Ukeketaji wanasiasa lawamani

15Feb 2020
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Ukeketaji wanasiasa lawamani

VITENDO vya ukeketaji bado ni tatizo linaloendelea kujitokeza kwenye baadhi ya mikoa hapa nchini, licha serikali kuweka sheria kali kusaidia kutokomeza ukatili huo.

Baadhi ya wawakilishi kutoka mashirika ya kimataifa, wakifuatilia kongamano hilo: PICHA: SABATO KASIKA

Inaelezwa kuwa miongoni mwa watu wanaochangia kuendelea kuwapo kwa ukeketeaji katika maeneo mbalimbali nchini ni baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakiupigia debe kichinichini kwa maslahi yao binafsi.

Velerian Mgani, ambaye ni Meneja Mradi wa Shirika la Kutokomeza Ukeketaji na Mimba za Utotoni (ATFGM) kutoka Tarime mkoani Mara, ndiye aliyotoa tuhuma hiyo baada ya kufanya uchunguzi wa kina.

Hayo yamefichuka wakati wa kongamano la maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukeketaji Duniani, lililofanyika Februari 6 mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo liliandaliwa an Umoja wa Ulaya nchini (EU), likiratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Maendeleo (UNFPA) na kushirikisha wadau mbalimbali wa kupinga ukatili huo.

Mgani aliwashukia wanasiasa na kusema wanachangia kukwamisha juhudi za kumaliza tatizo hilo katika jamii, kutokana na kile anachodai kuwa wanafanya hivyo kwa kuhofia kung’olewa madarakani.

WANAFANYAJE?

Meneja huyo anasema, kuna jamii bado zinakumbatia mila potofu na kwamba zinapopata wanaoziunga mkono, hasa wanasiasa zinaendelea kuwepo na kukwamisha juhudi za kumaliza tatizo hilo.

“Wanasiasa wana ushawishi mkubwa katika jamii na waposema jambo wanasikilizwa na ndivyo inavyotokea kule kwetu, kwani wapo baadhi yao katika mikutano wanatamka wazi kwamba mila za ukeketaji zipo tangu enzi na enzi hivyo wananchi waachwe waendelee nazo,” anasema Mgani.

Anafafanua kuwa kwa mazingira hayo, baadhi ya koo zimeendelea kukeketa watoto wa kike kana kwamba ni jambo la kawaida na kumbe ni ukatili wa hali ya juu kwa wasichana na wanawake.

“Nimewahi kusikia mwanasiasa akisema, ukeketaji umekuwapo hata kabla ya Yesu Kristo, hivyo wananchi waachwe waendelee na utamaduni wao waliouzoea kwa miaka yote, na wanafanya hivyo ili kupata kura,” anasema.

Anasema, umefika wakati wanasiasa wakemewe, wasitafute kuungwa mkono kwa kukumbatia ukatili badala yake watafute kura kwa njia nyingine, na siyo kuhimiza kuendelea kwa mila potofu kama hizo.

Anasema, baadhi ya jamii bado ziko nyuma, hazina uelewa kuhusu madhara ya ukeketaji, na kwamba hizo ndizo wanasiasa wanazitumia kuzishawishi ziwaunge mkono kwa vile na wao wanazitetea, ili ziendelee kukeketa.

NYUMBA SALAMA

Inaelezwa kuwa elimu ya kupinga vitendo vya ukeketaji itolewe, lakini nyumba salama ni muhimu ziwe nyingi zaidi zinasaidia kuokoa watoto wa kike dhidi ya vitendo hivyo.

Akichangia mada katika kongamano hilo, Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Hope for Girls and Women Tanzania la Mugumu Serengeti mkoani Mara, Rhobi Samwelly, anasema nyumba hizo zimekuwa kimbilio la mabinti wengi.

“Ninasema hivyo nikiwa na mfano hai. Shirika letu limeokoa wasichana 1807 kwa kuwalea katika nyumba salama tunazomiliki ikiwamo ya Mugumu na Butiama, hivyo nyumba hizo zijengwa nyingi zaidi,: anasema Rhobi.

Anasema, serikali na wadau wa kupinga ukatili imejitahidi kutoa elimu, ili jamii iachane na vitendo hiyo, lakini bado vipo, hivyo nyumba salama zijengwe za kutosha kote nchini, ili zitumike kuokoa watoto wa kike.

" Siyo kwamba ninapinga elimu, bali ninachoshauri ni kujenga nyumba salama nyingi zaidi, kwani zimekuwa kimbilio la watoto wanaokwepa ukeketaji kutoka nyumbani kwao na kuwa salama zaidi,” anasema.

Anasema, Desemba mwaka jana, nyumba salama ya Butiama ilipokea zaidi ya wasichana kutoka Tarime waliojisalimisha baada ya kukimbia vitendo vya ukeketaji ambavyo wangefanyiwa mwezi huo.

“Desemba huwa ni mwaka wa ukeketaji, ulipotimia tu na wao wakakimbia kuja kwetu, tuliwatunza na kisha tunafanya mawasiliano na wazazi wao kwa kushirikiana na serikali, hatimaye wakarudi kwao,” anasema.

Rhobi anasema, kabla ya kuwarejesha, shirika hilo lilijenga uhusiano na wazazi Wa mabinti hao kuwaambia madhara ya ukeketaji wakakubali, ukawekwa utaratibu maalum wa kuwapokea huku wakiwa wamehakikishiwa usalama na sasa wanaendelea na masomo.

KUWATIA MOYO

Mwakilishi Mkazi wa UNFPA Tanzania, Jacqueline Mahon, anasema, watoto wa kike wanaokimbia ukeketaji lazima wapongezwe na kutiwa moyo.

Anasema wanatakiwa kuwa mabalozi wa kusaidia kupinga vitendo vya ukeketaji katika jamii na kwa watoto wenzao mashuleni.

Anasema, UNFPA inaendelea kusaidia juhudi za serikali na taasisi za kijamii kuendeleza mapambano ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto hadi kufikia sifuri mwaka 2030.

“Kwa hiyo hawa watoto wa kike wanaokimbia ukeketaji, wanatakiwa kuwa mabalozi wa kusaidia kupinga vitendo vya ukeketaji katika jamii, hivyo ni muhimu watiwe kwa uamuzi wao huo,” anasema Mahon.

Wakati mwakilishi huyo akisema hayo, Mratibu wa Dawati la Jinsia na Watoto, kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, SSP Faidha Suleiman, anasema, ukeketaji ni kosa la jinai.

Anasema jeshi linafanya kazi kwa karibu na mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali yanayopinga ukatili wa kijinsia na limekuwa likipata taarifa mbalimbali zinazohusu vitendo hivyo na kuvikabili mapema.

"Mwaka huu unagawanyika kwa mbili, hivyo tunajua kwamba kwa mkoa wa Mara kutakuwa na ukeketaji, nasi tumeshajipanga kukabiliana na tukio hilo kuhakikisha hakuna nayekeketwa,” anasema Faidha.

Anasema, polisi ina mkono mrefu na ina watu wake ndani ya jamii, hivyo ana uhakika wazazi watakaothubutu kukeketa watoto wao, watakumbana na mkondo wa sheria, na kuwataka waache mara moja.

Habari Kubwa