Ukeketaji sasa wafanyika kwa siri kubwa Singida

14May 2019
Salome Kitomari
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ukeketaji sasa wafanyika kwa siri kubwa Singida
  •  Ni kwa imani ya kutibu ugonjwa wa ‘lawalawa’
  •  Ni kupitia kucha ndefu iliyofugwa na ngariba
  •  Kidonda hupakwa mkojo au masizi ili kipone

​​​​​​​KWA mujibu wa Kamusi ya Kiswahili (Swahili Oxford Living Dictionaries), neno mila lina maana ya mambo yanayofanywa na jamii fulani ambayo yanalingana na asili, mazingira na nyendo za jamii hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ikungi, Justice Kijazi, (kulia) akisalimiana na wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Ikungi,mkoani Singida. PICHA: MPIGA PICHA WETU

Nimeanza kutoa maana ya neno hilo, kwa sababu makala zangu tatu zijazo kuanzia hii zinajikita zaidi katika eneo hili la mila kutoka mojawapo ya makabila yaliyoko Kanda ya Kati na Ziwa.

 

Jamii nyingi katika maeneo mbalimbali nchini na kwa maana hiyo makabila tofauti yameweza kuwa yalivyo hivi leo pamoja na mambo mengine kwa sababu ya kutoa kipaumbele kwenye mila zao.

 

Hivyo mila ni eneo la thamani kubwa ambalo limechangia maendeleo ya jamii kwa upande mmoja, lakini pia kudumaa kwa baadhi ya jamii nchini na katika maeneo mengi Afrika na hata nje ya bara hili.

 

Pamoja na hayo kuna baadhi ya mila ambazo zimepitwa na wakati, ama kutokana na kuwa kandamizi au kwa sababu ya athari kubwa kwa baadhi ya wanajamii katika maisha yao yote.

 

Na ndiyo maana athari zake zimekuwa zikipigiwa kelele na serikali pamoja na mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali na wadau wenye mapenzi mema ili zitokomezwe kabisa.

 

Kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali na wadau kuhakikisha mila zisizofaa haziendelei na wanaoziendeleza wanachukuliwa hatua za kisheria, mila hizi sasa zinafanyika kwa usiri mkubwa.

 

Mojawapo ya Mila hizo ni ya ukeketaji (FGM), inayohusisha kuondolewa kwa sehemu au jumla ya sehemu za siri za msichana.

 

TAKWIMU

 

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kwamba kati ya wasichana na wanawake milioni 100 na 140 wamefanyiwa ukeketaji, na wasichana milioni mbili zaidi wako katika hatari ya kukeketwa kila mwaka.

 

WHO inasema wengi ya wanawake na wasichana hawa wanaishi katika nchi 28 za Afrika, Tanzania ikiwamo, chache za Mashariki ya Kati na Asia, Jumuiya ya wahamiaji barani Ulaya, Australia, New Zealand, Marekani na Canada.

 

Na ndiyo maana Umoja wa Mataifa (UN), ukaiweka Februari 6 ya kila mwaka kuwa siku ya kutokomeza aina zote za ukeketaji kwa watoto wa kike na wanawake duniani.

 

UN iliweka siku hii kwa kuzingatia kuwa kitendo hicho pamoja na kukiuka haki za binadamu kinakwamisha harakati za maendeleo ya kundi hilo wakati huu ambapo dunia inasaka si tu ulinzi wa kila binadamu, pia kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu.

 

Hata hivyo, pamoja na juhudi hizo, bado kuna makabila au baadhi ya watu ambao wanahama na mila hizo zisizofaa ikiwamo ya ukeketaji kila waendako.

 

KWA NINI?

Wanahama nayo kwa kuamini kuwa wasipofanya hivyo watapata laana au majanga mbalimbali.

 

Yapo makabila nchini yanayojulikana kwa kuendeleza mila hiyo ingawaje sasa kwa kujificha na hivyo kuja na mitindo tofauti ya ukeketaji.

 

Kuna makabila ambayo sasa yanakeketa watoto wa kike katika umri wa kati, moja kwa moja wakiandaliwa kuolewa.

 

Lakini wapo wanaolewa kwenye familia fulani wakiwa hawajakeketwa ambapo hulazimishwa kwanza kukeketwa ili wakubalike katika familia walizoolewa.

Aidha, kuna wanaokeketwa wakiwa watoto na wengine kwenye madarasa ya awali.

 

Mikoa wa Kanda ya Kati kwa maana ya Dodoma na Singida ni miongoni mwa mikoa ambayo bado ukeketaji unaendelea kufanyika.

 

Katika mikoa hii, ukeketaji unafanyika kwa watoto wachanga lakini kwa siri kubwa, kwa ushirikiano baina ya ngariba, wazazi wa mtoto na mama mkwe kwa madai ya kutimiza mila hiyo.

 

SHIRIKA LA ESTL

 

Mkurugenzi wa Shirika la Empower Society Transform lives (ESTL), Joshua Ntandu, ameueleza muungano wa Asasi zisizo za kiserikali zinazopinga ukeketaji zilipokutana jijini Dar es Salaam, kuunda umoja wa kupambana na suala hilo hivi karibuni, namna ukeketaji unavyofanyika mkoani Singida.

 

Anasema Mkoa wa Singida una makabila makubwa mawili ambayo ni Wanyaturu na Wanyiramba, yote yakitekeleza mila hiyo kwa usiri mkubwa.

 

Ntandu anabainisha kwamba ukeketaji katika mikoa hiyo hufanywa na wanawake wanaoamini kuwa ndiyo namna sahihi ya kutibu ‘lawalawa’.

 

“Hiyo ni baada ya kuona serikali inafuatilia kwa karibu ili ichukulie hatua wanaoendeleza mila hii potofu,” anasema.

 

Anasema utafiti uliofanywa na shirika hilo umebaini kuna usiri mkubwa kwa kuwa jamii hizo zinaamini ukeketaji unatibu ugonjwa wa lawalawa, ambao kihalisia unatokana na uchafu kwenye sehemu za siri za mtoto wa kike.

 

“Wazazi wengi wanaamini kwamba wakikata sehemu za siri za mtoto, wanatibu ugonjwa huo… hata hivyo kiuhalisia si kweli kwani huo ni ugonjwa wa njia ya haja ndogo unaosababishwa na uchafu kwenye sehemu hizo na tiba yake si kukeketa mtoto,” anasema.

 

KINACHOFANYIKA

 

Ntandu anasema ukeketaji hufanywa na ngariba ambaye amefuga ukucha mrefu wenye makali kwa ajili ya kukata kinyama husika pale mtoto anapozaliwa.

 

Mkurugenzi huyo anabainisha kwamba wanakeketa watoto wakiwa wachanga kwa kuwa nyama yao inakuwa bado laini.

 

“Ngariba anafuga ukucha mdogo ambao ni kwa ajili ya kazi hiyo na wakati mwingine anatumia kisu maalum cha asili,” anasema na kuongeza:

 

“Kwa kutumia ukucha uliochongwa, hukata kidogo kidogo hadi kukimaliza kinyama kilichopo kwenye eneo la siri.”

 

KISHA TUMBAKU AU MASIZI

 

Ntandu anasema baada ya ngariba kufanya kazi yake, kidonda hupakwa tumbaku au masizi kama namna ya kukiponya.

 

“Kutokana na jitihada za serikali kuingilia kati na kuwakagua watoto kila wanapopelekwa kliniki, sasa wamekuja na mbinu nyingine,” anasema na kuongeza:

 

“Wazazi katika makabila haya

huvizia na kuitekeleza mila hii nyakati ambazo watoto wamemaliza chanjo zote au wakati wanajiandaa kwenda shule ya awali ama nyakati za likizo, hasa ya mwezi Desemba, ambacho huwa ni kipindi cha baridi.”

 

TIBA YA KIDONDA CHA UKEKETAJI

 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, vidonda vya ukeketaji hutibiwa kwa usiri mkubwa nyumbani na kuwa wapo baadhi ya waathirika ambao hupoteza maisha kutokana na kuoza sehemu za siri.

 

MKOJO WA BIBI KIZEE

 

“Tiba inafanywa na bibi kizee ambaye ameshaacha kufanya mapenzi… hukojoa mkojo wake ambao huhifadhiwa kwenye kibuyu kwa muda wa siku saba… baada ya hapo mkojo huo hupakwa kwenye kidonda cha mtoto husika kila siku,” anasema.

 

Ntandu anabainisha kwamba wakati mwingine wazee wa kike saba (mabibi) hukojoa mikojo yao ambayo kwa pamoja huhifadhiwa kwenye kibuyu kwa siku saba.

 

“Hiyo ndiyo inakuwa tiba ya vidonda vitokanavyo na ukeketaji kwa watoto tofauti tofauti waliokeketwa wakati huo,” anasema.

 

Mbali na madhara ya kuoza, Ntandu anabainisha kwamba watoto wengine hukumbana na maumivu makali.

 

MATIBABU HOSPITALINI

 

Anasema pamoja na madhara hayo, bado wazazi huwa hawawapeleki hospitali watoto wao walioathirika kwa hofu ya kukumbana na mkono wa sheria.

 

“Mbaya zaidi nyama zinazokatwa kutoka kwa watoto baada ya kukeketwa huhifadhiwa na nyingine hutupwa kwenye zizi la mifugo kwa imani ni chanzo cha kupata utajiri, jambo ambalo si kweli kwani familia husika huendelea kuwa maskini,” anasema.

 

MKURUGENZI HALMASHAURI

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ikungi mkoani Singida, Justice Kijazi, anathibitisha kuwepo kwa vitendo hivyo.

 

Hata hivyo anabainisha kwamba serikali inachukua hatua mbalimbali kukomesha mila hiyo ikiwa ni pamoja na kushirikiana na asasi zisizo za kiserikali kuelimisha jamii.

 

Kijazi anasema kuna mashirika yasiyo ya kiserikali yanayoelimisha jamii juu ya umuhimu wa kuacha mila ya ukeketaji, na kwamba halmashauri kupitia idara ya maendeleo ya jamii inatoa elimu kuhusu madhara kwa watoto wa kike wanapokeketwa.

 

“Tunatoa elimu kwenye jamii na shuleni kuelimisha wazazi na watoto wenyewe kukataa kufanyiwa ukeketaji,” anasema na kuongeza:

 

“Kwa kuanzia kuna kata za Puma, Ikungi, Isuna na Man’gonyi ambako kuna shirika linatoa elimu kwa wanawake, ngariba na familia mbalimbali juu ya madhara ya ukeketaji pamoja na kuunda kamati za ukeketaji na sasa wameacha,” anasema.

 

Kijazi anasema wamelitaka shirika hilo kujitanua na kuzifikia kata zote 28 ili wapeleke elimu na kuwaeleza mangariba madhara ya ukeketaji.

 

“Lakini tunatoa pia kipaumbele kwa mangariba wapate shughuli za kufanya   zitakazowaingizia kipato,” anasema.

 

VIKUNDI

 

Mkurugenzi huyu anasema kwamba katika halmashauri hiyo kuna vikundi vimeundwa ambavyo vinapewa mikopo na miongoni ni vikundi vya mangariba ambao kupitia mikopo hiyo wanafanya miradi ya kuwaingizia kipato.

“Lakini tumeanzisha vilevile mpango wa kuwakagua watoto wanapozaliwa na wanapopelekwa kliniki na wanapobainika kukeketwa, wazazi huchukuliwa hatua za kisheria,” anasema.

Habari Kubwa