuu wa serikali.

Aidha kuna mrundikano wa kesi nyingi zinazohitaji uchunguzi kupitia kwa maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, kutokana na jeshi hilo kuwa na changamoto ya fedha kwa ajili ya gharama za kesi hizo zikiwamo za ubakaji zinazohitaji vipimo vya DNA.

Habari Kubwa