Ukawa unavyozidi kutibuka baada ya Lowassa kuibwaga

20Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Ukawa unavyozidi kutibuka baada ya Lowassa kuibwaga

KURUDI CCM kwa aliyekuwa Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa, pia mgombea wa urais wa vyama vya wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), akitokea Chama cha Chadema, kunafungua ukurasa mpya wa siasa za ushindani nchini na kuhitimisha minong’ono ya muda mrefu kuwa atakihama chama hicho .....

Aliyekuwa Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Profesa Lipumba (kulia), wakati akimkaribisha Lowassa upinzani baada ya kujiunga na Chadema, kushoto ni Freeman Mbowe Mwenyekiti wa Chadema. PICHA: MTANDAO.

kikuu cha upinzani.

Kuhamia kwa Lowassa upande wa pili kulipokelewa kwa msisimko mkubwa na shamrashamra nyingi na kulisababisha sintofahamu kuhusu nani angegombea urais kupitia Ukawa, ikizingatiwa kuwa kwa wakati huo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema Dk.Wilbroad Slaa alikuwa akitazamiwa kupeperusha bendera ya wapinzani.

Pia, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, kabla ya kutokea mgogoro alikuwa miongoni mwa wanaotajwa kutaka kugombea urais kupitia Ukawa.

Hata hivyo, kwa mshangao wa wengi vigogo hao wawili waliwekwa kando na hatimaye Lowassa kupewa nafasi ya kupeperusha bendera ya umoja huo wa vyama wa upinzani.

Ujio wa Lowassa ulileta mpasuko mkubwa kwa vyama vya upinzani na kusababisha baadhi ya vigogo kubwaga manyanga, akiwamo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Slaa, kujiuzulu nafasi yake.

Aidha, alitangaza kuachana na siasa za vyama kwa kile alichodai hawezi kumnadi Lowassa ambaye hapo kabla wapinzani walidai kuwa hafai kuongoza nchi.

Kadhalika, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye hapo awali alihudhuria mapokezi ya kumkaribisha Lowassa Ukawa, naye alijiuzulu uenyekiti wake kwa madai kuwa nafsi yake inamsuta na kuwa hawezi kumpigia debe kuingia Ikulu kwa sababu zilizofanana na za Dk. Slaa, lakini Profesa Lipumba hakujivua uanachama wake.

Ikiwa ni takriban miaka minne imepita tangu Lowassa ajiunge upinzani na kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu, kurudi kwake CCM kunaacha maswali mengi juu ya uamuzi wake huo, hasa ikizingatiwa kuwa amefikia maamuzi hayo wakati ambapo mwenyekiti wake yupo rumande.

Akizungumzia kurudi kwa Lowassa katika chama chake cha zamani Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, amenukuliwa akimtakia heri na kuongeza kuwa Lowassa alikuwa ugenini na sasa amerudi nyumbani.

“Lowassa mwenyewe amesema amerudi nyumbani. Maana yake ni kwamba alikuwa ugenini tangu Julai 2015 hatukununuliwa kama tulivyowahi kutukanwa huko nyuma,” Lissu alisema.

UPINZANI SI BWERERE

Ukichambua kwa makini kauli ya Lowasa ya kurudi nyumbani na ile ya Lissu ya kuwa Lowassa alikuwa ugenini tafsiri zaidi inayoweza kupatikana ni kwamba Lowassa mazingira ya upinzani yalikuwa ni mageni kwake na ambayo asingeweza kuyaishi kwa muda mrefu.

Maisha ya kiharakati kuchanganya kukamatwa kamatwa mara kadhaa na vyombo vya dola ni vitu vigeni ambavyo hakuwa akikutana navyo akiwa Chama Cha Mapinduzi akiwa kule hata baada ya kujiuzulu alipata ulinzi kama ilivyo kwa mawaziri wakuu wastaafu.

Aidha, alishiriki shughuli mbalimbali za kichama na kiserikali ambazo hazina bughudha wala kashkash kama ilivyo kwa upinzani kitu ambacho alionekana kuanza kukirudia akiwa upinzani mathalani, hivi karibuni wakati aliposhiriki ufunguzi wa maktaba ya kisasa ya kielektroniki ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Katika majukumu hayo kikubwa zaidi kilichojitokeza ni kuanza kusifiwa na viongozi wa serikali na Chama Cha Mapinduzi.

Akizungumza katika mkutano wa kumkaribisha nyumbani waziri mkuu huyo mstaafu alitaka asiulizwe maswali zaidi ya nini hasa kimemfanya arudi nyumbani na kusisitiza kuwa amerudi nyumbani na si kwa jirani.

“Nimerudi nyumbani wala si kwa jirani, msiniulize nimerudi kufanya nini,” Lowassa anasisitiza.

Lowassa ametuacha na maswali ya nini sababu hasa ya kurudi nyumbani hasa ukizingatia malengo yaliyo mfanya kuhamia upinzani hayajatimia. Watu wanajiuliza amekerwa na nini kutoka upinzani au amevutiwa na nini hasa kutoka chama chake cha zamani ambako amekuwa akikilalamikia kwa uonevu mara kadhaa?

Uamuzi huu wa Lowassa na hasa ikizingatiwa kuwa ni mwanasiasa mkongwe unathibitisha maana ya siasa kuwa lengo lake kuu linaweza kuwa zaidi ya moja kwa wakati mmoja.

WAPINZANI WAPARAGANYIKA

Kile kilichowafanya wapinzani hasa Ukawa kutengana sasa hakipo tena. Matumaini ya kuendelea kuungana yanazidi kupotea. Kwani licha ya Lowassa kuondoka kilichotokea ni Lipumba kuachana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye sasa ni mwanachama wa ACT-Wazalendo, huu ni ufa mwingine mkubwa ndani ya Ukawa, unaoacha maswali mengi.

Licha ya Maalim Seif na CUF kuwa washirika wakuu wa Ukawa pamoja na Chadema, anatangaza kuwa amefanya uchunguzi kwenye vyama vingi vya siasa na akaona kinachomfaa ni ACT- Wazalendo ambacho si mdau wa Ukawa. Vipi waliokuwa wana Ukawa wenzake?

Dk. Slaa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema kwa sasa ni Balozi nchini Sweden. Aliondoka Chadema kwa madai kuwa hakuwa tayari kumnadi Lowassa kama alivyodai, Profesa Lipumba. Je, atakuwa tayari kuachia ubalozi kurejea katika upinzani?

Katika siasa yote yanawezekana kutegemeana na utashi wa wahusika na pia siku moja katika ulimwengu wa siasa inatosha kubadili historia iliyokuwapo hapo kabla, hivyo tutegemee mengi katika siasa.

Hata aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema huko nyuma, Zitto Kabwe na baadaye kufukuzwa uanachama na hatimaye kupoteza ubunge wake kwa sasa ni mshirika mkubwa wa chama chake cha zamani katika mambo mbalimbali na hata kwa wana Umoja wa Katiba ya Wananchi –Ukawa.

HAKUNA ADUI

Somo linalojiri hapa ni kwamba katika siasa hakuna urafiki wala uadui wa kudumu kwa kuwa ni nani aliyejua kuwa Lowassa na Jakaya Kikwete ambaye alikuwa Rais na kumteua Lowassa kuwa Waziri Mkuu wangeweza kutofautiana?

Ama Profesa Ibrahim Lipumba na Maalim Seif kufikia hatua ya kufikishana mahakamani na mahakama kutoa ushindi kwa Mwenyekiti Lipumba, hatua inayomlazimisha Maalim Seif kuhamia ACT –Wazalendo?

Au ni nani aliyejua kuwa Dk. Slaa na Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, hatimaye wangekuja kutofautiana na kufarakana? Ni wazi chama kilichokufukuza leo kinaweza baadaye kukupokea upya kutokana na mazingira ya wakati huo. Mathalani, aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila aliwahi kufukuzwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiitwa sisimizi lakini baadaye alikuja kuwa mshirika mkubwa wa Ukawa na hatimaye mkewe ni mbunge wa viti maalum kupitia Chadema.

Kubwa la kujifunza katika siasa ni kuwa kuna mambo yasiyotabirika na ambayo si ya uhalisia, kwa kuwa wanasiasa wanaweza kuhubiri mvinyo lakini kinywaji chao ni maji, aidha wanaweza kuhubiri matumizi ya maji japo ni washiriki wakuu wa mvinyo.

Habari Kubwa