Ukimya kutawala migogoro EAC, dalili za kushindwa kwa jumuiya?

12Jun 2019
Mashaka Mgeta
DAR
Nipashe
Ukimya kutawala migogoro EAC, dalili za kushindwa kwa jumuiya?

NI kama hakuna kinachoendelea katika kupata suluhu ya migogoro ‘inayozitafuna’ baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Kusini (EAC), hususani kati ya Rwanda dhidi ya Burundi na Uganda.

Kwa hali ilivyo sasa, mataifa wanachama wa EAC yaliyo katika migogoro ya kidiplomasia yanaendelea ‘kujitenga na maadui’ zao, yakitafuta jinsi yanavyoweza kukuza uhusiano hasa unaolenga nyanja za kiuchumi.

 

Wakati hayo yakiendelea, EAC inaendelea na mchakato utakaozifikisha nchi wanachama kuwa shirikisho moja.

 

Kushamiri  kwa migogoro hiyo hakutoi taswira nzuri kwa hali ya baadaye ya EAC. Tayari nchi kama Rwanda inayoguswa kuwa ‘kiini’ cha migogoro hiyo, ikifungua uhusiano zaidi na mataifa mengine ya ukanda wa Kusini mwa Afrika, hususani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

 

 

Migogoro inayoendelea ‘kuitesa’ EAC inajumuisha ule uliodumu kwa takribani miaka minne sasa ukizihusisha nchi za Burundi na Rwanda. Burundi ‘ilishaapa’ kwamba Rwanda haina sifa za kuwa mshirika wake wa maendeleo.

 

Unapoisoma dira ya EAC inaeleza kwamba ni kutanua wigo wa ushirikiano kati ya nchi wanachama pamoja na mambo mengine, masuala ya siasa, uchumi na kijamii kwa maslahi ya pande zote.

 

Hivyo migogoro ya kidiplomasia kama huo wa Rwanda na Burundi inazidi kuongeza changamoto katika kufikia azma hiyo.

 

Jamal Juma ni mwanataaluma wa ushirikiano wa kimataifa, anasema nchi zilizo wanachama katika ushirikiano wa kikanda zinapoibua na kuweka bayana mgogoro kati yao, zinafifisha (kimantiki) malengo, mipango na mikakati inayokusudiwa, ili ziweze kuwa na nguvu kubwa za kiuchumi, kiulinzi na kijamii.

 

“Huwezi kuwa na jumuiya imara katika ukanda husika wakati wanachama wake hawazungumzi lugha moja, hawapo pamoja bali wanatengana kwa migogoro hasa ya kidiplomasia,” anasema Juma anapohojiwa juu ya mtazamo wake kuhusu kudorora kwa ushirikiano wa baadhi ya nchi wanachama wa EAC.

 

 

Ikumbukwe kwamba katika mgogoro wa kidiplomasia uliowekwa wazi kati ya mataifa hayo, Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, amekuwa akimshutumu Rais Paul Kagame wa Rwanda na utawala wake kwa kuihujumu Burundi.

 

Rais Nkurunziza akasema kujiingiza kwa Rwanda katika masuala ya ndani ya Burundi kulisababisha athari tofauti ikiwamo kukosekana kwa amani na utulivu nchini humo.

 

Lakini serikali ya Rwanda imekuwa ikakanusha madai hayo mara kwa mara na kwa upande mwingine, ikieleza pia shutuma zake dhidi ya Burundi, kama ambavyo imekuwa ikifanya kwa mataifa mengine yaliyo kwenye mgogogro kama huo.

 

Yapo matukio kadhaa ambayo Burundi imekuwa `ikiinyooshea kidole’ Rwanda kwamba inahusika ama kuwa karibu na uratibu na utekelezaji wake.

 

Kwa mfano ni kuhusiana na uhasama uliopo kati ya utawala wa Rais Kagame wenye Makao Makuu yake jijini Kigali na ule wa Rais Nkurunziza wenye Makao Makuu aliyoyahamisha kutoka Bujumbura kwenda Gitega, ulikolea zaidi mwaka 2015.

 

Wakati huo, Rais Nkurunziza alikuwa katika mchakato wa kuingia katika awamu ya tatu ya utawala, hivyo kuzua utata kiasi cha kusababisha maandamano nchini mwake, na baadaye kunusurika katika mapinduzi ya kijeshi yaliyozimwa.

 

Mapinduzi hayo yalifanyika Mei, 2015 wakati Rais Nkurunziza akiwa jijini Dar es Salaam kushiriki kikao cha usuluhishi wa mzozo wa kisiasa uliohusu kutaka kuongeza muda wa kuiongoza Burundi.

 

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Usalama wa Burundi ‘aliyetumbuliwa’ na Rais Nkurunziza Februari, 2015, Meja Jenerali Godefroid Niyombare, alitangaza mapinduzi hayo kupitia kituo binafsi cha redio cha Bonesha FM.

 

Ikulu ya Rais Nkurunziza ilijibu baadaye kwamba mapinduzi hayakufanikiwa na mhusika alikuwa akisakwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

 

Pia, kumewahi kutokea mapigano ya kutumia silaha za moto kufuatia mauaji ya raia na wapiganaji kwenye maeneo ya mpakani mwa nchi hizo.

 

Hayo ni miongoni mwa matukio ambayo Burundi inaihusisha Rwanda kiasi cha kuifanya serikali ya Rais Nkurunziza, kutamka wazi kwamba Rwanda imekosa sifa za kuendelea kuwa mshirika wake.

 

Na kwa hali hiyo, Burundi ikaiomba EAC kuitisha kikao cha dharura kwa lengo la kupata suluhu ya mzozo huo ambao hata hivyo hakikufanyika.

 

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Burundi, Uganda na Rwanda zipo katika historia inayozipitisha kutoka kwenye uhusiano mwema na ule unaowakaribisha kuingia katika vita.

 

Ni ‘urafiki wa mashaka’ ukijikita katika historia inayoonyesha kuwa Rais Kagame amewahi kuwa mmoja wa ‘nguzo’ zilizofanikisha kilichokuwa kikundi cha uasi kumuingiza madarakani Rais Yoweri Museveni mwaka 1986.

 

Kwa upande wake, Rais Museveni pia anatajwa kuwa mshirika wa karibu aliyeibuka baadaye na kukisaidia kilichokuwa kikosi cha uasi cha Kagame (kabla ya kuwa Rais) kuingia madarakani.

 

Kwa maana nyingine, viongozi hao wawili wenye historia ya kutokea jeshini na kupigana vita vya msituni, wanajuana kwa muda mrefu na pia kusaidiana katika harakati za kisiasa na uongozi kwa mataifa yao.

 

Lakini wawili hao wamejikuta mara kadhaa wakiwa katika mgogoro unaokuwa kufikia hatua ya kuhatarisha uhusiano wa wananchi wao, umoja na mshikamano ndani ya EAC.

 

Hivi karibuni, Uganda iliishutumu serikali ya Rais Kagame kwa kuzuia malori ya mizigo na magari mengine kutoka nchini mwake kuingia Rwanda.

 

Pia Uganda ikasema serikali hiyo iliwazuia raia wake wasivuke mpaka kuingia nchini humo (Uganda), wakati ambapo mataifa hayo jirani yanaingia kwenye mgogoro.

 

Utawala wa Rwanda uliyazuia maroli na magari mengine kutoka Uganda kuingia nchini humo, Msemaji wa Serikali ya Rais Museveni, Ofwono Opondo, aliwaambia waandishi wa habari.

 

Hata hivyo, serikali ya Rais Kagame kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi, Richard Sezibera, ilikanusha shutuma hizo na kufafanua kwamba magari hayo yalielekezwa kupitia mpaka wa Kagitumba uliopo Kaskazini mwa nchi hiyo ili kupisha ujenzi wa barabara yenye shughuli nyingi katika mpaka wa Gatuna.

 

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa kwa takribani muongo mmoja tangu vikosi vya majeshi kupigana hadi kumwaga damu kwenye jiji la Kisangani, Mashariki mwa DRC, Uganda na Rwanda wamekuwa katika ‘urafiki wa mashaka’.

 

Hata hivyo, mzozo huo ulichukua sura tofauti hadi Julai 2011 ambapo Rais Museveni alifanya ziara iliyowashangaza wengi kwenda Rwanda na kutumia siku kadhaa, akiwa na timu ya wataalamu wake walioingia mikataba kadhaa ya ushirikiano kati ya nchi mbili hizo.

 

 

UENYEKITI WA KAGAME EAC

 

Devotha Masha, anayejitambulisha kuwa mfuatiliaji wa masuala ya EAC, anasema kwa hali ilivyo sasa ni vigumu kufikiria kupatikana kwa suluhu ya migogoro ndani ya jumuiya hiyo, hasa inayozihusu Rwanda dhidi ya Burundi na Uganda.

 

Masha anasema kiwango cha mgogoro kati ya mataifa kinapodhihirika kupitia kwa marais wa nchi husika kinahitaji zaidi utashi wa kisiasa na kujitenga na ‘upande’ ili kupata suluhu ya kudumu.

 

Anasema hali hiyo haionekani kwa EAC kutokana na namna uongozi ulivyo, Rais Kagame akiwa Mwenyekiti wakati huo huo mhusika muhimu katikati ya migogoro kidiplomasia inayoitikisa jumuiya hiyo.

 

Rais Kagame ‘alichukua’ nafasi hiyo kutoka kwa mtangulizi wake, Rais Museveni wa Uganda ambao pia mataifa yao yapo katika mgogoro.

 

Ingawa ni hivyo, taarifa zinazodaiwa kutoka ndani ya sekretarieti ya EAC zikaripotiwa na gazeti la East African kuwa jumuiya hiyo ilitambua ugumu uliopo kwa Rais Kagame kuchukua nafasi hiyo hasa baada ya kuwekewa pingamizi na Burundi, lakini hatimaye uteuzi wake ukapitishwa ‘kwa mbinde’.

 

Francis Chota, mhitimu wa shahada ya uhusiano wa kimataifa anasema isingefaa kwa Rais Kagame kuchukua nafasi hiyo kwa vile kunaweka mazingira ya kupunguza tija katika kupata suluhu ya migogoro iliyopo.

 

Mwanaharakati wa masuala ya migogoro ya kijamii, Silvanus Isdory anasema ni vigumu kupata suluhu ya mzozo unaohusisha mmoja wa upande kuwa na nguvu za kiutawala na uongozi.

 

“Katika utatuzi wa mgogoro wowote, ili upate suluhu nzuri ya kudumu, pande zinazopingana zisiwe katika mamlaka ya utawala ama uongozi, na ndio maana hata kiongozi anaposhutumiwa, ni vema akajizulu kupisha uchunguzi, ndivyo ilivyo katika migogoro pia,” anasema.

 

Anasema ingawa EAC inaweza kuwa na mifumo ya kitaasisi inayoweza kukabiliana na kuwapo katika uongozi kwa Rais Kagame na kushughulikia mzozo ambao serikali yake inashutumiwa, lakini mazingira ya kupata suluhu ya kudumu hayatakuwa na wigo mpana kufikia lengo.

 

Vyanzo vingine vimewakaririwa na vyombo mbalimbali vya habari na mawasiliano vikieleza kuwa kutokana na mzozo unaoendelea kati ya Burundi na Rwanda, kuna uwezekano kuvunjika kwa EAC kama ilivyotokea mwaka 1977.

 

Lakini Katibu Mkuu wa EAC, Libérat Mfumukeko, anasema kuvunjika kwa jumuiya hakuwezi kutokea tena na kufafanua kuwa awali (1977) ilikuwa ‘nyakati za giza’ tofauti na sasa ambapo jumuiya imepiga hatua kubwa katika kujiimarisha kwake.

 

Lakini swali bado linabaki kuwa, je ukimya unaojitokeza kwa migogoro inayozikabili nchi wanachama wa EAC, utarajiwe kuibuka na mafanikio katika kuidhibiti ama itakuwa mwanya wa mpasuko zaidi katika jumuiya hiyo?

 

 

Makala haya yameandikwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali. Mwandishi wake anapatikana kupitia simu namba +255 754 691540

Habari Kubwa